23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wagonjwa wa sickle cell hatarini Muhimbili

1Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

HALI za watu wanaotibiwa ugonjwa wa sickle cell katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, ziko hatarini kukosa tiba ya uhakika baada ya kitengo kilichokuwa kikiwahudumia bure kufungwa.

Taarifa za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata Dar es Salaam jana, zinasema Muhimbili imesitisha ghafla matibabu bure kwa wagonjwa hao bila kutoa taarifa rasmi, hali ambayo imezua sintofahamu, licha ya wagonjwa wengi kutoka mikoani kufuata tiba hiyo.

Kwamba huduma hiyo ilikuwa ikitolewa bure hospitalini hapo kwa miaka 10 katika kitengo maalumu kilichopo jengo la watoto, chini ya ufadhili wa Serikali ya Uingereza.

Gazeti hili jana asubuhi lilitembelea kitengo hicho na kushuhudia wazazi karibu 50 wakiwa na watoto wao, wakisubiri huduma ya kliniki, lakini walijikuta wakipigwa na butwaa baada ya kujulishwa utaratibu mpya na wauguzi wa kitengo hicho kuwa kuanzia sasa wanatakiwa kulipia huduma walizokuwa wakipatiwa bure kila wanapofika kliniki.

Huku wakiwa na nyuso za huzuni juu ya utaratibu huo mpya, baadhi ya wazazi hao walikubali kupanga foleni ili kulipia Sh 4,500 ambayo walijulishwa ni kwa ajili ya kupata kipimo cha damu.

Hata hivyo, wazazi wengine walionekana kukaa pembeni wakisononeka na kujadili juu ya utaratibu huo, huku wengine wakisema hawakuwa wamejiandaa kwa ajili ya kulipia gharama hizo.

 

WAZAZI WANENA

Mmoja wa wazazi hao, Grace Kabera, mkazi wa Makongo, Dar es Salaam, alisema taarifa ya kuanza kulipia kliniki imemshtua.

“Jamani hii imeanza lini? Kweli leo (jana) wametu-‘surprise’, mbona hawakutuambia? Namba zetu za simu walizichukua za nini? Hawajatuma hata meseji kwenye simu kutueleza mabadiliko haya… tunatakiwa kulipia na bado dawa zake ni ghali, hali ya maisha ni ngumu, sijui kama tutaweza kumudu gharama hizi,” alisema Grace.

Naye Mkami Kitigwa, mkazi wa Temeke, alisema pamoja na kutakiwa kulipia huduma hiyo, siku za karibuni amekuwa akiambiwa aende Hospitali ya Amana, ambako hata hivyo alielezwa hakuna huduma hiyo.

Kwa upande wake, Getruda Thadeus mkazi wa Tabora, alisema tangu mwaka 2001 mtoto wake amekuwa akipata huduma hiyo, na kwamba alifunga safari kwa ajili ya klikini, lakini sasa amegonga ukuta kwa sababu hakujiandaa kwa fedha za matibabu.

 

DAKTARI

Daktari mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema gharama ya kutibu mtoto mmoja ni karibu Sh 50,000.

“Hapo wameambiwa walipie kipimo cha damu Sh 4,500, bado wakitoka huko lazima wamuone daktari na utaratibu huwa Sh 11,000 ambaye atamwandikia dawa kulingana na kile alichobaini, kwa maana hiyo ili mtoto atibiwe mzazi atahitaji kuwa na angalau kuanzia Sh 50,000 na kuendelea,” alisema.

 

MKUU WA KITENGO

Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA ilimtafuta mkuu wa kitengo hicho, Profesa Julia Makani ili kujua uhalisia wa mabadiliko hayo.

Profesa Makani ambaye pia ni mfanyakazi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS), alisema utaratibu wa kuwatibu bure wagonjwa hao umebadilika kwa kuwa mradi uliokuwa ukiwapatia ufadhili muda wake umemalizika tangu Machi 31, mwaka huu.

“Wagonjwa wa sickle cell walikuwa wakipatiwa matibabu bure, baada ya MUHAS kupata ufadhili mwaka 2004 kupitia Shirika la Welcome Trust la Uingereza ambalo lenyewe huwa linafadhili masuala ya utafiti,” alisema.

Alisema kitengo hicho kimefanya kazi hiyo ya kutoa huduma bure chini ya ufadhili huo kwa muda wa miaka 10 hadi Machi 31, mwaka huu ambapo ulifikia tamati.

“Nilipoona muda wa mradi unamalizika Novemba, mwaka jana niliwaandikia barua Muhimbili kuwajulisha ili wachukue hatua ya kuwahudumia wagonjwa hawa ambao hadi sasa wamefikia 6,000 lakini hakuna majibu niliyopata,” alisema.

 

KAULI YA MUHIMBILI

MTANZANIA lilimtafuta Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa MNH, Aminiel Aligaesha, ambaye hata hivyo aliomba apatiwe muda ili kuweza kulifafanua suala hilo kwa kuwa alikuwa anaingia kwenye kikao na madaktari wa kitengo hicho kwa ajili ya suala hilo.

 

WAZIRI UMMY

MTANZANIA lilimtafuta Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kutaka kupata kauli yake juu ya mabadiliko hayo, lakini hata hivyo alimuomba mwandishi kumtafuta Kaimu Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru kwa kuwa yeye yupo mjini Dodoma kwa shughuli za kibunge.

 

PROFESA MUSERU

Alipotafutwa Profesa Museru, alisema mabadiliko hayo yametokana na kumalizika kwa muda wa mradi huo uliokuwa ukifadhili matibabu ya wagonjwa hao.

“Napenda jamii ielewe kwamba Muhimbili hatujasitisha na hatutasitisha huduma ya matibabu bure. Ila ni kweli kwamba kwa upande wa sickle cell kulikuwa na mradi ambao ulikuwa ukifadhili matibabu hayo kutolewa bure, ambao umeisha hivi karibuni na hivyo inabidi wagonjwa wale waingizwe kwenye mfumo wa kawaida wa matibabu kama wagonjwa wengine,” alisema.

Alipoulizwa ni kwanini hawakutoa taarifa hiyo mapema kwa wagonjwa hao ili wajiandae na mabadiliko hayo, Profesa Museru alikiri kwamba hilo ni kosa.

“Tunaomba samahani kwa hilo… lakini sidhani kama imetokea hivyo au wameambiwa hivyo (lazima walipie), ila kama atakuwepo ambaye anashindwa kulipia gharama, kuna utaratibu, ipo ‘mechanism ya social welfare’ ambao watakaa naye na kumsikiliza.

“Hata hivyo hili tutalitatua, tatizo ni kwamba tuli-‘over look’ kujitayarisha kwamba hawa wagonjwa watatibiwa namna gani baada ya mradi kuisha,” alisema Profesa Museru.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles