22.1 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Lucy Kibaki afariki dunia

lucykibakiNAIROBI, KENYA

LUCY Kibaki, mke wa Rais mstaafu wa Kenya, Mwai Kibaki, amefariki dunia jana asubuhi wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Bupa Cromwel, jijini London, Uingereza.

Kitengo cha Habari cha Rais wa Kenya (PSCU), kilitangaza jana kuwa Kenya na dunia nzima inaomboleza kumpoteza Mama Kibaki ambaye alikuwa akiugua kwa mwezi mmoja.

Wakati wa uhai wake, Mama Kibaki alijishughulisha kwa kiwango kikubwa na kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa Ukimwi.

“Mheshimiwa afya yake haikuwa nzuri kwa mwezi mmoja na alikuwa akipatiwa matibabu hapa Kenya kabla ya kupelekwa Uingereza,” taarifa iliyosainiwa na Rais Uhuru Kenyatta ilieleza.

Mama KIbaki anakumbukwa kwa kauli yake ya “Domo Domo” alipokuwa akiwasuta viongozi na siasa za kupiga domo badala ya kuangazia maendeleo na masuala yanayonufaisha wananchi.

Mke huyo wa rais mstaafu Kibaki, alikimbizwa katika Hospitali ya Nairobi mwezi uliopita baada ya kutibiwa katika Hospitali ya Gertrude huko Muthaiga.

Wiki iliyopita familia ya Kibaki ilieleza kwa mara ya kwanza kwamba ilibidi Lucy apelekwe ng’ambo kwa matibabu maalumu baada ya kuzidiwa na ugonjwa ambao familia haikuweka bayana kuueleza.

Marehamu ameacha watoto wanne, Judy Wanjiku, Jimmy Kibaki, David Kagai na Tony Githinji.

Alizaliwa mwaka 1940 huko Mukurwe-ini kwa mchungaji wa kanisa la kikoloni la Presbyterian Afrika Mashariki, John Kagai na mama Rose Nyachomba.

Alikuwa mwalimu katika Chuo cha ualimu  Kamwenja kabla kuhamishwa Chuo cha Kambui.

Aliacha kazi ya ualimu katika chuo hicho ambacho kwa sasa kinaitwa Chuo cha Wasichana Kiambu baada ya uhuru mwaka 1963 ili kuiangalia familia yake kwa karibu wakati mumewe akiwa amejikita katika siasa.

Katika ujumbe wake wa rambirambi, Rais Kenyatta alisema Mama Kibaki atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya nchi.

“Ni pigo kwetu kumpoteza Mama wa Taifa wa zamani kwa uongozi wake na dhamira yake ya kuboresha ustawi wa Wakenya na kuwa kwake mstari wa mbele kupigana dhidi ya maradhi ya Ukimwi, kitu ambacho kinabakia ndani ya nyoyo za wengi,” alisema Rais Kenyatta.

Septemba 2003, Mama Kibaki aliandaa kongamano la kwanza la kimataifa kuhusu Ukimwi na alishiriki kuanzishwa kwa jukwaa la wake wa marais Afrika katika kupambana na Ukimwi (OAFLA).

Mke huyo wa rais mstaafu mwenye umri wa miaka 75, amekuwa akionekana kwa nadra tangu mumewe Kibaki aondoke madarakani mwaka 2013.

Pia hakujitokeza hadharani wakati Kibaki alipokabidhi madaraka kwa Rais Kenyatta.

Kabla ya hapo, alikuwa akijulikana kwa kuzungumzia masuala ya familia na mataifa, hata akiwa pembeni ya mumewe au viongozi wakubwa, kiasi cha kujijengea taswira ya ubabe.

Naibu Rais wa Kenya, William Ruto, alituma ujumbe wake katika mtandao wake wa Twitter akisema ameshtushwa kusikia taarifa ya kifo hicho kwa masikitiko makubwa na anamwombea Kibaki na familia yake.

Viongozi wengine nchini humo waliotuma ujumbe katika Twitter ni pamoja na Jaji Mkuu, Willy Mutunga, Kiongozi wa Chama Tawala Bungeni, Aden Duale na Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles