29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA AZUA MJADALA NDANI, NJE CHADEMA

ASHA BANI Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM


SIKU moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kukutana Ikulu na Rais Dk. John Magufuli, uamuzi huo umezua mjadala ndani na nje ya chama chake cha Chadema.

Hatua hiyo imeonekana kupokewa kwa hisia tofauti na viongozi wa chama hicho na wasomi, huku wengine wakipongeza na kupinga hatua hiyo.

Wakizungumza na MTANZANIA jana, wanasiasa, wasomi na wachambuzi wa siasa, wamesema kuwa hatua hiyo sasa inaweza kufungua ukurasa mpya wa kisiasa nchini.

Lowassa, juzi alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli kwa dakika 45, huku taarifa ya Ikulu ikieleza kuwa mwanasiasa huyo alimpongeza kiongozi huyo wa nchi kwa kazi nzuri anayoifanya.

 

PROF. SHARIFF

Akizungumzia kukutana kwa viongozi hao, Profesa Abdul Shariff, alisema hana uhakika kama Lowassa alifikisha ujumbe na ajenda za wapinzani ambazo wamekuwa wakizilalamikia mara kwa mara.

Profesa Sharrif ambaye pia ni mtaalamu wa sheria, alisema kuwa iwapo Lowassa alikwenda kusifu na anataka kurudi CCM, ni haki yake na hakuna kipengele kinachomzuia.

“Kama kweli alifikisha ujumbe huo, alitakiwa alipotoka katika mkutano huo aseme walichozungumza, lakini ametoka na kusifia tu kama tulivyoona katika vyombo vya habari.

“Sikushtuka kwani Lowassa alihama CCM kutokana na kunyimwa nafasi ya kugombea urais tu na hakuwa na sababu nyingine, hivyo ikitokea anataka kurudi ni sawa kwa kuwa uchaguzi umeisha na sababu iliyomwondoa imepita,” alisema Profesa Shariff.

 

PROF. BAREGU

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Profesa Mwesigwa Baregu, alimtaka Lowassa ajitokeze hadharani na kueleza kwa umma ajenda iliyompeleka Ikulu ili kuondoa minong’ono iliyotawala.

Alisema kitendo cha yeye kutoka Ikulu na kukaa kimya kinazua maswali na minong’ono miongoni mwa Watanzania hali inayosababisha watu washindwe kuelewa dhamira yake.

“Ni haki yake kwenda huko kama Mtanzania yeyote, kikubwa tunachotaka kukijua ni ajenda iliyompeleka,” alisema Profesa Baregu.

Baregu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema iwapo alichozungumza na Rais Magufuli ni kile ambacho kimetolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, basi atakuwa hajamshauri mambo mengi kiongozi huyo wa nchi.

“Atakuwa amekosa fursa ya kumshauri Rais kuhusu hali ya usalama inavyoendelea nchini kwani ni mbaya na hakuna majibu ya nani anayefanya mauaji katika maeneo mbalimbali, ikiwamo mauaji ya Kibiti na kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

“Pia kuna matukio mengine kama kuokotwa kwa miili katika ufukwe wa Bahari ya Hindi, kutekwa na kupotea kwa watu nchini,” alisema Profesa Baregu.

Alisema jambo jingine ambalo alitakiwa kumweleza Rais ni hali ya uchumi nchini ambayo inaonekana kudorora.

“Japo wanakataza kusema vyuma vimekaza, lakini hali ya uchumi nchini ni ngumu, tunaona mabenki yakifungwa na mambo mengi hayaendi sawa,” alisema Profesa Baregu.

Alisema alipaswa pia kumshauri Rais Magufuli juu ya hali ya kisiasa nchini ambayo inaonekana dhahiri kuwa kuna uminywaji wa demokrasia na uvujwaji wa katiba ya nchi.

“Yeye alisema anao ushahidi wa kuibiwa kura zake, sasa kama amepata ushahidi mwingine kuwa uchaguzi ulikuwa wa haki awaeleze wananchi. Labda ameamua kurudi katika chama chake cha awali CCM ili kujipanga kwa uchaguzi wa 2020,” alisema Baregu.

 

PROF. JESSE

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kitivo cha Sheria, Profesa James Jesse, alisema hatua ya kukutana kwa viongozi hao wakuu wa kisiasa ni isahara njema kwa taifa.

Alisema Lowassa na Magufuli walichuana vikali katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, hivyo kitendo cha kukutana kinaonyesha hawana tofauti na kunaweza kumaliza uhasama wa kisiasa katika baadhi ya maeneo ambayo chuki ilianza kutawala.

“Siasa zinaweza kubadilika katika baadhi ya maeneo na hii ni ishara njema na ni yenye tofauti kubwa na si kubaki na siasa za uhasama. Kukaa meza moja na kuzungumza kunaweza kukawa na maendeleo katika taifa kutokana na mashauriano wanayoyafanya viongozi hao wawili,’’ alisema Profesa Jesse.

 

CUF MAALIM SEIF

Akizungumzia kukutana kwa wanasiasa hao, Mkurugenzi wa Habari Uenezi, Uhusiano na Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), upande wa Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad, Salim Bimani, alisema hatua hiyo inaweza ikawa na busara kama Lowassa alikwenda kumwomba Rais aweze kuruhusu mikutano ya siasa, kukosoa pale anapokosea.

“Kama pia alikwenda akamshauri watu kuwa na uhuru wa kutoa maoni yao, kukosoa kama Serikali inakosea, kuendelea na mchakato wa kupata katiba mpya, kufanya mikutano ya siasa na hata Bunge kuonekana mubashara, basi atakuwa hajakosea yupo sahihi, lakini si vinginevyo,’’ alisema Bimani

 DK. BANA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema hatua ya kukutana kwa viongozi hao ni nzuri na imeandika historia mpya kwa taifa………

Kwa habari zaidi, jipatie nakala yako ya MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles