30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Lugha ya Kichina inavyofungua milango ya ajira nchini

DSC_6366NA LEONARD MANG’OHA (MSJ), DAR ES SALAAM

CHINA ni moja ya mataifa yaliyopiga hatua zaidi kiuchumi ikilinganishwa na mataifa kama Marekani, Ujerumani na mataifa mengine yenye misuli ya kiuchumi duniani.

Uchumi wa taifa hilo umejikita zaidi katika kilimo kinachochangia asilimia 9, sekta ya huduma asilimia 50.5 na viwanda vikichangia asilimia 40.5.

Linatajwa kuwa taifa linaloongoza katika utengenezaji wa bidhaa na msafirishaji mkuu wa bidhaa zinazotengenezwa nchini humo kwenda katika masoko ya nchi mbalimbali ulimwenguni.

Kwa takwimu za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) za mwaka 2015, uchumi wa taifa hilo unakadiriwa kukua kwa asilimia 6.9 kwa mwaka huku pato la mtu mmoja mmoja likielezwa kufikia Dola za Marekani 8,239.

Haikuwa kazi rahisi kufikia hatua hiyo ikichukuliwa kuwa taifa hilo lilikuwa ni moja ya mataifa yenye uchumi mdogo hadi kufikia miaka ya 1960.

Iliwapasa kufunga mkanda na kuanza mapambano ya kuyatafuta mafanikio hayo yanayoonekana sasa miongoni mwa Watanzania na ulimwengu mzima.

Tanzania ikiwa moja ya mataifa yanayoingiza bidhaa nyingi kutoka China haina budi kujifunza baadhi ya mambo kutoka kwa taifa hilo la kikomunisti.

Lugha kama nyenzo kuu ya mawasiliano baina ya mtu na mtu katika shughuli ya aina yoyote ile huenda ikawa kikwazo baina ya pande pili zinazoshirikiana pale inapotokea haziwezi kuelewana kutokana na utofauti wa lugha.

Inapotokea hali ya aina hii ni lazima mmoja kati yao kujifunza lugha ya mwenzake ili kuweza kuwasiliana kwa urahisi na kwa upande wa ushirikiano mara nyingi aliye chini kiuchumi hulazimika kujifunza kwa aliyemtangulia kutokana na kuwa mhitaji zaidi.

Kutokana na Tanzania kutegemea mambo mengi ya kibiashara kutoka China kama vile magari, vipuli vya mitambo mbalimbali pamoja na vifaa vya kilimo na ujenzi haina budi kuhakikisha raia wake wanajifunza lugha ya taifa hilo.

Katika kuhakikisha Tanzania inajifunza kutoka kwa China, uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), unatarajia kuanzisha Stashahada na Shahada ya Kichina kuwezesha Watanzania kujifufnza lugha hiyo na kurahisisha mawasiliano kwa kutumia fursa zinazotolewa na nchio hiyo ndani na nje ya nchi.

Makamu Mkuu wa UDSM (Taaluma), Profesa Florence Luoga, anasema ufundishaji wa lugha ya kichina utawezesha Watanzania wengi kushirikiana na China katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kama biashara.

Anasema kutokana na makampuni mengi ya kichina kuwekeza hapa nchini kufahamu lugha hiyo kutatoa fursa kwa Watanzania wengi kuajiriwa na kampuni hizo.

Mkurugenzi wa Confucius Institute (CI) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Zhang Xiazhen, anasema kwa sasa lugha ya kichina ni daraja linalounganisha sehemu kubwa ya dunia hivyo kwa taifa lolote linalofuata mfumo wa kiuchumi wa China na kutegemea bidhaa kutoka nchi hiyo haliwezi kuikwepa kujifunza kuchina.

“Huwezi kuikwepa lugha ya kichina kwa sababu Tanzania inatumia bidhaa nyingi kutoka China kutokana na kuuzwa bei nafuu ukilinganisha na bidhaa kutoka mataifa mengine hasa ya Ulaya na Marekani,” anasema Zhang.

Anasema kozi hiyo ilianzishwa chuoni hapo mwaka 2013 kama kozi fupi ambapo kwa kipindi chote imekuwa ikifundishwa kama somo la ziada kwa wanafunzi wa kozi mbalimbali.

Zhang anasema zimekuwa zikitolewa nafasi nyingi za ufadhili wa masomo na serikali ya nchi hiyo lakini wanakosekana watu wa kwenda kusoma kutokana na kutofahamu lugha hiyo.

“Kufundishwa kwa lugha hiyo kutatoa fursa kwa Watanzania wengi kusoma nchini China na kuendeleza biashara baina ya nchi hizi.

“Sisi tulikuwa taifa la uchumi wa chini, tulilazimika kujifunza lugha za mataifa yaliyoendelea na kujifunza teknolojia yao,” anasema.

Mkurugenzi mwenza wa CI katika chuo hicho, Profesa Alvin Mtembei, anasema lengo la kuanzishwa kwa kozi hiyo ni kuwezesha upatikanaji wa walimu wa kutosha kufundisha shule mbalimbali nchini.

Anasema kwa sasa wameanza kufundisha lugha hiyo katika Shule ya Sekondari Baobab ya jijini Dar es Salaam na Christina ya Tanga huku wakitarajia kuifundisha katika Mkoa wa Mtwara na Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT).

“Kwa sababu lugha ni daraja linalounganisha watu basi Watanzania pia lazima wajue lugha na tamaduni za kichina, mwitikio ni mzuri kwa kipindi chote tulichoanza kufundisha hapa chuoni” anasema Profesa Mtembei.

Walimu wanaofundisha kozi hiyo huletwa nchini kutoka Chuo Kikuu cha Zhejiang cha China ambacho hufanya kazi kwa ushirikiano na UDSM.

Dk. Isaac Mbata ni Ofisa Tawala wa Confucius institute, anasema taasisi hiyo inafanya kazi chini ya serikali ya china iliyoanzishwa mwaka 2004 ikiwa na lengo la kufundisha lugha ya taifa hilo sehemu mbalimbali duniani.

Kwa mujibu wa Dk. Mbata, kwa sasa taasisi hiyo ina vyuo 500 duniani kote nusu yake vikiwa nchini Marekani.

Anasema tangu kuanzishwa kwa kozi fupi UDSM zaidi ya wanafunzi 1,500 wamejimejitokeza kusoma ambapo kwa sasa kuna wanafunzi 200.

Mwaka jana wanafunzi 12 waliosoma lugha ya kichina chuoni hapo walikwenda Marekani kwa mafunzo ya vitendo kwa udhamini wa Kampuni ya Golden Land Group ya China na sasa wameajiriwa katika matawi yake yaliyopo hapa nchini.

Anasema ujenzi wa maktaba ya iliyozinduliwa hivi karibuni na Rais Dk. John Magufuli, ni utekelezaji wa mkataba wa elimu baina ya Tanzania na China uliofikiwa wakati wa ziara ya Rais wa  nchi hiyo hapa nchini mwaka 2013. Pia anasema ni moja ya jitihada za kusambaza lugha ya Kichina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles