31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

CHANZO CHA BOMBA LA GESI KULIPUKA CHATAJWA

Na Komba Kakoa-DAR ES SALAAM


CHANZO cha kulipuka kwa moto katika bomba la kusambaza gesi eneo la Buguruni kwa Mnyamani, kimetajwa huku ikielezwa kuwa kilisababishwa na wakandarasi wanaoweka bomba la maji la Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco).

Taarifa iliyotolewa jana baada ya tukio hilo na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kapuulya Musomba, ilisema pamoja na hali hiyo walifanikiwa kudhibiti moto huo.

“Kulitokea moto maeneo ya Buguruni uliosababishwa na bomba la kusambaza gesi viwandani kutobolewa na Excavator, naambiwa ni ya wakandarasi wa uwekaji wa bomba la maji la Dawasco.

“Hata hivyo, hali imetulia na kwa muda huu watumia gesi viwandani wanaanza kurudishiwa na sehemu iliyotobolewa itaangaliwa vizuri ili kukarabatiwa,” alisema Musomba katika taarifa yake na kutoa pole kwa waathirika wa tukio hilo.

 

USHUHUDA

Akizungumza na MTANZANIA iliyofika katika eneo hilo jana na kuzungumza na mashuhuda wa tukio hilo, Athuman Ramadhan, alisema kuwa waliwaona mafundi hao wakichimba mtaro na kuwaambia wanatakiwa kuchukua tahadhari kwani eneo hilo limepita bomba la gesi.

Alisema hata walipowaambia, lakini bado mafundi hao waliendelea na kazi hiyo ndipo walipojikuta wakikwama baada ya kutoboa bomba hilo la gesi na moto kuanza kulipuka.

 

WAATHIRIKA WAIBIWA

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Faru, Simba Said, alisema tatizo hilo limechangiwa na dereva wa tingatinga kukosa mawasiliano mazuri na wananchi ambao walimpa tahadhari kabla.

“Licha ya kutokuwa na mawasiliano mazuri, lakini pia hao mafundi wanaonekana ni jeuri, kwani eneo hilo kuna alama zinazotahadharisha, lakini walijifanya wataalamu hatimaye wakatoboa bomba la gesi na kusababisha athari kubwa,” alisema Said.

Aidha alisema kuwa amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya vijana kuingia kwenye baadhi ya nyumba katika eneo hilo na kuanza kuiba mali za waaathirika wa moto huo.

“Inasikitisha kuona baadhi ya wenzetu wakifurahia mateso ya wenzao na kuamua kuwaibia, jambo hili halivumiliki, tutawatafuta na kuwakamata, naomba Jeshi la Polisi watusaidie pindi tutakapohitaji msaada wao,” alisema mwenyekiti huyo.

 

WAATHIRIKA

Mmoja wa waathirika, Hassan Simba, ambaye nyumba yake imeteketea kwa moto, alisema hana la kufanya kwa sasa kwani hakuna kitu chochote alichookoa ndani ya nyumba yake.

“Sijui nifanyeje kwani baada ya kupokea taarifa na kufika nyumbani, sikuweza kuokoa kitu hata kimoja, nilikuta wapangaji na familia yangu wakilia wasijue kitu cha kufanya,” alisema Simba.

 

VIONGOZI WANENA

Diwani wa Vingunguti, Omary Kumbilamoto (CUF),  alisema kuwa kilichotokea kwenye eneo hilo ni uzembe wa mamlaka kutowasiliana kwani wahusika walitakiwa kukaa kabla ya kuanza kwa ujenzi huo.

Kumbilamoto ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, alisema kuwa amesikitishwa na tukio hilo huku akitaka hatua zichukuliwe kwa waliolisababisha.

Kutokana na tukio hilo, Mbunge wa Segerea, Bonnah Kaluwa (CCM), alifika katika eneo hilo na kutoa pole kwa waathirika na alisema kwa sasa wataalamu wanaendelea kufanya tathimini.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, alifika katika eneo hilo na kusema kuwa familia moja yenye watu 13, itakuwa chini ya uangalizi wa Manispaa ya Ilala wakisubiri tathmini inayofanywa na wataalamu.

 

MAJERUHI WATATU

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Kituo cha afya Buguruni, Dk. Isack Makundi, alisema alipokea mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo ambaye ni mtoto.

“Juzi tulipokea majeruhi mmoja ambaye ni mtoto, akiwa ameungua zaidi kichwani. Hata hivyo baada ya huduma tulimhamishia Hospitali ya Amana na leo (jana) asubuhi tumepokea majeruhi wengine wawili, mwanamke na mwanaume wakiwa wameungua mikononi na mgongoni ila kwa sasa wanaendelea vizuri,” alisema Dk. Makundi.

 

MTOTO APOTEA

Katika ajali hiyo, ilielezwa kuwa mtoto Shukuru Yahaya (14), amepotea na hajulikani alipo.

Akieleza tukio hilo, kaka wa mtoto huyo, Selemani Yahaya, alisema mdogo wake hawakumwona tangu moto ulipolipuka katika eneo hilo.

Alisema baada ya tukio hilo mdogo wake alikurupuka mithili ya mtu aliyerukwa na akili na kuanza kukimbia ovyo na hadi jana jioni bado alikuwa hajapatikana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles