24.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

DJUMA ATISHIA NAFASI YA KICHUYA SIMBA

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM


KAIMU kocha mkuu wa timu ya Simba, Masoud Djuma, ametishia nafasi ya winga Shiza Kichuya, baada ya kuamua kutoa nafasi kwa kila mchezaji wa Simba kuonesha kiwango chake uwanjani ili kumshawishi kupata nafasi kikosi cha kwanza.

Uamuzi huo unatokana na kitendo chake cha kufanya mabadiliko katika mchezo wa juzi dhidi ya URA ya Uganda katika  Kombe la Mapinduzi, kumchukiza  Kichuya ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Mohamed Ibrahim ‘MO’.

Kichuya ambaye hucheza kama mchezaji tegemeo katika kikosi cha Simba, hakuonesha kufurahishwa na kitendo cha kumpumzishwa na kocha huyo ambaye alichukua nafasi ya kocha Mcameroon Joseph Omog.

Simba iliondolewa katika Kombe la Mapinduzi baada ya kufungwa bao 1-0 na URA na kushindwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, ambayo inafika tamati Januari 13, mwaka huu.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Djuma alisema alipojiunga Simba alikutana na mfumo ambao haukuwa ukitengeneza nafasi nyingi za mabao, hivyo akalazimika kutumia mfumo ambao una tija katika kupatikana kwa mabao mengi pia unatoa nafasi ya kuwatumia wachezaji tofauti ili kupata matokeo mazuri.

“Nilipofika Simba nilikutana na timu yenye wachezaji wengi wa kati lakini haikuwa ikitengeneza nafasi nyingi ya kupata mabao, hivyo ilinilazimu kubadili mfumo wa kunipa nafasi ya kuwatumia wachezaji tofauti.

“Mfumo wangu unatoa nafasi nyingi ya kuwatumia wachezaji tofauti hata wale ambao hawakuwa wakipata nafasi, lakini sasa nawatumia na kulingana na wingi wa wachezaji sitarajii kumtumia mchezaji mmoja katika kila mchezo ni jambo lisilowezekana,” alisema Djuma.

Djuma alisema kuwa ni jukumu la mchezaji husika kuonesha uwezo wake lakini suala la nani atacheza nafasi gani kwa muda gani litabaki kuwa chini yake kutokana na mahitaji ya mfumo anaoutumia.

“Tatizo wachezaji bado hawajaelewa mfumo wangu ila watakapoelewa hawatapata shida kila kitu kitaenda vizuri, hiyo ndiyo sababu ya kufanya vibaya katika michuano ya Mapinduzi lakini tutakwenda kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza.

Akizungumzia kitendo kilichooneshwa na Kichuya, Djuma alisema ni tabia ya kila mchezaji si Afrika tu, ila duniani kote wakati timu inapotaka ushindi.

“Kila mchezaji anayo tabia ya kutaka ushindi hivyo wachezaji aina ya Kichuya wapo duniani kote pale timu inapokosa kufikia lengo huchukia,” alisema Djuma.

Akizungumzia mchezo dhidi ya URA, Djuma alisema: “Ni mchezo ambao ulikuwa na presha kubwa tulihitaji ushindi na wapinzani wetu walihitaji hilo, tumeondolewa mashindanoni hivyo tunapaswa kuangalia Ligi Kuu kuhakikisha tunafanya vyema.”

Katika mchezo huo dhidi ya URA, Djuma aliwatoa Shiza Kichuya, Nicholous Gyan, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin na Mwinyi Kazimoto, nafasi zao zilichukuliwa na Mohamed Ibrahim ‘MO’, James Kotei, Yusuph Mlipili, Laudit Mavugo na Said Ndemla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles