*Milioni 500/- hazijulikani zilizopo, zabuni yake ilitangazwa siku moja
*Taarifa ya polisi, CAG zatofautiana, kamati yaahidi kumuona Spika
NA BAKARI KIMWANGA, DODOMA
WAKATI sakata la ufisadi wa mkataba kati ya Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd na Jeshi la Polisi likiendelea kufukuta, imebainika Sh milioni 500 zilichotwa bila maelezo yoyote.
Habari za uhakika zilizopatikana mjini hapa jana, zinasema upotevu huo umebainika baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CGA), kufanya ukaguzi wa taarifa za mapato na matumizi ndani ya Jeshi la Polisi.
Taarifa hizo ziliwasilishwa juzi na Ofisa Masuhuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira na Naibu Inspekta Generali wa Polisi (D/IGP), Abdulrahman Kaniki.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), vigogo hao walishindwa kutoa maelezo ya kina kuhusu tofauti hiyo ya fedha, mbele ya wajumbe wa kamati hiyo.
Chanzo hicho kiliiambia MTANZANIA mjini hapa jana, kuwa wajumbe wote walitilia shaka mkataba kati ya polisi na Kampuni ya Lugumi ambao zabuni yake ilitangazwa kwa siku moja na kesho yake ukasainiwa.
YALIYOBAINIKA
Chanzo chetu kinasema katika kikao na vigogo hao, wajumbe wa PAC walihoji taarifa ya utekelezaji wa mkataba huo na kuonyesha hofu ya kuwapo ‘wingu la ufisadi’ ambalo linahitaji majibu.
“Zabuni ilitangazwa Septemba 22, mwaka 2011 na mkataba kusainiwa Septemba 23, mwaka huo huo, ndani ya siku moja mkataba ukasainiwa jambo ambalo ni hatari.
“Jambo jingine linaloshtua, tangu wakati huo mashine zote wanasema zipo, lakini hazifanyi kazi na swali ambalo wajumbe wanahoji, inakuwaje wanatoa zabuni bila kufanya ‘visibility study’ ya kina ili kujua uwezo wa hii Kampuni ya Lugumi kama ilishawahi kufanya kazi ya aina hii ama la.
“Tumejipanga kwa kila hatua, tumemtaka Makamu Mwenyekiti wetu Aeshi Hilaly, awasilishe taarifa nzima kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai na mwishowe taarifa hii iwasilishwe mbele ya Bunge ili umma ujue namna watu wanavyotafuta fedha kinyume cha sheria,” kilisema chanzo chetu.
Mbali na hilo, pia kamati imebaini tofauti ya fedha zilizopo katika mkataba huo ambapo taarifa ya Jeshi la Polisi inaonyesha walitoa Sh bilioni 37,163,940,127.7, wakati taarifa ya CAG, inaonyesha zilizotolewa ni Sh bilioni 37,742,913,007, ikiwa na tofauti ya zaidi ya Sh milioni 500.
“Katibu Mkuu na wenzake, walipotakiwa kutoa maelezo ya kina kuhusu zilipo Sh milioni 500 walishindwa, wajumbe wakageuka mbogo na kutaka suala hilo litolewe maelezo ya kina.
“Licha ya hali hii, PAC tulibaki tukijiuliza, hata kama kulikuwa na ulazima wa kufunga mashine hizi kwa dharura inakuwaje hazifanyi kazi? Maana kuna kila dalili ya fedha za umma kuliwa mchana kweupe,” kilisema chanzo chetu.
Pia kamati hiyo ilibani mkataba ulitolewa kwa ‘single source’ (yaani kampuni moja bila kuishindanisha na nyingine), badala ya tenda kushindaniwa na kampuni nyingi zaidi.
VIGOGO WAHAHA
Baada ya PAC kuendelea na kazi ya kuchambua taarifa hiyo, kigogo mmoja ambaye anatajwa kuhusika katika mkataba huo, amekuwa akihaha kuomba nguvu ya wabunge wa Kambi ya Upinzani, hasa wale wanaotokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili wamnusuru.
“Ninamshangaa huyo waziri (jina linahifadhiwa), anahangaika bure, eti anasema watu hawampendi na wanamchukia, amefikia hatua ya kusema PAC inatumiwa na wauza dawa za kulevya.
“Sisi ni wajumbe ambao kila mmoja anajiweza, hata siku moja hatuwezi kukaa kutegemea fedha za watu, ila tunafanya kazi kwa masilahi ya nchi yetu na si vinginevyo. Tumeridhika na posho tunazolipwa na Bunge, hatuna haja ya kutumika kwa mtu yeyote ila tunasukumwa na uzalendo kwa Taifa letu,” kilisema chanzo chetu.
Katika kile kinachoonekana ni kama maigizo, baada ya PAC kutaka mkataba na taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa ufungaji wa mashine za utambuzi wa alama za vidole katika vituo vya polisi 108 nchini, sakata hilo limekuwa likichukua sura mpya kila kukicha.
Uamuzi huo uliibua hisia miongoni mwa jamii ambapo katika kipindi cha siku mbili baada ya PAC kutaka ripoti hiyo, Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, iliingilia kati ambapo mwenyekiti wake, Balozi Adadi Rajabu, alikiri kupokea mkataba huo.
UTATA
Kampuni ya Lugumi inadaiwa kupewa tenda na jeshi hilo kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole – ‘Biometric Access’ katika vituo 108 nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37.
Hadi sasa mashine hizo zimefungwa katika vituo 14 pekee na tayari kampuni hiyo imelipwa Sh bilioni 34 ambazo ni sawa na asilimia 99 ya fedha zote za mkataba.
Katika sakata hilo, inadaiwa Kampuni ya Lugumi ilipewa zabuni hiyo ikiwa haina uzoefu wa kazi hiyo.
“Wamepewa mkataba sawa, lakini mbona taarifa zinaonyesha kuwa kampuni hii haijasajiliwa kama Biometric Access Company na haijawahi kufanya kazi zozote zinazohusu Biometric Access Control?” alihoji mmoja wa wataalamu.