25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Lugola aibukia vituo vya polisi Buruguni, Tabata

Na FELIX MWAGARA-MOHA, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amefanya ziara ya kushtukiza kituo cha Polisi Tabata na Buguruni jijini Dar es Salaam, ili kujua kama maagizo yake aliyoyatoa katika vituo mbalimbali yameanza kufanyiwa kazi.

Ziara yake hiyo aliifanya jana saa 2:45 asubuhi kwa kuibukia katika Kituo cha Tabata na moja kwa moja alianza kuulizia mahudhurio ya wafanyakazi wote wa kituo hicho na kujua nani yupo kazini na nani hayupo na kwanini hajafika ofisini hapo kwa muda huo wa asubuhi.

Wakati alipokuwa kituoni hapo, alichukua kitabu cha taarifa za watuhumiwa wote waliopo mahabusu na baadaye kuelekea katika mahabusu hiyo, akiwahoji watuhumiwa kwa kuwaita kwa majina kujua makosa yao yaliyoyafanya wawepo kituoni hapo.

Baada ya kumaliza katika kituo hicho, saa 5 asubuhi alielekea kimyakimya katika Kituo cha Polisi cha Buguruni na kuwahoji watuhumiwa waliopo mahabusu katika kituo hicho na kujua makosa mbalimbali yanayowakabili, huku polisi wapelelezi wa tuhuma zao wakiwepo katika tukio hilo.

Akizungumza baada ya kumaliza ziara yake, alisema alitoa maagizo mbalimbali katika ziara zake nchini, hivyo anafuatilia kujua kama maagizo yake yameanza kufanyiwa kazi au bado baadhi ya vituo vimeyapuuza.

“Lengo la hii ziara yangu ni kuboresha utendaji kazi wa vituo vya polisi nchini, sijaja kumuadhibu mtu mimi, hivyo msiwe na wasiwasi, bali kilichonifanya hapa nije ni kufuatilia maagizo mbalimbali ambayo niliyatoa kama kweli mnayafanyia kazi,” alisema Lugola.

Maagizo aliyoyatoa miezi miwili iliyopita katika ziara zake mikoa mbalimbali nchini ni kuhakikisha pikipiki zinaondolewa katika vituo vya polisi, dhamana zitolewe saa 24, ikiwamo Jumamosi na Jumapili, pamoja na polisi kutowabambikizia kesi wananchi.

Hata hivyo, Lugola alivipongeza vituo hivyo vya polisi vilivyopo wilayani Ilala na pia Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma alichokitembelea wiki iliyopita kwa kuanza kuyafanyia kazi maagizo yake aliyoyatoa, zikiwamo baadhi ya bodaboda kuondolewa vituoni na zilizobaki zina kesi mahakamani.

“Nilifanya ziara ya kushtukiza pale Kituo cha Polisi cha Tabata, na pia nimekuja hapa Buguruni, kwa kweli wameanza kuyafanyia kazi maagizo yangu, pikipiki zote nilizozikuta zina sababu ya kuwepo hapo, na si vinginevyo kama walivyokuwa wanaziweka kiholela hapo awali,” alisema Lugola.

Pia Waziri huyo wa Mambo ya Ndani ya Nchi aliwataka makamanda wa polisi nchini kuwafuatilia askari wao kwa umakini ili kujua utendaji kazi wao.

“Hamjui siku wala saa ambayo nitakuja, tufanye kazi, tuwahudumie wananchi, tusiwaonee wananchi, tujitume kufanya kazi kwa weledi, sitamvumilia mtu ambaye atavunja utaratibu,” alisema Lugola.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles