Na Mwandishi Wetu, Moshi
Timu ya Gofu ya Jeshi la Ulinzi La Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo, imeibuka kinara katika shindano la “Northern Zone Championship 2024” lililofanyika kwa siku tatu TPC Moshi mkoani Kilimanjaro.
Katika shindano hilo, mchezaji Isihaka Daudi kutoka Lugalo aliibuka mshindi wa kwanza.
Akizungumza katika hafla ya kufunga shindano hilo, Isiaka amewashukuru waandaaji pamoja na wachezaji wenzie na kusema licha ushindani mkali ameweza kuiwakilisha vyema klabu yake.
Nahodha Wa Klabu ya GoFu Lugalo, Meja Japhet Masai kwa niaba ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo, amepongeza mfumo wa kietroniki wa kuweka matokeo ya wachezaji.
Pia ametumia nafasi hiyo kutangaza ujio wa shindano litakalofanyika Machi 9,2024 kwenye viwanja vya Lugalo Gofu Dar es Salaam likihusisha klabu zote nchini.
Kwa upande wake Nahodha wa Klabu ya TPC Moshi, Jafari Ally ameipongeza Lugalo Gofu kwa ushindi na ushiriki wao pamoja na mikakati ya kuendeleza wachezaji watoto kielimu na mchezo huo.
Wachezaji wengine walioibuka washindi ni Ibrahim Mtemi kutoka TPC akishika nafasi ya pili, huku Ally Isanzu wa TPC na Michael Masawe wa Lugalo wakifungana katika nafasi ya tatu.