24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

4G LTE ya Vodacom kuandika historia Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

Intaneti humwezesha mtu kupata taarifa mbalimbali zinazoendelea dunianiKAMPUNI za simu nchini kwa nyakati tofauti zimezindua teknolojia mpya ya 4G-LTE ambayo inatajwa kuchochea mapinduzi ya upatikanaji wa huduma za data na kuongeza pato la taifa.

Huduma hiyo ya 4G-LTE, tayari imezinduliwa na kampuni mbalimbali za simu za mkononi huku zikitarajiwa kuongeza kasi na ufanisi kwenye huduma za intaneti.

Hivi karibuni Kampuni ya Vodacom Tanzania ambayo ilizindua huduma hiyo na kuzua gumzo kwenye soko la watumiaji wa intaneti kwenye simu za mkononi.

Watumiaji wengi wa simu hizo wameanza kufuatilia kujua tofauti iliyopo kati ya huduma za intaneti za sasa na teknolojia hii mpya iliyozinduliwa (4G LTE).

Licha ya kwamba kampuni hiyo si ya kwanza kuanzisha huduma hiyo nchini, lakini uanzishwaji wake wa 4G unafuatiliwa na watumiaji wengi kutokana na historia yake tangu ilipoanza kutoa huduma za mawasiliano nchini.

Mbali na uanzishwaji wake kuwa wa kishindo na kuungwa mkono na Watanzania wengi pia huduma mbalimbali ambazo imeanzisha kama vile M-Pesa, M-Pawa na nyinginezo zimekuwa zikiongoza na kudhihirisha kuwa haianzishi huduma kwa kukurupuka bali inajipanga kuhakikisha inakuwa bora na kukidhi kiu ya wateja wake.

Wakati huduma hii imeanza kushika kasi jijini Dar e Salaam, baadhi ya wateja wake wa huduma za mawasiliano wanajiuliza maswali mbalimbali  kuhusiana na teknolojia hiyo.

Baadhi yao walisema teknolojia hiyo isingeweza kufanya vizuri Tanzania kutokana na sababu mbalimbali huku wengine wakiwa na mawazo kwamba huenda huduma hiyo ni kwa watu wenye kipato cha juu tu.

Hata hivyo watu wengine wanajiuliza kwanini huduma hiyo haisambazwi nchi nzima kama zilivyo teknolojia nyingine.

Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Rosallyn Mworia (pichani), anawataka Watanzania kuondoa hofu ya kuanzishwa kwa huduma mpya au kukatishwa tamaa na changamoto zinazotokea wakati huduma zinapoanzishwa.

“Sehemu yoyote duniani kikianzishwa kitu kipya kinafanyiwa majaribio na ndipo kinatumiwa na baadaye kuzoeleka kwa watumiaji,” anasema.

Kuhusiana na huduma hii ya 4G anasema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita hadi mwaka huu, imeanza kutumika katika nchi za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania na matumizi yake yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku.

“Teknolojia hii inazidi kukua katika ukanda wa Afrika Mashariki ikiwa imeanzishwa na makampuni mbalimbali yanayotoa huduma za simu katika ukanda huu baadhi yake yakiwa Safaricom ya nchini Kenya, MTN nchini Rwanda na Uganda, Viettel nchini Burundi, Tigo kwa hapa nchini na uwekezaji wa kufanikisha teknolojia hii umekuwa ukifanyika kwa ushirikiano na makampuni makubwa ya mawasiliano kutoka nchi zilizoendelea kama Erickson, Nokia, Huawei na mengineyo,” anasema Mworia.

Aidha, Mworia anasema Vodacom nayo imejitosa katika kutoa huduma hiyo ikiwa na uhakika wa kufanya vizuri kutokana na uwekezaji mkubwa ilioufanya na maandalizi ya muda mrefu ya kuhakikisha inaingia kwa uhakika na kuileta sokoni  kwa ubora wa hali ya juu.

“Watanzania na wateja wetu wategemee huduma bora za mawasiliano nchini kutokana na uwekezaji na ubunifu unaoendelea kufanyika katika sekta hii ikiungwa mkono na jitihada za serikali ambayo tayari imejenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao utasaidia kuboresha mawasiliano nchini,” anasema.

Mworia anasema badala ya kuogopa teknolojia mpya na kusema kuwa 4G haiwezekani kuwepo nchini watumiaji wanapaswa kujua kuwa katika mataifa yaliyoendelea wanaongelea kutoka kwenye matumizi ya 4G kwenda 4G.5 mpaka 5G.

Kuhusu teknolojia hiyo kutosambaa nchi nzima, Mworia anasema teknolojia kama hizo zinahitaji uwekezaji mkubwa na hutumika kwa simu maalumu za Smart Phone na kwamba kubadilika kwake kunahusisha kubadilisha kadi za simu, hivyo inabidi kuisambaza taratibu kuepusha usumbufu kwa wateja.

“Teknolojia mpya inapoingia haibadilishi iliyopo kwa siku moja, bali mabadiliko yanaenda kwa awamu na ndivyo wanavyoshauri wataalamu wa teknolojia na mawasiliano.

“Tumeanza kutoa huduma hii sehemu chache na tutazidi kuisambaza sehemu mbalimbali. Bado tunakabiliwa na upungufu wa masafa ya kusambaza teknolojia hii nchini kote lakini tunaendelea kuwasiliana na mamlaka husika ili kuhakikisha Watanzania wote wanaingia katika ulimwengu wa teknolojia kama ilivyo dhamira yetu,” anasema.

Katika hatua nyingine, Mworia anasema licha ya kuwa na 4G LTE bado teknolojia ya 3G ya Vodacom inazidi kufurahiwa na wengi na kampuni inaendelea kufanya uwekezaji wa kuiimarisha.

Ambapo kwa mwaka huu imeongeza minara mipya nchi nzima na kufikia 1500.

Anasema huduma ya 4G yenye kasi kubwa ya Vodacom itarahisha mawasiliano ya intaneti  kwa wateja wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles