23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Lugumi yarudi kivingine

bunge1*Programu ya kufunga mashine yaisha muda

Na MWANDISHI WETU, DODOMA

SAKATA la mkataba tata wa Sh bilioni 37 kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises Limited, limechukua sura mpya baada ya programu ya kufunga vifaa hivyo kudaiwa kwisha muda wake.

Kwisha kwa muda wa programu hiyo, kunaweza kulifanya Jeshi la Polisi kumwangukia mmiliki wa Kampuni ya Lugumi aweze kurejea na kufunga vifaa hivyo kwa makubaliano mapya.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghejwa Kaboyoka, kulieleza Bunge uamuzi wao wa kuunda kamati nyingine ili kwenda kuhakiki vifaa hivyo tena kwa mara ya pili kutokana na sintofahamu iliyojitokeza.

Kutokana na hali hiyo, Kaboyoka alisema hivi karibuni kwamba licha ya kamati yake kutoa maagizo saba kuhusu suala la Lugumi, bado wamelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha kunakuwapo na jenereta ya dharura ili ‘seva’ ya kuratibu mashine hizo iliyopo makao makuu ya jeshi hilo, iweze kupokea taarifa kwa uhakika.

Pamoja na hayo, chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Kamati ya PAC, kiliiambia MTANZANIA kwamba taarifa ya Jeshi la Polisi kuhusu ufungaji wa mashine hizo za vidole, inaonyesha hadi sasa ni mashine 68 tu ndizo zilizofungwa na si 104 kama taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilivyoeleza.

“Licha ya hali hiyo, taarifa zinaonyesha hata programu maalumu ambayo inatakiwa kufungwa kwenye mashine hizo, imemalizika muda wake.

“Kwa hali hiyo, Jeshi la Polisi ni lazima lirudi tena kwa Lugumi na kumpa fedha nyingine ili aweze kufunga mashine zilizobaki.

“Kama unavyojua, suala la Lugumi ni zito na limekuwa likibeba vigogo kadhaa serikalini na hata nje. Ila kama wakubwa wataona hawawezi kumpa Lugumi hiyo kazi, watalazimika kwenda Urusi ambako ndiko kuna wataalamu wa kufunga mashine hizo.

“Tafsiri ya hapa ni nini, sasa Serikali italazimika kurudi tena kwa Lugumi ili wampe fedha nyingine au waende Urusi au Mareakani, ambako pia kuna wataalamu waliokwishasaini mkataba na Kampuni ya Infosy Ltd inayohusika na mashine hizo,” kilisema chanzo chetu.

Kampuni ya Lugumi iliingia mkataba wa Sh bilioni 37 na Jeshi la Polisi wa kufunga mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole nchi nzima.

Hata hivyo, kampuni hiyo ilibainika kutotimiza matakwa ya mkataba wake baada ya kufunga mashine 14 tu kati ya 108 ilizotakiwa kufunga ingawa tayari ilikuwa imelipwa asilimia 99 ya fedha kwa mujibu wa mkataba.

Pamoja na hali hiyo, mwaka 2011 Kampuni ya Biometrica LLC ya Marekani, iliingia katika sakata hilo ikiwasilishwa na Kampuni ya Teknolojia ya Infosys IPS Tanzania Limited na kuingia nayo mkataba wa kufunga baadhi ya mashine hizo za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi nchini.

“Mwaka 2011 tulipata kazi ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi na kazi hii sisi tuliipata kupitia Kampuni ya Biometrica LLC ya nchini Marekani ambao wao walisema wamepata taarifa zetu kupitia Kampuni ya Dell ya Marekani.

“Tulifanya kazi yetu kwa mujibu wa mkataba na baada ya kumaliza tulilipwa Dola 74,420 (sawa na shilingi 162,849,565), ila ninapenda kusema kuwa wakati wote hatukujua kama kuna mtu anaitwa Lugumi,” ilieleza taarifa hiyo ya Infosys.

Kutokana na hali hiyo, kwa sasa Kampuni ya Lugumi inaonekana kutaka kurejea kwa kasi huku baadhi ya wabunge wakijipanga kutaka kuihoji Serikali katika kikao cha Bunge lijalo wakitaka Spika wa Bunge, Job Ndugai, aunde kamati teule ili kumaliza mzizi wa fitina.

Wakati wabunge hao wakijipanga kufanya hivyo, tayari Kaboyoka ambaye pia ni Mbunge wa Same Mashariki kupitia Chadema, alisema  wanalichukua suala hilo na kuanza uchunguzi wa kina na taarifa itakapokamilika, itawasilishwa bungeni.

Kaboyoka alitoa kauli hiyo wiki iliyopita alipokuwa akihitimisha hoja yake kuhusu taarifa ya kamati yake ya PAC bungeni ambako alieleza kukwama kwa kamati yao katika ukaguzi wa suala hilo kutokana na kukosekana kwa fedha.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2013/14 ndiyo iliyofichua udhaifu huo.

Oktoba 28, mwaka huu, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Projestus Rwegasira, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Bunge ya kuhakikisha mfumo wa vifaa vya utambuzi wa alama za vidole unafungwa katika wilaya za kipolisi 108 nchi nzima kwa muda wa miezi mitatu.

Juni 30, mwaka huu, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, baada ya kuahirisha Bunge la Bajeti, aliiagiza Serikali kuhakikisha mfumo huo unafanya kazi ili kuwadhibiti wahalifu na kuitaka Kamati ya PAC ifuatilie suala hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles