27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

JAJI: KUMNYIMA LEMA DHAMANA NI KUNAJISI SHERIA

Na JANETH MUSHI,-ARUSHA


JOPO la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, limefuta rufaa mbili za Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) dhidi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), baada ya mawakili wa Serikali kuieleza mahakama kwamba hawana nia ya kuendelea nazo.

Kutokana na hali hiyo, waliiomba mahakama kufuta rufaa hizo zilizokuwa zinahusu dhamana ya mbunge huyo.

Rufaa hizo namba 9 na 10 za mwaka 2017, jana zilipangwa kuanza kusikilizwa mbele ya majaji Benard Luanda, Mussa Kipenka na Stella Mugasha.

Katika kesi hiyo, upande wa Serikali uliwakilishwa na mawakili Faraja Nchimbi na Paul Kadushi, huku Lema akiwakilishwa na Peter Kibatala na Adam Jabir.

Kabla ya rufaa hiyo kuanza kusikilizwa, wakili Nchimbi aliomba kuwasilisha ombi mahakamani hapo akidai kuwa baada ya kuipitia kwa kina, kwa sababu zisizozuilika, hawana nia ya kuendelea na rufaa namba 9.

“Baada ya kupitia kwa kina DPP ameona hana nia ya kuendelea na rufaa hii, anaomba kuiondoa mahakamani na tunaomba mahakama kuifuta rufaa hii kwa kanuni ya 4 ya mahakama ya mwaka 2009,” alisema Nchimbi

Alisema uamuzi wa kuondoa rufaa hiyo, ulifikiwa Februari 24, mwaka huu ila kutokana na muda kuwa ulishaisha, walishindwa kupeleka notisi ya kuiondoa.

Baada ya hoja hizo, wakili wa upande wa utetezi, Kibatala, alikubaliana na ombi hilo akisema hawana pingamizi kwani rufaa ilikuwa imefunguliwa, hivyo wakaiomba mahakama hiyo kuondoa kwenye rekodi pingamizi za awali ambazo waliziwasilisha mahakamani hapo.

Akisoma uamuzi mfupi kuhusu ombi hilo, Jaji Kipenka alikubaliana na ombi hilo la mawakili wa Serikali na kukubali kufuta rufaa hiyo.

Katika rufaa namba 10, wakili Kadushi aliieleza mahakama kuwa katika hoja za awali wamekubaliana na hoja moja ambayo kimsingi inahusika na masharti ya kanuni ya 77 ambayo inasema rufaa ikiondolewa mahakamani haiwezi kurudishwa hadi ipate kibali cha mahakama.

Wakili Kadushi aliiomba mahakama hiyo kuiondoa rufaa kwani ilikiuka kanuni ya 77. Walikuwa wanapinga Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kusikiliza rufaa yao wenyewe.

Kibatala alisema hawana pingamizi na ombi hilo na kuiomba mahakama hiyo kuondoa kwenye rekodi pingamizi za awali walizokuwa wameziwasilisha katika rufaa hiyo.

“Tunaomba mahakama kwa kuwa ina mamlaka ya kutatua tatizo hili, iondoe tatizo na kutoa tafsiri ya notisi ya rufaa,” alisema Kibatala.

Jaji Luanda alisema mikono yao imefungwa kisheria, hawawezi kufanya chochote, kwani Jamhuri ndiyo walikata rufaa na ndiyo wameiondoa hivyo hoja hiyo itaenda kujadiliwa Mahakama Kuu.

Katika rufaa namba 9 mawakili wa Serikali walikuwa wakipinga Jaji Salma Maghimbi kusikiliza rufaa yao, ambayo baada ya kufutwa sasa jalada hilo litarudi Mahakama Kuu kwa jaji huyo ili kuisikiliza rufaa ya Serikali. Awali alisema kuwa amefungwa mikono ya kisheria kutokana na kusudio hilo.

Katika rufaa namba 10, wanapinga uamuzi wa Jaji Dk. Modester Opiyo aliyempa Lema muda wa ziada wa siku 10 kukata rufaa nje ya muda akipinga mwenendo na uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha uliosababisha kuwa mahabusu licha ya dhamana yake kuwa wazi.

 

KIBATALA ALIA

Wakili Kibatala alishindwa kujizuia kwani alionekana akilia ndani ya chumba cha mahakama, wakati Jaji Luanda alipokuwa akijibu hoja ya kuomba mahakama itoe tafsiri ya notisi ya rufaa.

 

OFISI YA DPP, AG

Baada ya mawakili hao wa Serikali kuomba kufutwa kwa rufaa hizo, Jaji Luanda alionyesha kukerwa na kitendo hicho na kusema ofisi ya DPP inafanya wanasheria wote waonekane hawana akili kwani suala hilo linatia najisi taaluma hiyo na ofisi hiyo kwa ujumla.

Alisema katika hali ya kawaida, mtu anatakiwa kushikiliwa kwa misingi ya sheria na kuitaka ofisi hiyo kuwa makini kwani haipendezi wala haiingii akilini mtu kushikiliwa kwa misingi ya kuminywa haki.

“Taaluma hii (sheria) na ofisi ya DPP mnaitia najisi, kitu kiko wazi ila mnafanya kitu cha ajabu, hakipendezi kwani mnafanya wanasheria wote tuonekane hatuna akili, mtu ashikiliwe kwa misingi ya sheria.

“Tumepitia jalada, tunashangaa hivi ofisi ya Mwanasheria Mkuu ina wanasheria? Kwanini huyu mtu yuko ndani mpaka leo?” alihoji Jaji Luanda.

 

NJE YA MAHAKAKAMA

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema wamefarijika kwa kiwango kikubwa kutokana na kauli ambazo zimetolewa na majaji japo hazikuwa sehemu ya uamuzi.

Alisema kitendo cha majaji kulaumu ofisi ya DPP na ofisi ya AG, ni jambo ambalo lazima lizungumzwe na watu wote kwa uwazi na kwamba mawakili wa Serikali hata kama wanapewa maelekezo, watambue wana wajibu wa kutekeleza viapo vyao vya uwakili.

“Tunaomba ofisi ya DPP waache michezo ya siasa ndani ya mahakama, kauli za jaji ni nzito kwetu kwa sababu tulishaanza kukosa imani na mahakama tukiamini inapewa maelekezo na Serikali juu ya nani apewe dhamana.

“Tumeamini mahakam siyo mkono wa pili wa Serikali ila ni mhimili unaojitegemea kwa misingi ya sheria, walikuwa wanatumia 'technicalities’ za kisheria, lakini tumefarijika sana na kauli za majaji zinazoonekana wamechoshwa na uovu uliokithiri wa kunyima haki ya mbunge kwa muda mrefu,” alisema Mbowe.

 

KIBATALA

Kwa upande wake, wakili Kibatala alisema: “Mmesikia mahakama ilivyokemea ofisi ya DPP namna ambavyo wamekuwa wakitumia mahakama kama mwavuli wa kumsumbua na kumweka ndani Lema bila sababu za kisheria, sisi tunafurahia, kinachofuata ni kuiomba Mahakama Kuu kwa kadiri inavyowezeka ituite ili kuweza kuendelea na uamuzi.”

Januari 4, mwaka huu Jaji Maghimbi alitarajiwa kutoa uamuzi juu ya rufaa iliyowasilishwa na upande wa Jamhuri wakipinga Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kumpa Lema haki ya dhamana, baada ya mawakili wa pande zote kuwasilisha hoja zao kwa maandishi.

Uamuzi huo ulikuwa unatarajiwa kutoa tafsiri ya kisheria ya notisi ya nia ya kukata rufaa iliyowasilishwa na mawakili hao wa Jamhuri, ambayo ilisababisha mahakama hiyo kutokuendelea na hatua ya kuweka masharti ya dhamana.

Jaji Maghimbi alilazimika kuahirisha uamuzi huo kutokana na mawakili wa Serikali kusajili nia ya kusudio la kukata rufaa Desemba 30, mwaka jana katika Masijala ya Mahakama ya Rufaa Tanzania iliyopo mkoani Arusha, kupinga asisikilize rufaa hiyo.

 

VIONGOZI CHADEMA

Miongoni mwa waliokuwapo mahakamani hapo ni pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti Mbowe, Katibu Mkuu Dk. Vicent Mashinji, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Profesa Mwesiga Baregu.

Wengine ni wabunge John Heche (Tarime Vijijini), Esther Bulaya (Bunda Mjini), John Mnyika (Kibamba), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Julius Kalanga (Monduli) na wabunge wa viti maalumu, Grace Kiwelu na Joyce Mukya.

Lema yupo mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo kwa zaidi ya miezi mitatu, ambako anashikiliwa baada ya kukosa dhamana kwenye kesi mbili za uchochezi zinazomkabili  dhidi ya Rais Dk. John Magufuli. Alikamatwa Novemba 2, mwaka jana mjini Dodoma.

Alifikishwa mahakamani Novemba 8 mwaka jana na dhamana yake ilikwama na kuleta utata katika kesi za uchochezi namba 440 na 441 za mwaka 2016 zilizofunguliwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles