24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa: Ushindi 90% CCM waibe 10

0D6A9052SHABANI MATUTU NA PATRICIA KIMELEMETA, DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu wa zamani ambaye pia ni mgombea urais kwa mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amewataka wananchi kuhamasishana na kumpigia kura ili apate ushindi wa asilimia 90.

Alisema akipata ushindi huo na hata kama Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiiba asilimia 10 ya kura zake, bado Ukawa watabaki na asilimia 80 ambao ni ushindi mzuri.

Akizungumza na wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), Buguruni, Dar es Salaam jana, Lowassa alisema hiyo ndiyo njia pekee ya kuishinda CCM.

“Hawa jamaa ni hodari sana wa kuiba kura, tunahitaji kufanyika kwa ushawishi na mshikamano, kila mtu anahitaji kushawishi wenzake angalau watano ili tujihakikishie ushindi wa asilimia 90 pindi watakapoiba asilimia 10 tutaibuka na ushindi wa asilimia 80.

“Ni bora tuhakikishe tunapata kura nyingi ili wakiiba wasiweze kutufikia na jambo jingine tulinde kura zetu kama ambavyo sasa Chadema wanafanya na CUF, wamekuwa ni bingwa wa kazi hiyo kwa muda,” alisema.

Alisema kama watahakikisha hilo linafanyika na wanashikamana pamoja, itakuwa vigumu kwa CCM kuwashinda kirahisi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Lowassa aliwaambia jambo muhimu wanalotakiwa kutambua ni kutoyumba, kwani kwa kufanya hivyo watasababisha kujiwekea mazingira magumu kuingia Ikulu na pia watambue kuwa kura ndiyo itawawezesha na si njia ya maandamano hivyo aliwaomba kuhifadhi shahada zao.

“Hivi sasa Watanzania wapo makini na wapo tayari kuongozwa kwenda Ikulu Oktoba 25, jambo la msingi ni kuhakikishi mnalinda shahada zenu na kutumia nidhamu, tukitumia kura hawa tutawashinda Jumapili asubuhi, hawana hoja tena washachoka,” alisema na kuongeza:

“Jambo muhimu ni kutoyumba, tukiyumba Ikulu mjue hatuingii, huko tutaenda kwa kura na si kwa maandamano naomba sana mhifadhi shahada zenu.”

UCHUMI

Lowassa, alisema miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakimuumiza tangu akiwa CCM ni nchi kutosonga mbele kimaendeleo.

Alisema CCM imekuwa ikiendesha uchumi kwa tabu na adha, jambo ambalo lilifanya kuwauliza wananchi kwamba wakati Mkapa anaondoka madarakani dola ilikuwa shilingi ngapi na sasa ni ngapi? Wananchi wakajibu ilikuwa 1,000 na leo shilingi 2,200 akawauliza je, huo ndio uongozi?

Lowassa aliwahoji tena, wakati Mkapa anaondoka madarakani bei ya mchele ilikuwa shilingi ngapi? Wananchi wakajibu ilikuwa 1,000 leo imefikia shilingi ngapi? Wakajibu 2,500.

“Naweza kutaja vitu vingine vingi, niridhike kwa kusema nachukia umasikini, nauchukia umasikini kwa akili yangu yote na ndiyo maana naomba ridhaa kwa Watanzania niende Ikulu nikatoe umasikini kwa Watanzania ili waweze kula milo mitatu, wawe na nyumba na gari la kutembelea,” alisema.

“Kwa miaka 50 Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alizungumzia kuhusu umasikini hadi leo bado tunazungumzia suala la umasikini, maradhi na ujinga kwanini? Kwanini tunakubali kuendelea kuwa nyuma, inabidi tufike mahali tujiulize kwanini Waganda, Wakenya, Wanyarwanda watupite kwa uchumi.

Maandamano

Katika maandamano yanayotarajiwa kufanyika leo, Lowassa alitoa wito kwa wanachama wanaounda Ukawa kuwa watulivu katika maandamano watakayofanya kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu ya kugombea urais.

Maandamano hayo yanatarajiwa kuanzia katika ofisi za chama hicho na kwenda ofisi za Chama cha NCCR- Mageuzi na baadaye NEC kuchukua fomu na wakishachukua wanamalizia ofisi za Chadema ambapo viongozi wa Ukawa watazungumza na wananchi.

“Kumbukeni maadui zenu huwa wanasema chama chetu kina fujo eti hakina heshima kwa akina mama na wazee, hivyo naomba tujihadhari na maneno hayo na katika maandamano ya leo tuwe na nidhamu na waungwana na tusikilize maelekezo ya Serikali, hawa wanataka kutuzingua hivyo tusiwaruhusu watuzingue,” alisema.

“Kwa kupitia umoja wetu tujue kwamba tusipochukua Ikulu mwaka huu itatuchukua miaka 50 ijayo, hivyo nawapeni pole kwa kujiuzulu kwa mwenyekiti wenu,” alisema.

“Ukawa kuna viongozi hodari na imara kwani wamepitia misukosuko mingi sana, lakini wameishinda kwa umoja na mshikamano wangeyumba wangechukulia poa.

“Ukawa ina Mwenyekiti wake, Emanuel Makaidi, Mwenyekiti Freeman Mbowe, James Mbatia ambaye anajua Qur’an na Biblia na Maalim Seif ni hodari sana wa kupatanisha watu na ni mpambanaji asiyekata tamaa nimepata faraja kujiunga nao,” alisema.

POLE YA KUONDOKA LIPUMBA

Lowassa pia alitoa pole kwa wanachama wa CUF kwa kuondokewa na mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba, ikiwamo na kuwapongeza kwa namna walivyolikabili jambo hilo.

“Tatizo la Afrika viongozi wanatumia mamlaka kienyeji sana, wamekuwa wanatengeneza Katiba kwa kuwarejesha madarakani ila hapa tunachotakiwa kufanya ni kuendelea kushirikiana na kuwa na umoja,” alisema.

Alisema mwaka 1995, Rais wa Awamu ya Kwanza Mwalimu Nyerere alipokuwa akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM aliwaambia wanachama wa chama hicho kwamba, ‘watu wengi wanataka mabadiliko hivyo wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM’.

Baada ya kusema maneno hayo, Lowassa alitoa kauli mbiu yake inayosema ‘safari ya mabadiliko wananchi wakajibu ‘nje ya CCM’.

Alisema ujio wake Ukawa, ni kutekeleza maagizo ya Mwalimu Nyerere ya kumtaka kutafuta mabadiliko nje ya CCM ikiwamo na kuandika historia ya nchi ambayo inawezekana.

“Ukawa ikiingia madarakani nchi itatulia tuli…wasiwadanganye kwani tupo imara na Mwenyezi Mungu atatusaidia, kwani wanajaribu kupitisha fedha lakini wajue kuwa viongozi wa Ukawa hawahongeki,” alisema.

 

JUMA DUNI

Naye mgombea mweza wa Chadema, Juma Haji Duni, alisema hakujiunga Chadema kwa ajili ya kutafuta cheo.

“Wanajua nilikuwa waziri lakini nimeacha na juzi nimekwenda kumpelekea barua Rais wa Zanzibar na kuacha, kwa CUF nilikuwa Makamu Mwenyekiti Taifa lakini nimeacha,” alisema.

Alisema sababu kubwa ni kuikomboa Tanzania ambayo imesalitiwa na viongozi wake walioaminiwa kuwa masikini baada ya kufika Ikulu waliwasaliti masikini wenzao.

“Tunashangaa badala ya Rais Jakaya Kikwete kupumzika huku tukimshukuru hata baada ya miezi miwili anatangaza shari, ila nawashukuru wanachama wa CUF kwa kunielewa kwamba nimetumwa na chama ili kushirikiana na kusonga mbele Inshallah kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu Magogoni tutafika,” alisema.

Alisema kama mwaka huu aliouita wa mageuzi wasipoingia Ikulu wajue watahitaji kusubiri miaka 50 zaidi kwa sababu CCM wakitulia watakuwa wagumu kuruhusu wapinzani kuing’oa kirahisi.

“Tunaomba muda wa miaka mitano tuwaonyeshe namna ambavyo Watanzania wanatakiwa kuishi,” alisema.

MAKAIDI

Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Emanuel Makaidi, alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanakusanyika kwa kuwahamasisha wananchi wengine wamsindikize mgombea wa Ukawa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuchukua fomu NEC.

Mwaka huu lazima CCM iondoke kwa kutumia umoja wetu hali inayosababisha CCM kuanza kutetemeka.

Kilichojiri

Kabla ya kuanza kwa mkutano huo ambao mwenyeji wake alikuwa Maalim Seif, alikuwa na kazi ya kuwapokea viongozi wa Ukawa ambapo wa kwanza kufika alikuwa Mbatia aliyefika saa 5:58 akafuatiwa na Makaidi 5:59.

Ilipofika saa 6:30, uliwasili msafara wa mgombea urais wa umoja huo, Lowassa aliyeambatana na Mbowe, Lissu, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, Naibu Katibu Mkuu Chadema-Bara, Salum Mwalimu na viongozi wengine.

Wakati viongozi hao wakiingia wanachama walikuwa wakishangilia kwa kuimba ‘Rais’, ‘Rais’…….na alipoingia ndani ya ofisi hizo za CUF ilisababisha wananchi kufungua geti la chama hicho na kuingia ndani ya ofisi hizo na kusababisha kushindwa kutosha kutokana na wingi waliokuwa nao.

Lowassa, alifika CUF kwa ajili ya kuzungumza na Baraza Kuu, alijikuta akishawishika kuzungumza na wananchi baada ya kuona umati mkubwa wa wanachama uliompokea.

Taarifa kutoka ndani ya CUF, zinasema kuwa mtu pekee anayepewa nafasi kubwa ya kukaimu nafasi ya Profesa Lipumba ni Mbunge wa Afrika Mashariki, Twaha Taslima.

MAALIM SEIF

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar  na Katibu Mkuu wa Chama  cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wanachama wa vyama vinavyounda Ukawa, kushirikiana na kuhamasishana nyumba kwa nyumba ili kupata ushindi dhidi ya CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Seif ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya urais Zanzibar kwa mwamvuli wa Ukawa chini ya tiketi ya CUF, alisema umoja wao hauna kurudi nyuma.

“Ukawa ni mbele kwa mbele kurudi nyuma mwiko, hivyo basi nakuhakikishieni Edward Lowassa anaingia Ikulu mwaka huu na tuiondoe kabisa CCM madarakani,” alisema.

Alisema wanachama wa vyama vinavyounda umoja huo, wanapaswa kushirikiana pamoja na kuhamasishana nyumba kwa nyumba ili kufikia lengo hilo.

“Safari ya matumaini itatimia ikiwa wanachama wanahamasishana ili kuhakikisha tunapata ushindi katika uchaguzi wa mwaka huu. Inshallah Mungu yupo pamoja nasi tunaamini kwa uwezo wake tutashinda,” alisema Seif.

Alisema upande wa Zanzibar, mchakato wa kupata ushindi umekamilika, kilichobaki ni kuapishwa tu baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka huu.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanachama wanapaswa kujenga umoja na ushirikiano ili kuhakikisha ushindi huo unapatikana.

 

FREEMAN MBOWE

 

Mbowe: Safari hii tumeipigania zaidi ya miaka 25

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema safari ya kuingia Ikulu wameipigania kwa zaidi ya miaka 25.

Alisema baadhi ya watu wamefariki dunia, wameumia, wamefilisika, wameachika na wengine wamepata kesi kwa ajili ya kutetea masilahi ya wananchi.

Kutokana na hali hiyo, alisema wakati huu wanapomalizia safari hiyo, wananchi hawapaswi kukata tamaa.

Alisema safari hiyo imekua mbaya zaidi baada ya kuunda Ukawa, ambapo CCM imekua ikitumia fedha kwa ajili ya kuwasambaratisha.

“Ikiwa anaondoka mwanachama mmoja, waliobaki hawapaswi kukata tamaa, bali wanapaswa kujipanga upya na kuhakikisha ushindi unapatikana, lengo ni kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema Mbowe.

Alibainisha wiki mbili zilizopita, Lowassa alikuwa CCM ambapo kwa sasa ni mgombea urais kupitia Chadema, wakati Dk. Juma Duni Hajji alikuwa CUF na sasa yupo Chadema na ni mgombea mwenza wa urais.

“Lengo la kuhama kwa viongozi hawa siyo kutafuta nafasi ya uongozi, ni kutetea masilahi ya wananchi,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanachama wanapaswa kujipanga na kuhakikisha wanapata ushindi kwa zaidi ya asilimia 90 ili waweze kuiondoa CCM madarakani.

 

JAMES MBATIA

Mbatia amtuhumu JK kwa uchochezi

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alimtuhumu Rais Jakaya Kikwete kwa kusema anatoa maneno ya kupandikiza chuki.

Alisema Rais Kikwete alitoa kauli hizo Oktoba 4, mwaka huu wakati Chadema wakiwa kwenye mkutano wa kumpitisha mgombea urais wa chama hicho na CCM ikimpokea mgombea urais wake, Dk. John Magufuli aliyekuwa ametoka kuchukua fomu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Alisema CCM wana uwezo wa kushinda kwenye uchaguzi wa mwaka huu kwa sababu uwezo wa kushinda wanao, sababu ya ushindi wanayo na adui yao ni mtu yeyote aliyekuwa upinzani.

Alisema kauli ya kuwa adui yao ni mtu yeyote aliyekuwa upinzani, siyo nzuri kwa sababu inaweza kuleta chuki kwa wananchi kwa sababu kwenye siasa hakuna uadui.

Alisema katika mkutano huo, pia Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema watu wanaoondoka katika chama hicho ni makapi.

“Nani makapi? Huwezi kumwita binadamu mwenzako makapi hata siku moja, hizi kauli siyo nzuri kwa sababu zinahamasisha chuki.

“Tunapaswa kuwaonyesha wananchi kuwa, Ukawa haina chuki na mtu bali tuna uwezo wa kuongoza nchi,” alisema Mbatia.

Alinukuu Zaburi 20 (6) akisema: “Pasipokuwa na kuni hakuna moto, pasipokuwa na uchochezi hakuna vita”.

Alisema wapinzani hawana chuki na mtu na kwamba wanachama wao wanapaswa kuwapuuza kwa kauli hizo za uchochezi.

Kutokana na hali hiyo, alisema wanapaswa kuunganisha nguvu na kuhakikisha katika uchaguzi wa mwaka huu wanashinda kwa kishindo ili waiondoe CCM madarakani.

Alisema jambo hilo ni rahisi endapo wanachama watahamasishana kujitokeza kupiga kura.

“Toka lini mmeona Ukawa wanamwaga damu! Ukiona mtu anasema wapinzani wachochezi achana naye, ukiona uchochezi unatendeka zuia, ikishindikana kemea, kama umeshindwa kabisa onyesha chuki.

Aliwataka wanachama hao kuichukia CCM kwani imezoea kuonyesha uovu kwa wananchi.

 

LISSU

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, aliwabeza watu wanaosambaza taarifa kwamba, mtu hawezi kuwania urais kama ana chini ya miezi mitatu kwenye chama husika.

Alisema watu hao wanatumia Katiba ya nchi wakisema hairuhusu mtu kugombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa hajatimiza miezi mitatu ndani ya chama husika.

Alisema uvumi huo siyo kweli, ila umesambazwa na baadhi ya watu wasiopenda umoja huo, hivyo basi wanachama wanapaswa kuwa makini na kuhakikisha hawawasikilizi.

Alisema anashangaa kuona baadhi ya watu wameanza kuandika habari za uzushi kwenye mitandao ambao ni ushahidi tosha wa kuwa CCM maji yamefika shingoni wameanza kukamata nyasi, hivyo basi wanapaswa kuwapuuza.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles