24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DC ashtushwa na kasi ya maambukizi ya ukimwi

irando

MKUU wa Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe, Juma Irando, ameshtushwa na kasi ya maambukizi ya ukimwi katika Tarafa ya Kamsamba wilayani hapa.

Irando alishtushwa na maambukizi hayo mwishoni mwa wiki wakati wa ziara yake katika Kituo cha Afya cha Kamsamba.

Akiwa kituoni hapo, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho, Stanley Simbeye, alimweleza mkuu huyo wa Wilaya kuwa kwa siku wanahudumia wastani wa wagonjwa 60 wakiwamo wanaoumwa malaria, tumbo, maambukizi ya njia ya mkojo na wenye virusi vya ukimwi na zinaa.

Kwa mujibu wa kaimu mganga huyo mfawidhi, kila watu 10 wanaopimwa virusi vya ukimwi, sita hugundulika kuwa na maradhi hayo, idadi ambayo alisema ni kubwa.

“Kila wagonjwa 10 tunaowapima maradhi hayo, sita huwa tunawakuta na virusi vya ukimwi. Kwa hiyo, naweza kusema hali ni mbaya sana katika tarafa yetu na nguvu za haraka zinatakiwa ili kukabiliana na maambukizi hayo,” alisema Simbeye.

Naye Diwani wa Kata ya Kamsamba, Prosper Nyalali (Chadema), alimwambia mkuu huyo wa wilaya, kuwa maambukizi ya ukimwi katika kata yake yanasababishwa na uwepo wa biashara ya mpunga inayowaleta watu wengi kutoka maeneo mbalimbali.

“Pamoja na sababu hiyo, uvuvi wa samaki katika Ziwa Rukwa, ulevi, ndoa za utotoni na ukosefu wa elimu ya afya ni sababu nyingine zinazochangia kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo,” alisema Nyalali.

Akizungumzia taarifa hizo, Irando aliwaagiza viongozi wa wilaya hiyo kuanza kutoa elimu ya afya kwa wananchi ili wajue madhara na njia za kukabiliana na maambukizi ya maradhi hayo.

Pia, aliwapongeza wauguzi na watumishi wa kituo hicho kwa jinsi wanavyotoa huduma za afya pamoja na kuwahamasisha wananchi wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Pia, alihimiza ujenzi wa uzio wa kituo hicho ili wahudumu wa afya waweze kutoa huduma katika mazingira yanayokubalika na bora zaidi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles