NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MGOMBEA urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ameanza kuishambulia Serikali ya awamu ya nne kwa kushindwa kuinua uchumi.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi waliofurika Makao Makuu ya Chadema, muda mfupi baada ya kutoka kuchukua fomu ya uteuzi katika ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Lowassa alisema Rais Jakaya Kikwete, aliyemuita rafiki yake, ameharibu uchumi wa nchi.
“Kitaalamu unaambiwa kwamba ‘No Research no right to speak’, mimi nina data zinazoonyesha namna ambavyo rafiki yangu JK ameuharibu uchumi wa nchi yetu. Wakati Mkapa anaondoka madarakani bei ya sukari ilikuwa Sh 650, lakini sasa ni Sh 2,500. Mchele ulikuwa Sh 550 leo hii ni Sh 2,200. Sembe ilikuwa Sh 250 lakini sasa ni 1,200. Je, Rais Kikwete hajauharibu uchumi?” aliwahoji wananchi waliojibu kwamba kauharibu.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliendelea kuwaeleza wanachama hao kuwa hata bei ya kiberiti iliyokuwa shilingi 50, lakini leo imefikia shilingi 200.
“Yapo mengi sana ambayo yanadhihirisha kuwa uchumi wetu umeharibiwa, nauli za daladala zimepanda, kila kitu kimepanda, sasa ni muda wa kuiambia CCM bye bye. Katika hali ya kawaida CCM haina haki ya kuendelea kuongoza taifa hili kwa kuwa imeharibu uchumi wetu,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na umati huo.
Lowassa alisema maandamano yaliyomsindikiza yanadhihirisha kauli aliyopata kuitoa Mwalimu Nyerere mwaka 1995 katika Mkutano Mkuu wa CCM, kwamba mabadiliko yasipopatikana ndani ya CCM yatapatikana nje ya chama hicho.
“Waangalie maandamano ya vijana, haijawahi kutokea kwa maandamano hayo yanayoashiria kwamba wananchi wamepoteza matumaini na CCM.
“Wako watu waliokuwa wakivisema vibaya vyama vya Chadema na CUF kuwa ni vyama vya fujo, sasa nimeamini kwamba ni waongo, leo tumewahakikishia kuwa tuna nidhamu na tutachukua nchi asabuhi kweupe na wataisoma namba.
“Narudia tena nauchukia umasikini, nauona kama ukoma, sasa nakwenda Ikulu kupambana na huo umasikini. Sasa ninawaomba kwa nidhamu ambayo mmeionyesha leo, muitumie kupigia kura Ukawa Oktoba 25, mwaka huu. Wale wana mbinu nyingi, lakini sisi kitakachotuingiza madarakani ni kura,” alisema.
Alisema wengi walioandamana kumsindikiza ni vijana, hivyo akiingia Ikulu kazi kubwa atakayoifanya ni kushughulika na matatizo yao.
“Nitaunda Serikali itakayojenga uchumi kwa ‘speed’ kali, kama mtu hawezi akae pembeni, tumekuwa nchi ya ajabu sana, hata shirika la ndege tunashindwa na Rwanda, bandarini mashine inalala, watu wanalala, sisi tutaanza na mchakamchaka wa maendeleo,” alisema Lowassa.
Kuhusu suala la Serikali ya awamu ya nne kutokomeza tembo, Lowassa alisema kipindi hiki wanyama hao na wengine wameuawa kwa wingi na kuandika historia tangu kuasisiwa kwa nchi hii.
“Kila mnyama ameuawa kwa wingi kuliko muda mwingine wowote katika historia katika historia ya nchi yetu,” alisema.
Lowassa pia alisema, waliojitokeza kumsindikiza wengi vijana hivyo anachukua dhamana kwao na atahakikisha atawapigania ili wawe na uchumi mzuri.
MBATIA
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, aliyaelezea maandamano hayo kuwa yameandika historia mpya ambayo ni elimu tosha kwa Watanzania.
“Elimu iliyotolewa na Watanzania hii leo walioanza kuandamana asubuhi Makao Makuu ya CUF Buguruni hadi saa 11:45 tunafika hapa ofisi za Chadema, wanaonyesha namna wanavyotaka kulikomboa taifa,” alisema.
Mbatia alisema takribani miaka 24 hajawahi kushuhudia halaiki ya watu wengi kama aliyoishuhudia kwenye maandamano yaliyofanyika jana.
“Mtume Muhammad (S.A.W) anasema mwenye kutaka dunia lazima apate dunia na mwenye kutaka ahera lazima apate elimu, na kila anayeipata elimu aichukue.
“Katika Biblia Zaburi 125:5, inasema Taifa likiachwa likitawaliwa na waovu, watu waadilifu wasiachwe wakawatawala kufanya maovu, hivyo hatusubiri katu kuacha taifa kutawaliwa na waovu,” alisema.
Alisema kwa maandiko hayo matakatifu, mgombea wa Ukawa, Lowassa lazima atakuwa rais wa Jamhuri ya Muungano bila fujo yoyote kama ilivyotokea katika maandamano ya kumpeleka kuchukua fomu NEC.
Mbatia alisema pamoja na kukimbiwa na Profesa Lipumba, akafikiria kwamba Ukawa ingeparaganyika, lakini imeendelea kuwa imara.
Mbatia alitoa wito kwa Rais Kikwete na wenzake kuchunga ndimi zao ili pindi Lowassa atakapoapishwa waweze kumtunuku nishani ya heshima.
MAALIM SEIF
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema Lowassa ameletwa na Mwenyezi Mungu kwa makusudi ya kuleta matumaini mapya kwa Watanzania.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, aliwataka wananchi waliohudhuria hapo kuhakikisha wanatumia kura ili kuiondoa CCM, hivyo aliwaomba kuchunga shahada zao za kupigia kura.
Alipinga taarifa ambazo zinasambazwa kwamba amedhamiria kuvunja Muungano jambo alilosema lilianzishwa na CCM.
“Maalim Seif nimekuwa nikipambania kuwepo kwa Serikali tatu zilizo na haki sawa kwa Watanganyika na Wazanzibar ambazo zitafanikishwa na katiba mpya,” alisema.
- MAKAIDI
Mwenyekiti wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Dk. Emmanuel Makaidi, alisema tangu azaliwe hajawahi kuona umoja kama huo.
“Kutokana na umati ambao leo umejitokeza, kama ningekuwa mimi nipo serikalini ningejiuzulu mapema, hadi sasa Lowassa na wenzake wanasubiri kuapishwa tu bila ubishi,” alisema.
Aliwaomba wanachama wa CCM kukubali matokeo mapema ili wasipoteze muda.
“Mimi nina ndugu yangu ambaye yupo CCM, pamoja na wanachama wengine watusaidie waje Ukawa ili kazi iwe rahisi.
“Kwa kilichotokea Dar es Salaam kama uso wa nchi, na mambo yaliyotokea leo ndiyo yalitokea nchi nzima, hiyo ni dalili ya kwamba wakati wa kuja Ukawa umefika, hivyo Oktoba 25 CCM bye bye, ” alisema Makaidi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Mohamed, alisema kuwa ushindi wa Lowassa upo wazi kutokana na historia yake ambayo inampeleka moja kwa moja Ikulu.
“Kwa Waislamu na Wakristo wasome kuran na Biblia watafahamu hatima ya Mussa aliyewaokoa wana wa Israel pamoja na Yusufu aliyenyanyaswa na kufanyiwa vitendo vya ukatili na ndugu zake, hivyo niwahakikishie dalili za ushindi zimekamilika In-sha-Allah, In-sha-Allah,” alisema.
YALIYOJIRI
Msafara wa Lowassa ulianzia katika ofisi za CUF, Buguruni saa nne asubuhi na kuelekea katika ofisi za NEC ambako uliwasili saa nane mchana, lakini walishindwa kuruhusiwa kuingia ndani kutokana na umati mkubwa ulioanzia Maktaba ya Taifa.
Waandamanaji walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kuwasifia viongozi ikiwamo “Kama sio nguvu zako baba na kama sio juhudi zako Nyerere na kama sio juhudi zako Mbowe… Lowassa tungempata wapi.”
Wimbo mwingine ulikuwa ni ‘Si mnaona muziki wa Lowassa… Magufuli atauweza wapi?’
Pia kuliwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali ikiwamo “Afe beki, afe kipa rais ni Lowassa 2015.”
Habari hii imeandaliwa na Elizabeth Hombo, Shabani Matutu, Aziza Masoud, Adam Mkwepu na Valentina Joseph (TUDARCO).