24.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Suala la wamachinga lipatiwe ufumbuzi wa kudumu

WAFANYABIASHARA wadogo wanaojulikana kama wamachinga, hivi sasa ni kada ambayo haikwepeki nchini.

Ni watu ambao ni lazima watafutiwe utaratibu mzuri wa kufanya biashara yao. Kulifumbia macho suala hilo ni kujidanganya na kujitafutia matatizo.

Kwa sababu hiyo, viongozi wa taifa nchini wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa wilaya na mikoa kuhakikisha unakuwapo utaratibu mzuri wa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kuendelea na shughuli zao bila bughudha.

Utaratibu huo ni pamoja na kuwatengea maeneo maalumu ya kufanyia biashara zao na kuhakikisha yana huduma muhimu kama vile maji, umeme na vyoo.

Bahati mbaya hilo halijatekelezwa kama inavyotakiwa katika wilaya na mikoa mingi nchini.

Bado kazi hiyo inaendelea kutekelezwa kwa mtindo wa zimamoto na kutofuata maelekezo yanayotolewa, hali ambayo wakati mwingine imekuwa ikisababisha vurugu kutoka kwa wafanyabiashara hao wakidai kutotendewa haki.

Kwa mfano hivi majuzi uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ulisema utaendelea kuwachukulia hatua za sheria na kuwafikisha mahakamani wafanyabiashara wadogo wanaoendelea kufanya biashara katika maeneo ya katikati ya mji.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo, alikaririwa akisema kuwa hiyo ni baada ya kufanya operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara hao walioacha maeneo waliyotengewa na kukaa katikati ya mji.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, licha ya operesheni hiyo, baadhi ya wafanyabiashara hao walionekana kuwa wabishi na kuendelea na shughuli zao katikati ya mji.

Ilielezwa kuwa zaidi ya wafanyabiashara 600 wametelekeza vizimba vyao katika masoko ya Mazimbu, Mwanzo Mgumu, Manzese, Mawenzi, Nanenane na kukimbilia katikati ya mji kitendo kilichosababisha kufungwa baadhi ya barabara kwa sababu ya msongamano.

Kama tulivyoeleza awali, hiyo ndiyo changamoto inayozikabili wilaya na mikoa mingi nchini – kukimbizana na wafanyabiashara wadogo kila kukicha.

Na chanzo kikubwa cha hali hiyo, kwa mujibu wa uchunguzi, ni kutofanyika maandalizi ya kutosha na kamilifu kabla ya kuwaondoa wafanyabiashara hao katikati ya miji.

Ieleweke kwamba wafanyabiashara wadogo ni chanzo kimoja kikubwa cha mapato ya Serikali – kutokana na kodi – kama utakuwapo mpangilio mzuri wa sehemu wanakofanyia shughuli zao.

Ilivyo, hivi sasa Serikali inakosa mapato kwa kiasi kikubwa kutokana na wamachinga hao kuendelea kufanya shughuli zao holela bila utaratibu unaoeleweka.

Wamachinga katika wilaya na mikoa mingi wamekuwa wakipelekwa katika maeneo ambayo hayakuandaliwa vya kutosha – si rafiki kwa biashara, jambo linalosababisha warejee katikati ya miji baada ya muda mfupi.

Tunasema kwanini uongozi wa wilaya na mikoa usijipe muda wa kutosha wa kuandaa maeneo ya kuwahamishia wamachinga hao?  Kwa mfano, kwanini maandalizi hayo yasichukue hata miezi sita ili wanapohamishwa wakute wanapohamishiwa ni rafiki kwa biashara pamoja na kuwa na huduma muhimu za maji, umeme vyoo na nyingine?

Jingine linalotakiwa ni kuwapa elimu ya kutosha kupitia viongozi na vikundi vyao, hatua ambayo inaweza kuchangia yasiwepo manung’uniko wanapohamishwa na hivyo kutorejesa maeneo ya katika ya miji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,074FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles