28.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA AFUNIKA DAR ES SALAAM

LOWASSANA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

JIJI la Dar es Salaam limezizima kwa takribani saa 13 jana wakati maelfu ya wafuasi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walipomsindikiza mgombea urais wa umoja huo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Wafuasi hao ambao hawakuonyesha kuchoka wala kupata muda wa kula, walianza kufika ofisi za makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), Buguruni kuanzia saa 11:00 alfajiri kumsubiri Lowassa na viongozi wengine wa Ukawa.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wafuasi hao wa Ukawa inayoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, walitembea kwa miguu kutoka ofisi hizo hadi katikati ya jiji – maeneo ya Posta, zilipo ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, umbali unaokadiriwa kufikia kilometa 20, jambo ambalo pia lilimshangaza Lowassa asiamini kilichotokea.

Lowassa alionyesha mshangao huo wakati akihutubia umati mkubwa wa watu waliomsubiri makao makuu ya Chadema, ambapo alisema tangu azaliwe hajawahi kuona msafara mkubwa kama huo, ambao ulisababisha wafanyabiashara wengi kusimamisha shughuli zao na kusimama barabarani kushuhudia na kupunga mikono.

Wafuasi hao wa Ukawa ambao walikuwa wamevalia sare rasmi za vyama vyao, walianza kuingia eneo la Makao Makuu ya CUF wakiimba nyimbo mbalimbali na wengine wakiwa wameshika mabango yenye ujumbe tofauti.

Ofisi za CUF ambazo zimezungukwa na soko kubwa la Buguruni, lilizingirwa na watu wengi kupita kiasi kadiri muda ulivyokuwa unakwenda.

 

MAALIM SEIF AWAHI KUKARIBISHA WAGENI

Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), Maalim Seif Sharif Hamad, ndiye aliyekuwa wa kwanza kufika katika ofisi hizo na kupokea wageni mbalimbali waliokuwa wakihudhuria.

Maalim Seif ambaye alionekana mwenye furaha muda wote, alianza kupokea viongozi mbalimbali wa vyama vinavyounda Ukawa, miongoni mwao ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi , James Mbatia, Mwanasheria Mkuu wa Chadema , Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, John Mnyika.

Wengine ni wabunge wanaomaliza muda wao, Makongoro Mahanga (Segerea), James Lembeli (Kahama) waliohamia Chadema hivi karibuni kutoka CCM, Godbless Lema (Arusha Mjini) na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini).

Wengine ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema , (Bavicha), Patrobas Katambi na viongozi wa ngazi mbalimbali wa vyama vya siasa.

 

LOWASSA AWASILI

Lowassa alifika katika ofisi za CUF saa 11.12 asubuhi akiwa kwenye gari T 878 CFU Nissan Lexas na mkewe Regina akitumia gari T 841 CYP Nissan V8, huku wakiwa wamezingirwa na ulinzi mkali.

Alipokaribia ofisi hizo, umati wa mashabiki ulilipuka kwa furaha, huku wakiimba “rais… rais… rais…” na kupunga hewani bendera, skafu na picha mbalimbali za Lowassa pamoja na mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji.

Katika eneo zilipo ofisi za CUF kulikuwa na ulinzi mkali ambapo vijana wa Blue Guard wa Chadema na Red Guard wa CUF, wakiwamo wacheza ‘karate’ waliokuwa wamevalia mavazi yao rasmi, walikuwa wamelizunguka eneo hilo.

Hali hiyo ilisababisha utulivu wa aina yake ambapo baadhi ya watu walisikika wakisema kwamba hata vijana waporaji wa eneo la sokoni walikuwa wamepumzika kwa siku ya jana.

Magari matatu yanayomilikiwa na vyama vya CUF na Chadema yalikuwa kivutio cha aina yake ambapo yalikuwa yakitoa burudani na kuwafanya wafuasi wa Ukawa kucheza muda wote bila kuchoka.

Kutokana na hamasa kuwa kubwa, kundi la wafuasi hao lilianza kuondoka katika eneo la makao makuu ya CUF kwa maandamano kuelekea ofisi za NEC hata kabla Lowassa na viongozi wengine wa Ukawa hawajafika.

Hali hiyo ilionekana kuwatisha askari polisi waliokuwa kwenye magari yao, ambao waliamua kusindikiza umati huo kwa mwendo wa taratibu bila bughudha.

Wafanyabiashara, wafanyakazi na watu mbalimbali walijikuta wakilazimika kusimamisha shughuli zao ilimradi waupungie mkono msafara wa Lowassa uliopitia Mtaa wa Uhuru hadi Mnazi Mmoja na kuelekea Posta wakitumia Barabara ya Bibi Titi Mohamed.

 

POLISI WATAKA KUZUIA MAANDAMANO

Saa 4:44 asubuhi, viongozi wa Ukawa walikuwa katika ofisi za CUF tayari kwa ajili ya kuanza msafara wa kwenda NEC, ambapo polisi kwa kushirikiana na Kikosi cha Usalama Barabarani wakiwa na silaha, walifika wakiwa na askari wengi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), ambao walikuwa wakitumia magari yenye namba PT 2081  Landrover, PT 2561 Suzuki na T 337 AKV  Land Cruiser.

Askari hao waliingia moja kwa moja ndani ya geti la ofisi za CUF hali iliyosababisha taharuki kwa wafuasi wa Ukawa ambao walisogea ili kujua kinachoendelea.

Baadhi ya wananchi walianza kuhofia kauli iliyotolewa awali na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kwenye vyombo vya habari, akizuia watu kuandamana kumsindikiza Lowassa katika ofisi za NEC.

Hata hivyo, baada ya mazungumzo kati ya askari hao na viongozi wa Ukawa, walipata mwafaka na hivyo msafara wa Lowassa na mgombea mwenza wake ulianza safari rasmi ya kuelekea ofisi za NEC saa 6:15.

 

VITUKO

Baadhi ya wafuasi wa Ukawa waligeuka kivutio cha aina yake kutokana na kuiga watu mbalimbali, ambapo kijana mmoja maeneo ya kituo cha mabasi cha Rozana, ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja, alijipaka chokaa kichwani kisha kuanza kutembea barabarani huku watu wakimshangilia wakidai ni Lowassa.

Kijana huyo alibebwa juu juu, huku watu wengine wakimpiga picha kwa ajili ya kumbukumbu zao.

Kijana mwingine ambaye naye pia jina lake halikufahamika mara moja, aliyekuwa amejifunga mabegani shati la kijani, alijilaza barabarani maeneo ya Kariakoo akijifanya kukata roho, akimaanisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiyo mwisho wake.

 

MABANGO

Baadhi ya wafuasi hao walibeba mabango yenye ujumbe mbalimbali kama; “Huwezi kuzuia mafuriko kwa mkono”, “Iwe jua au mvua mabadiliko ni lazima”, “Twende pamoja na Lowassa hadi Ikulu 2015”, “Lowassa Rais Wetu”, “Nape bao la mkono utajifunga mwenyewe”, “Tumechoshwa na CCM miaka 51 wanafunzi hawana madaftari”, na “Tawile miaka 51 tumechoka kupiga ramli”. Wengine walibeba mbao zilizochongwa kama funguo wakimaanisha funguo ya mlango wa Ikulu.

Kutokana na msafara kuwa mrefu, wakati Lowassa na wenzake wakianza kuondoka ofisi za CUF Buguruni, msafara wa kwanza wa watembea kwa miguu tayari ulikwishafika ofisi za NEC.

Msafara wa Lowassa ulitanguliwa na pikipiki na kufuatiwa na magari ya kila aina.

Wakati msafara huo ukielekea Posta, watu waliokuwa wamesimama kandokando ya barabara walikuwa wakionyesha ishara ya vidole viwili juu na wengine wakipunga hewani vitambulisho vya kupigia kura, huku wakihanikiza maneno ya kejeli kwa CCM.

 

LEMA ADANDIA BODABODA

Mbunge wa Arusha Mjini, Lema, alishangaza watu baada ya kuamua kupanda bodaboda eneo la Malapa.

 

WAFANYABIASHARA

Wafanyabiashara ndogo ndogo wa soko la Kariakoo, maarufu kama machinga, walisimama eneo la makutano ya mitaa ya Uhuru na Msimbazi, na wengine walijiunga kwenye msafara wa Lowassa kuelekea NEC.

Wakizungumza na gazeti hili, wafanyabiashara hao, walisema kushiriki kwenye maandamano hayo ni njia mojawapo ya kuonyesha kuwa wapo pamoja na Lowassa katika uchaguzi ujao.

“Tuko hapa kumuunga mkono rafiki yetu na ndugu yetu Lowassa, ili kuuonyesha umma kuwa tunamjali, tunamuheshimu na tunapaswa kumuunga mkono wakati wa kuchukua fomu,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah Salum.

Aliongeza wamehamasishwa na hoja za Lowassa kuchukia umasikini, kwamba hilo limewapa matumaini makubwa na kuamua kumuunga mkono.

“Hakuna fedha zozote zilizotolewa zaidi ya mapenzi yetu kwake, ndiyo maana tumejitokeza kwa wingi ili tuweze kumuunga mkono, tuna imani anaweza kupata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu,” alisema.

Alisema mkakati wao ni kuhakikisha kuwa CCM inaondoka madarakani katika uchaguzi wa mwaka huu na kubaki kuwa chama cha upinzani kama ilivyo kwa vyama vingine.

“Kuiondoa CCM madarakani ni kitu rahisi sana kwa sababu tumejipanga, tumedhamiria na tutahakikisha tunapata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi huu,” alisema.

 

WANAFUNZI

Katika eneo la Chuo Cha Teknolojia (DIT), wanafunzi waliokuwa wamesimama pembezoni mwa barabara, walikuwa wakiimba; “Kama sio juhudi zako Nyerere na Lowassa angetoka wapi”, huku wengine wakiimba; “Kama siyo juhudi zako JK na Lowassa tungempata wapi.”

Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na MTANZANIA walisema kuwa hawawezi kumwacha Lowassa, na kwamba wataendelea kumuunga mkono hadi dakika ya mwisho kwa sababu wanaamini anaweza kuwapa maisha bora, ajira, mikopo ya vyuo vikuu pamoja na mazingira mazuri ya kusoma.

Habari hii imeandikwa na ARODIA PETER, PATRICIA KIMELEMETA na ESTHER MNYIKA

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles