Na JUDITH NYANGE – MWANZA
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amefuta hati za viwanja 15 vilivyokuwa vinamilikiwa na Hermant Patel na kurejesha umiliki wake kwa serikali.
Inaelezwa kuwa viwanja hivyo vilipatikana kwa njia ya udanganyifu.
Akizungumza na waandishi wa habari Mwanza jana, Lukuvi alisema anaishukuru ofisi ya ardhi Kanda ya Ziwa kwa kutekeleza agizo la kufuta umiliki wa hati 15 za Patel.
Alisema mtu huyo alipata hati hizo kwa njia ya udanganyifu kwa kutumia hati ya uraia pacha wa Tanzania na Uingereza.
Waziri alisema awali ilidhaniwa Patel anamiliki hati tano za viwanja lakini kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) imegundulika ana hati 15 alizozipata kwa njia ya udanganyifu kwa kuwa na uraia wa nchi mbili.
“Patel ni raia wa Uingereza kwa sheria za nchi hii haziruhusu raia wa kigeni kumiliki ardhi, viwanja vyote 15 ambavyo alikuwa anavimiliki vimerudi serikalini.
“Leo nimeagiza ekari 30 alizokuwa anamiliki katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega mkoani Simiyu vikabidhiwe kwa mkurugenzi vitumike kwa shughuli za maendeleo ikiwamo uchimbaji wa mabwawa.
“Viwanja vingine vilivyobaki kwa kuwa vipo mwambao wa Ziwa Victoria vitangazwe ili vipate wawekezaji.
“Viwanja vingine vilivyobaki ambavyo Patel alikuwa anavimiliki katika mikoa ya Mwanza, Geita na Simiyu nimevirudisha katika kamati ya ugawaji wa ardhi ya taifa vipigwe mnada serikali ipate fedha.
“TAKUKURU wataendelea na hatua nyingine za kisheria ikiwemo kumfikisha mahakamani,” alisema Lukuvi
Lukuvi aliwaonya watu wote wenye tabia kama ya Patel ya kutumia hati za kuishi nchini zenye uraia wa nchi mbili, ambao walifanya udanganyifu na wanamiliki ardhi kama raia wa Tanzania wajisalimishe vinginevyo watashughulikiwa na kunyang’anywa ardhi wanazozimiliki.