25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

LUKUVI AMTIKISA MAKONDA

*Azuia ekari 1,500 alizopewa na mfanyabiashara wa kiasia


Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amemtikisa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kuzuia ekari 1,500 za ardhi alizopewa na Kampuni ya Azimio Housing Estate (Ahel) na kusema kuwa ni mali ya Serikali.

Uamuzi huo wa Serikali umekuja siku chache baada ya Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Mohamed Iqbal kutangaza kumpa Makonda ekari hizo zilizoko katika eneo la Kisarawe II, Wilaya ya Kigamboni ili kuendeleza viwanda vidogo vidogo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Lukuvi alisema Makonda alidanganywa kwa sababu wananchi walishashinda kesi mahakamani ambayo ilifunguliwa na Iqbal.

“Eneo lile ni la Serikali si la yule mtu aliyejitangaza anampa Makonda na kwa sababu amemdanganya na mimi ndiye msimamizi wa ardhi, nitamsaidia Makonda kuchukua hatua ili watu wasijipendekeze kusafisha maovu yao kwa kutumia migongo ya viongozi.

“Hadi siku ile (Jumanne iliyopita) alipokuwa anajipendekeza kwa Makonda, ardhi ile haikuwa yake, wananchi walishashinda mahakamani kwa sababu hakuwa na vielelezo.

 “Ukimdanganya Mkuu wa Mkoa umeidanganya Serikali, Makonda hakuomba ile ardhi ila yeye (Iqbal) ndiye alikwenda kumgawia na amemgawia akijua kwamba alishashindwa,” alisema Lukuvi.

Alisema tayari Serikali imeanza kuwashughulikia wananchi ili wapate haki yao na eneo la viwanda libaki na kwamba wazo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo wazo lao.

Lukuvi alisema eneo hilo litabaki kuwa la viwanda baada ya kuondoa matumizi mengine ya wananchi na kwamba eneo jingine litakuwa la dampo.

 

JINSI ALIVYOPEWA

Februari 21, mwaka huu mfanyabiashara huyo alisema aliamua kutoa eneo hilo kuunga mkono juhudi za Rais Dk. John Magufuli ambazo zinalenga kukuza sekta ya viwanda nchini.

“Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliniomba nisaidie katika suala hili la kuendeleza viwanda na mimi nimekubali kutoa ardhi kwa sababu wafanyabiashara ndogo ndogo wanakua na ili waweze kufanikiwa zaidi ni lazima kuweka mazingira mazuri ya kufanyia shughuli zao,” alisema Iqbal.

Kwa upande wake, Makonda alisema eneo hilo litagawanywa kwa wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba wanatarajia ujenzi utaanza Aprili.

“Changia ukijijua mikono yako ni misafi, kwa sababu ukichangia wakati mikono yako ni michafu, hiki si kichaka cha kujificha. Mimi bado nitakushughulikia tu kwa sababu safari yangu ya kwenda mbinguni bado haijakamilika,” alisema Makonda.

 

RIPOTI YA CAG

Kampuni ya Azimio Housing Estate ilihusishwa katika kashfa ya ubadhirifu wa fedha na ukiukwaji wa taratibu na sheria katika usimamizi wa miradi kadhaa ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Ilitakiwa kuendeleza ekari 20,000 za ardhi zilizopo Kigamboni, lakini baada ya NSSF kufanya tathmini, ilibaini kuwa ekari zilizopatikana ni 3,503 tu.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2014/2015 inaonyesha kampuni hiyo ilishindwa kutoa hatimiliki za ardhi ambayo iliahidi kutoa kama uchangiaji wa mtaji licha ya NSSF kulipa asilimia 20 ya fedha kama mtaji ambazo zilikuwa kwenye hatari ya kupotea.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara, aliiambia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwa mradi wa mji wa kisasa wa Kigamboni maarufu kama Dege Ecco Village uligubikwa na utata.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, hadi mradi huo unasimama Februari mwaka jana, shirika hilo lilikuwa limetoa Dola za Marekani milioni 129 na Azimio ilikuwa imetoa Dola milioni 5.5 na ekari 300 tu.

 

KIINI CHA MGOGORO

Vyanzo mbalimbali vimelieleza MTANZANIA kwamba mgogoro huo umedumu kwa zaidi ya miaka 10 na kabla ya kufikishwa mahakamani, ulishashughulikiwa na Manispaa ya Temeke, Tume ya Rais ya Kushughulikia Migogoro na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi bila mafanikio.

MTANZANIA lilifanikiwa kupata nakala zabarua kadhaa zinazoonyesha namna Serikali ilivyoshughulikia mgogoro huo.

Barua ya Kamishna wa Ardhi, C. Binali, ya Februari 26,  mwaka 2007 inaonyesha mgogoro huo ulishashughulikiwa na Tume ya Rais ya Kushughulikia Migogoro chini ya Meya wa Manispaa ya Temeke wa wakati huo.

“Manispaa wamebainisha kwamba mwenyekiti na diwani wa kata yenu walifanya mkutano ambapo ilibainika mliuza maeneo yenu kwa ridhaa yenu wenyewe na si kwamba mlinyang’anywa kama mlivyoeleza katika barua yenu,” ilisema sehemu ya barua hiyo kujibu malalamiko ya Mohamed Kandamba na wenzake.

Barua nyingine ya Mei 9, mwaka 2008, iliyoandikwa na Katibu wa Waziri, I. Mbagule kwenda kwa Maduhu Pius na wenzake, inaonyesha kwamba Iqbal hakuwa mwekezaji bali mfanyabiashara.

“Baada ya uchunguzi wa kina kuhusu malalamiko yenu, Mhe Waziri amebaini kwamba Iqbal aliyanunua mashamba ya wakazi wa maeneo yanayolalamikiwa baada ya wenye mashamba kumuomba ayanunue,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

 

KUHAMIA DODOMA

Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi alisema viongozi wote wakuu watahamia mkoani Dodoma na kwamba huduma zilizokuwa zinaendelea kutolewa kwenye kanda zimeimarishwa zaidi na watu wa Mkoa wa Pwani watahudumiwa katika Kanda ya Dar es Salaam.

“Leo (jana) tumegawa na magari ambayo yatarahisisha utendaji kazi kwenye kanda, nia yetu ni kuimarisha hizi kanda ziweze kutoa huduma na wafanyakazi wengi tumewagawa kwenye kanda. Nitapanga ratiba ya kutembelea mikoani ikiwamo Dar es Salaam katika kutatua kero mbalimbali,” alisema Lukuvi.

Kuhusu ukaguzi wa ardhi, alisema baada ya kupata mafanikio makubwa katika ukaguzi wa mashamba, sasa wameelekeza nguvu katika ukaguzi wa mashamba na viwanja vya mijini.

“Tumegundua watu wengi wanamiliki mashamba mijini, kama Kigamboni huko wana ekari 5,000 lakini wana makaratasi tu hawana hati wala ‘offer’, sasa hawalipi kodi ya ardhi. Hivyo kila mtu mwenye ardhi yoyote, iwe alipewa kindugu, kimila ama kwenye Serikali za mtaa ajisalimishe mwenyewe kwa ofisa ardhi ili aorodheshe ardhi aliyonayo. Sisi tutaanza kumtoza kodi kulingana na tamko lake,” alisema.

Alisema ikifika Juni kama kutakuwa na ardhi haijasajiliwa Serikali itaitaifisha na muhusika hatalipwa fidia.

“Tunaanza kushtuka kwamba kuona pengine hawa wenye fedha chafu wanazitumia, wanazisafisha kwa kununua ardhi, kujenga majengo, tunataka wasajili kama kweli wamenunua kihalali,” alisema Lukuvi.

Alisema hapa nchini ardhi nyingi mijini zinamilikiwa na watu wengi wasiokuwa na hati kitendo kinachoikosesha mapato Serikali kutokana na watu hao kutolipa kodi.

“Watu wote wanaomiliki ardhi kwa karatasi ambazo si za Serikali nataka walipe kodi kama watu wengine, ili wapate ulinzi wa Serikali lazima wajiorodheshe,” alisema.

Pia alisema wale waliokuwa na ofa wajitokeze kuzirudisha ili waweze kupatiwa hati kwani kuanzia sasa ofa hazitolewi tena.

Kuhusu makazi ambayo hayajapimwa, alisema wamebuni utaratibu wa kurasimisha makazi kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo husika ambapo hugharamia na kutengenezewa michoro ya kupitisha miundombinu na huduma nyingine za kijamii kisha wanatengenezewa hati.

Kwa mujibu wa Lukuvi, mpango huo sasa umeanza kutekelezwa katika eneo la Chasimba, Makongo, Kimara na kwamba kuanzia Julai mwaka huu kila mtu mwenye nyumba ambayo iko katika eneo ambalo halijapimwa naye atakuwa na haki ya kulipa kodi.

“Tunapanga vizuri nyumba zilezile ambazo zilijengwa bila kupimwa, lakini wananchi angalau wanapata kuwa na barabara ya pamoja, eneo la kujenga shule na zahanati kwa makubaliano yao. Kama eneo limejaa wanakubaliana wenyewe nani abomoe ili ijengwe shule,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles