24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa aiteka Mwanza

LOWASSA Elias Msuya na Fredrick Katulanda
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amepata mapokezi makubwa jijini Mwanza alikokwenda kutafuta udhamini kwa ajili ya kuomba kuwa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo jumla ya wanachama 2,927 wamejitokeza kumdhamini.
Lowassa aliyewasili katika uwanja wa ndege wa Mwanza saa tano asubuhi, alipokelewa kwa maandamano ya pikipiki, magari na watu watembeao kwa miguu kuelekea ukumbi wa mikutano wa Mahatma Gandhi uliopo Nyamagana.
Mapokezi hayo ni wazi yanaweza kutuma ujumbe hasi kwa baadhi ya wapinzani wake hususani makada wengine wa chama hicho wanaowania urais ambao wamekuwa wakiitumia na hata kuona kuwa Kanda hiyo ya Ziwa ni ngome yao ya kisiasa.
Akizungumza katika mikutano wilaya ya Ilemela na Nyamagana ambayo ilifurika watu hadi nje ya ukumbi, Lowassa alisema uchaguzi wa mwaka huu ni mgumu kwa kuwa umekuja wakati nchi imegundua rasilimali ya gesi inayonyemelewa na makampuni makubwa ya kimataifa.
Lowassa aliwataka wananchi kuwa makini ili mataifa tajiri yasiwachagulie Watanzania rais.
“Uchaguzi wa mwaka ni wa kipekee, mkubwa na wa muhimu sana katika nchi yetu. Nawaomba Watanzania watafakari sana maneno hayo. Kwamba nchi yetu imepata gesi asilia nyingi sana. Tutakuwa katika mataifa makubwa yenye gesi.
“Gesi ni kama mafuta, ni mtaji mkubwa sana kwa Taifa letu. Lakini gesi hiyo inaweza kuifanya nchi kuwa tajiri au masikini,” alisema Lowassa.
Alisema gesi hiyo ina washindani wakubwa aliowaita ‘multinationals’, akisema ni matajiri wakubwa wenye kucha ndefu zenye nguvu.
“Wakubwa hao kwa mafuta waliogundua na gesi nyingi watataka kuja na kuzoa utajiri huo na kuusomba kwa njia za kitaalamu za kisasa.
“Ni wakati mgumu katika nchi yetu, tumepata kitu cha baraka ama laana. Kwa hiyo uchaguzi utakuwa mgumu kwa sababu hao wakubwa siwataji majina watataka kumchagua mtu au chama watakayeweza kumshika pua wampeleke pembeni,” alisema.
Huku akiwasifu marais waliopita tangu Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Rais Jakaya Kikwete, alisema wameshinda vita dhidi ya makampuni yanayonyemelea rasilimali za Tanzania na kwamba kwa sasa CCM inakabiliwa na mtihani mkubwa.
“Sasa chama chetu kinapimwa kama kitaweza kushinda uchaguzi, ili watu hawa wasiingize watu wao kwa mbinu, mtakuja kutahamaki chama chenu kinashindwa. Hii itatokea msipojipanga,” alionya Lowassa.
Aliwaomba wanachama hao kukijenga chama kwa msimamo wa pamoja ili kukabili vita dhidi ya mataifa tajiri (multinationals) ya kuchukua rasilimali za nchi kwa kuchagua kiongozi atakayesimamia na kulinda rasilimali za Taifa.
“Wito wangu kwa wana CCM tuungane sasa kuliko wakati wowote. Uchaguzi uliopita Mwanza hapa mlipoteza viti vitatu, mkapoteza watu kama kina Lawrence (Masha), watu makini na wenye uwezo. Watu watakaokiongoza chama chetu kupata ushindi, kiendelee kuwa chama cha wanyonge,” alisema.
Aliwatahadharisha pia wana CCM hao kuchagua mtu atakayeweza pia kuwa Mwenyekiti imara wa chama badala ya kuchagua watu wasiokijua chama.
“Nasema uchaguzi huu ni mtihani mkubwa kwa CCM. Ina uwezo wa kushinda mtihani huu tukiwa na umoja na mshikamano. Tunao? Tukiwa na watu watakaosimamia maslahi ya Taifa kweli kweli. Nitakapokuja kuomba kura nitawaambia mnichague mimi…” alisema.
Huku akiwataka wanachama hao kupuuza maneno ya kashfa dhidi yake, aliwataka kujiandikisha kwa wingi ili waweze kupata ushindi.
“Nilikwenda Moshi kwenye msiba, yule padre aliponiona alisema nimemwona Lowassa hapa. Sasa nawaambieni watu wote kura yangu nitampa Lowassa… (sisi Wachaga) tulijaribu kumpeleka Mrema kwa kusukuma gari lake. Akasema siri ya kumwingiza mtu Ikulu ni kura. Siri ni nini?
“Mapenzi yenu yote mliyonionyesha, mapokezi yote, kama hamkujiandikisha mmeliwa. Kahakikishe mke wako anajiandikisha, mme wako anajiandikisha, mtoto wako hata mshkaji peleka akajiandikishe,” alisema huku akishangiliwa na wanachama hao.
Sijawahi kupata mapokezi mazuri na makubwa kama haya. Mnanipa matumaini kuwa nitakapokuja mtanipa kura.
Awali akizungumza kumkaribisha Lowassa kupokea udhamini wa wanachama wa CCM, Dk. Raphael Chegeni, alitumia msemo wa Kisukuma kuwa ‘Ng’ombe anayetangulia mtoni ndiye anayekunywa maji meupe, masafi na wanaokuja nyuma hukuta yameshavurugwa na kuchafuka’.
Katika shughuli hiyo, Lowassa aliambatana na Khamis Mgeja ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mwenyekiti mstaafu wa Mkoa wa Dodoma, Pancras Ndejembi na Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai.
Wengine ni Mwakilishi wa wazee wa Mkoa wa Mwanza, Masalu Ngofilo, Mbunge wa zamani wa Nyamagana, Lawrence Masha pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles