23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa kidedea

2*Aongoza kwa asilimia 54.5

*Asema Serikali dhaifu imesababisha migogoro

 

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

 

UTAFITI mpya uliofanywa na Taasisi ya Tanzania Development Initiative (TADIP) umeonyesha mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, angeshinda kwa asilimia 54.5 kama Uchaguzi Mkuu ungefanyika ndani ya wiki tatu za Septemba mwaka huu huku mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, angepata asilimia 40.

 

Matokeo ya utafiti huo yametolewa ikiwa ni siku chache baada ya wiki hii Taasisi ya Twaweza kutoa matokeo ya utafiti wao yaliyoonyesha kama kura zingepigwa Agosti na Septemba, mwaka huu, Dk. Magufuli angeshinda kwa asilimia 65 na Lowassa akipata asilimia 25, pia utafiti mwingine uliotolewa juzi na Kampuni ya Ipsos zamani ikijulikana kwa jina la Synovate, ulionyesha kuwa Dk. Magufuli angeshinda kwa asilimia 62 kama uchaguzi ungefanyika Septemba, mwaka huu huku Lowassa akipata asilimia 31.

 

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utafiti huo mpya Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Bodi ya TADIP, George Shumbusho, alisema utafiti huo umefanywa katika mikoa 10 yenye wapiga kura wengi zaidi ndani ya wiki tatu za Septemba, mwaka huu na moja ya swali waliloulizwa wananchi ni mgombea yupi wangemchagua kuwa rais ikiwa uchaguzi ungefanyika siku taarifa ya utafiti huo ulikuwa ukikusanywa.

 

“Utafiti ulifanywa kuanzia Septemba nne mpaka Septemba 23 na asilimia 54.5 ya washiriki walijibu kwamba wangemchagua Lowassa, asilimia 40 walisema wangemchagua, Dk. Magufuli huku asilimia mbili walisema wangemchagua Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo,” alisema Shumbusho.

Pia alisema asilimia 0.4 walisema watamchagua Hashim Rungwe kutoka Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma) na asilimia 0.1 walisema wangemchagua mgombea wa Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), Chifu Lutalosa Yemba, wakati asilimia tatu walisema hawajui wangemchagua nani.

 

Katika kipengele cha kukubalika kwa mikoa, alisema Lowassa anaungwa mkono zaidi katika mikoa minne ya Kilimanjaro kwa asilimia 73, Tanga kwa asilimia 70, Arusha kwa asilimia 67 na Dar es Salaam kwa asilimia 55 wakati Dk. Magufuli akiungwa mkono zaidi katika mikoa miwili ya Dodoma kwa asilimia 53 na Morogoro kwa asilimia 63.

Shumbusho alisema kwa upande wa umri, Lowassa anaonekana kuungwa mkono zaidi na vijana na watu wenye umri wa kati  ya miaka 18 hadi 47 wakati watu wazima wenye umri wa juu ya miaka 47 wanamuunga mkono Dk. Magufuli.

 

Pia alisema utafiti huo uliangalia kukubalika kijinsia ambapo wanaume wanaomkubali Lowassa ni asilimia 58 wakati wanawake ni asilimia 48 huku Dk. Magufuli anakubaliwa na wanaume kwa asilimia 36 na wanawake kwa asilimia 48.

Kuhusu uanachama na ufuasi, alisema utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia 35 ya wananchi walisema ni wafuasi wa CCM wakifuatiwa na Chadema kwa asilimia 32  huku wananchi walioonyesha kutokuwa na ufuasi ama uanachama ni asilimia 25.

 

“Chama cha ACT-Wazalendo kina wafuasi kwa asilimia tatu wakati NCCR-Mageuzi ikiwa na asilimia moja na asilimia mbili ilikuwa ni kwa vyama vingine vilivyobaki,” alisema Shumbusho.

 

MATOKEO YA UBUNGE

 

Akizungumzia nafasi ya ubunge, Shumbusho alisema matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa CCM kingeongoza kwa kupata wabunge kwa asilimia 40 ikifuatiwa na Chadema kikipata asilimia 30.

 

Alisema asilimia 20 ya wahojiwa walisema wangechagua mgombea wa Ukawa katika nafasi ya ubunge wakati ACT-Wazalendo kikipata asilimia tatu, CUF kikipata asilimia mbili na NCCR na TLP kila kimoja kikipata asilimia mbili.

 

MATOKEO YA UDIWANI

 

Katika nafasi ya udiwani alisema wagombea wa CCM wanaongoza kwa uwezekano wa kupigiwa kura kwa asilimia 37 wakifuatiwa na Chadema kwa asilimia 31 wakati waliotaja Ukawa ni asilimia 20  na ACT-Wazalendo ni asilimia tatu, CUF asilimia tatu huku NCCR-Mageuzi ikiwa na asilimia mbili na asilimia mbili ya wananchi walisema hawajui.

 

METHODOLOJIA

Kuhusu methodolojia waliyoitumia katika utafiti huo, Mshauri Mwelekezi wa TADIP, Constatine Deus, alisema ulifanywa kwa wiki tatu za kwanza za Septemba, mwaka huu ukihusisha watu waliojiandikisha kupiga kura katika mikoa 12 ya Tanzania Bara huku mtizamo ukijikita zaidi katika mikoa iliyothibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

 

Alisema watu 2,500 walilengwa kupewa madodoso huku watu 2,040 pekee walishiriki kwa maana ya kuyarejesha.

 

“Utaratibu wa kuchagua washiriki ulifanyika kwa njia nasibu huku kila mkoa walengwa wakigawanyika katika makundi matatu ya maeneo, mijini, miji midogo na maeneo ya pembezoni,” alisema Deus.

 

Mshauri huyo alisema wakusanya taarifa pia walichagua washiriki kwa kuzingatia uwakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii kama vile jinsia, kiwango cha elimu, umri wa washiriki na kadhalika.

Alisema kwa mujibu wa matokeo, asilimia 51 ya waliohojiwa katika utafiti walikuwa watu wenye umri kati ya miaka 18 hadi 28 wakifuatiwa na watu wenye umri kati ya miaka 29 na 39 waliokuwa sawa na asilimia 30.

 

“Watu wenye umri kati ya miaka 40 hadi 49 walikuwa sawa na asilimia 10, miaka 50 hadi 59 walikuwa asilimia saba na wenye umri wa miaka 60 walikuwa na uwakilishi wa asilimia mbili,” alisema Deus.

Alisema asilimia 38 ya wahojiwa walikuwa na elimu ya sekondari, asilimia 37 walikuwa wa elimu ya msingi wakati wananchi wenye elimu ya shahada ya kwanza walikuwa asilimia 10 na asilimia saba ni ngazi ya chuo na cheti.

 

Alisema watu wasiosoma katika mfumo rasmi wa elimu ni asilimia nne wakifuatiwa na watu wenye elimu stashahada asilimia tatu wakati idadi ya washiriki wenye elimu ya uzamili iliwakilishwa kwa asilimia 0.3 na uzamivu iliwakilisha asilimia ndogo zaidi ya 0.1.

 

MCHAKATO WA KUPIGA KURA

Katika mchakato wa upigaji kura, Shumbusho, alisema wananchi waliulizwa ikiwa wanadhani upigaji kura utafanyika kwa uhuru na haki asilimia kubwa ya wananchi walisema ndiyo.

 

Alisema asilimia 89 ya wananchi walisema kuwa wanadhani upigaji kura utakuwa huru na haki ikilinganishwa na asilimia nane waliosema hapana na asilimia tatu walisema hawajui.

TAFITI YA MEI NA JUNI

Shumbusho alisema awali walifanya utafiti kuhusu vipaumbele vya wananchi na zaidi ya asilimia 80 ya wananchi walitaja elimu wakati asilimia 75 walitaka afya na kipaumbele cha maji kilikuwa asilimia 63.

 

Alitaja kipaumbele kingine kuwa ni kilimo na kilikuwa asilimia 58 wakati ajira ni asilimia 45 huku rasilimali zikiwa asilimia 38, rushwa asilimia 23 na viwanda asilimia 24.

 

Wakati huo huo, mwandishi wetu Fredy Azzah kutoka wilayani Simanjiro anaripoti kuwa Lowassa amesema Serikali iliyopo madarakani na viongozi wake ni dhaifu ndiyo maana wameshindwa kumaliza mgogoro wa wakulima na wafugaji wilayani Kiteto, pia pamoja na matusi yote yanayoendelea watawajibu katika masanduku ya kupigia kura siku ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

 

Lowassa alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti alipokuwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana katika Viwanja vya Soweto vilivyopo Kijiji cha Matui Wilaya ya Kiteto na ule uliofanyika katika Viwanja vya Soko la Getini eneo la Mererani, wilayani Simanjiro.

 

“Sisi hatuna haja ya matusi yao, sisi tulichonacho ni kichinjio tu cha kura (kadi ya kupiga kura), wafundisheni adabu kwenye kichinjio,” alisema Lowassa katika mkutano uliofanyika Mererani na kuhudhuriwa na maelfu ya watu.

 

SERIKALI DHAIFU

 

Akiwa Kiteto, Lowassa alisema Serikali iliyopo madarakani pamoja na viongozi wake ni dhaifu na ndiyo maana wameshindwa kumaliza mgogoro wa wilayani Kiteto.

 

 

“Mgogoro huu umefikia hapa kutokana na udhaifu wa viongozi na Serikali, kuna watu waliopoteza maisha na wengine wamenyang’anywa mashamba.

 

“Walionyang’anywa mashamba watarudishiwa kama tume imeona inatakiwa ifanyike hivyo na hiyo tume ndiyo itakuwa mwarobaini wa mgogoro huu,” alisema Lowassa.

Neema kwa wachimbaji

 

Akiwa Mererani, alisema endapo akipata nafasi ya kuingia madarakani, atahakikisha asilimia 50 ya Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Tanzania One, atazigawa kwa wananchi huku wachimbaji wadogo wadogo wakianzishiwa benki yao.

 

“Tatizo la Tanzanite one mkishanipa kura nakusudia asilimia 50 tutatoa kwa wananchi, wachimbaji wadogo wadogo mpate benki yenu binafsi, lazima kuwasaidia ili muweze kuendelea,” alisema Lowassa.

 

NADEKA

 

Alisema mapokezi makubwa aliyopata kutoka kwa wananchi wa Mererani, yanamfanya adeke kwa sababu yupo nyumbani.

 

“Kwanza nadeka, nikiangalia umati wote uliokuja kunipokea nadeka kweli maana nipo nyumbani, asanteni sana kwa mapenzi yenu, nimekuja kuwaomba kura, nahitaji kura kama milioni 14 na ushee, nataka kura nyingi ili hata wakiiba zibaki nyingi, siyo kupiga kura tu na pia mzilinde,” alisema Lowassa.

 

Alisema katika jimbo hilo kuna kura 16,000 hivyo ni vyema wakahakikisha wanampigia yeye na kisha kuzilinda.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles