Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
KLABU ya gofu ya Lugalo imefanya vizuri katika mashindano ya gofu ya NBC Tanzania Open 2021 baada ya wachezaji wao kuibuka washindi kwenye vipengele mbalimbali, huku ikitwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza.
Katika michuano hiyo iliyomaliza jana, mchezaji chipukizi wa Lugalo, Isihaka Daudi ameibuka kidedea kwa kutwaa ubingwa wa jumla, akizima ufalme wa nahodha wa timu ya Taifa, Victor Joseph wa Dar Gymkhana ambaye ameshika nafasi ya pili.
Isihaka amepata ushindi huo kwa kupiga mikwaju 272, wakati Victor wa amepiga mikwaju 298, huku mshindi wa tatu naye kutoka Lugalo Richard Massawe akipiga mikwaju 316 kwa mashimo 72.
Mashindano hayo yamefanyika kwa siku tatu na kumalizika jana Desemba 5, 2021 yakishirikisha klabu za Tanzania kwenye viwanja Gofu Lugalo, Dar es Salaam.
Katika ‘division A’ mshindi wa kwanza ni Baraka Samweli kwa mikwaju 286, akifuatiwa na Zakaria Edward mikwaju 289, namba tatu ni Nicholas Chitanda alipiga mikwaju 292, wote wa Lugalo.
Kwa upande wa watoto (Juniors) waliocheza viwanja 36, mshindi wa kwanza ni K Angelo kwa mikwaju 132, wa pili Ibrahimu Juma mikwaju 134, huku mshindi pekee wa ‘gross’ akiwa ni Rahimu Ally mikwaju 324 wote wa Lugalo.
Wachezaji wa kulipwa kwa mashimo 72, namba moja ni Frank Mwinuka(Lugalo) alipiga mikwaju mikwaju 294, wa pili Hassan Kadio (Dar Gymkhana) mikwaju 300, wa tatu Bryson Nyenza (Lugalo) mikwaju 302, wa nne ni Nuru Mollel (Arusha) mikwaju 308 wa tano ni Isack Wanyeche (Kili Gofu) aliyepiga mikwaju 309.
Kwa wachezaji wazee (senior men) namba moja ni A Kiarie mikwaju 155, akifuatiwa na Alfred Kinswaga wa Dar Gymkhana mikwaju 162.
Kwa upande wa wanawake katika mikwaju ya jumla (net), mshindi wa kwanza kwa mikwaju 144 ni Joyce Odira (Lugalo), wa pili Rehema Athumani (Dar Gymkhana) mikwaju 148, huku gross mshindi akiwa mmoja, Angel Eaton(Lugalo) mikwaju 163.
Akizungumzia ubingwa huo,Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali Michael Mstaafu Michael Luwongo, amesema ubingwa wa Isihaka ni heshima kubwa kwao kwa sababu ni mafanikio ya mradi wa watoto.
“Mshindi aliyeshinda leo(jana) kwenye kombe hili kubwa la NBC Tanzania Open 2021, ni kijana aliyekulia hapa na kujifunzia gofu hapa na leo hii tunamuona jinsi alivyoburuza watu, kwangu mimi amenipa heshima kubwa sana, nitakaa na kamati yangu ya klabu ili tumtafutie zawadi ya ziada.
“Hiyo ni zawadi ya kutupa heshima sisi Wanalugalo Golf Club, kwa hiyo ndugu yangu Isihaka Daudi leo nakupa wadhifa wa uheshimiwa katika klabu hii kwa sababu hili kombe ndiyo mara ya kwanza lipo hapa,” ameeleza.
Naye mgeni rasmi wakati wa kufunga mashindano hayo, akizungumza katika hafla ya kutoa zawadi kwa washindi jana usiku, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Abdallah Possi, amesema amevutiwa na mchezo huo, huku akiahidi kuanza kucheza.
Aidha Dk. Possi ameipongeza klabu ya Lugalo kutokana na mtindo inaotumia kuendeleza mchezo wa gofu hasa kuibua vipaji vya watoto.
Pia ameipongeza benki ya NBC kwa mapinduzi iliyoyafanya katika michezo hadi kufikia kudhamini mashindano ya gofu, pamoja na kuwa mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara.
“Michezo ni uwekezaji naomba muendelee hivi hivi, mmefanya mapinduzi makubwa, pia nimefarijika kuona kundi kubwa la watoto wanaocheza gofu na hata bingwa wa mwaka huu nimembiwa ameanzia Juniors.
“Pia niwapongeze TGU (Chama cha Gofu Tanzania), na vyama vyote kwa kuendeleza mchezo huu, Serikali tunathamini sana mchezo wenu na ningeomba tukutane hivi karibun ili tupange mikakati,” amesema Dk. Possi.
Amesema Serikali ipo tayari kuwatafutia TGU, eneo la kujenga kiwanja cha gofu na kuutaka uongozi wa chama hicho kuwasilisha maombi haraka.
Naye Mwenyekiti wa TGU, Chriss Martin, ameiomba Serikali kudhamini timu ya Taifa ya mchezo huo ili kufanya vizuri katika mashindano ya Kimataifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Wateja Binafsi na Wafanyabiashara ndogondogo wa benki ya NBC ambao ndiyo wadhamini wa michuano hiyo, Elibariki Masuke, amesema wamefurahi jinsi mashindano yalivyoendeshwa na kuwafanya wavitiwe kuendelea kudhamini mchezo huo.
“Ni mara yetu ya kwanza kudhamini gofu, kwa kweli, mashindano yamekuwa mazuri sana, yamekutanisha wachezaji wengi tunaahidi kuendelea kudhamini gofu,” amesema Masuke.