Na Felix Mwagara-KILOSA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ametumia saa tano kuwatuliza wananchi wa Tarafa ya Kimamba Wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro, ambao walikuwa na hasira kali wakilalamika kunyang’anywa ardhi na wafugaji pamoja na Polisi kuwanyanyasa wananchi hao kwa kuwaweka ndani.
Waziri Lugola ambaye aliwasili saa sita mchana akitokea mjini Morogoro kwa ajili ya kutekeleza ahadi yake kwa wananchi hao baada ya kuwaahidi wiki iliyopita alipofanya ziara katika Tarafa hiyo ambayo ina wakazi zaidi ya elfu hamsini, ili aweze kutatua kero zao za ardhi wakiwa na nyaraka zao za uthibitisho.
Kabla ya mkutano wa hadhara na wananchi hao, Waziri huyo alifanya kikao cha ndani na viongozi wa Wilaya hiyo wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya, kwa lengo viongozi hao kumpa sura halisi ya mgogoro huo ambao unaelekea katika uvunjifu wa amani.
Lugola aliwasili eneo la mkutano mara baada ya kumaliza kikao cha ndani, ambapo alipokelewa na mabango ya wananchi yaliyokuwa yameandikwa ujumbe mbalimbali ikiwemo ‘Polisi wa Dumila wanatumika kuwanyanyasa wananchi na polisi wa Chanzulu wanakamata watu na kuwaweka ndani wananchi wanaotafuta haki ya ardhi’, wafugaji wanapora ardhi zetu, polisi wanapewa rushwa na wafugaji kutuweka ndani’.
Akizungumza na mamia ya wananchi hao, Lugola alisema amekuja kusikiliza kero za wananchi hao baada ya kutoa ahadi yake wiki iliyopita, hivyo anatumaini wananchi hao wanavielelezo kama alivyowaagiza waje navyo katika mkutano huo.
Lugola alisema Jeshi la Polisi alihusiki na masuala ya ardhi isipokuwa limekuwa likichukua hatua pale migogoro hiyo inapoelekea kwenye uhalifu ama uvunjifu wa amani.
Lugola alishangiliwa na wananchi hao alipowaita waje mbele ya meza kuu ili waweze kutoa kero zao, ndipo idadi kubwa ya wananchi hao waliitikia wito huku baadhi yao wakiwa na nyaraka mbalimbali kama walivyoelekezwa.
Licha ya wananchi hao kutoa kero mbalimbali tuhuma nyingi walizielekeza kwa mfugaji maarufu ambaye ni Mmasai katika Wilaya hiyo, Lipasio Mbokoso, anayedaiwa kunyang’anya ardhi zaidi ekari 270 huku akitumia fedha.
Waziri Lugola alimwita Mbokoso katika mkutano huo ili aweze kujitetea kwa nyaraka zake, ndipo ikajulikana kuwa ardhi hiyo ni mali yake halali baada ya kushinda kesi iliyofunguliwa na wananchi hao mahakamani.
“Nyaraka zinaonyesha Mbokoso ni mmiliki halali wa ardhi hii, na pia wananchi ambao nimewataja walifungua kesi, na Mbokoso akashinda kesi hiyo Mahakama Kuu, baadaye mkakata rufaa mkaenda mahakama ya rufaa, pia akashinda, ndugu wananchi naomba mueleze na hakuna haja ya malumbano, huyu ni mmiliki halali wa mali hiyo, msidanganywe na mtu yeyote, fuateni sheria pamoja na kuiheshimu hukumu ya mahakama,” alisema Lugola.
Aliongeza kuwa, kuna baadhi ya wanasheria feki katika eneo hilo wanawarubuni wananchi kwa kuwapotosha na kuwasababisha waingie kwenye migogoro ya ardhi.
“Wanasheria feki ndio wanaochangia migogoro ya ardhi katika sehemu mbalimbali ya Wilaya ya Kilosa, nawataka wananchi kutowatumia badala yake mfuate sheria kama inavyoelekeza,” alisema Lugola.
Kutokana na matatizo ya ardhi kuendelea kutokea katika eneo hilo, Waziri Lugola amemtaka Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Wilbroad Mutafungwa kuchunguza nyaraka zote za migogoro ya ardhi inayowasilishwa na wananchi ili kujua kama ni halali au zimeghushiwa.
Sambamba na hilo, Lugola amemtaka Kamanda huyo kuwachukulia hatua kali za kinidhamu askari wote wasiokuwa waadilifu katika eneo hilo na Mkoa kwa ujumla, wakiwamo wanaohusika kuwanyanyasa wananchi hasa katika masuala ya ardhi.
Kauli ya Waziri huyo ilileta furaha kwa sehemu kubwa ya wananchi hao licha ya kuwa baadhi yao walibaki wakilalamika kuwa, Polisi wameshindwa kutatua kero zao na kuwadharau wakulikuma na kuwathamini wafugaji.
Kutokana na hayo Waziri huyo aliahidi kufuatilia mara kwa mara amani ya eneo hilo.