24 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

Matajiri wapigwa stop urais CCM

Mohamme+Seif+KhatibELIZABETH MJATTA (DAR) NA DEBORA SANJA (DODOMA)

SIKU chache baada ya Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEO,s RoundTable) kutoa matangazo ya kufanya mdahalo na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliochukua fomu ya kuwania urais, ili kuwapima kupitia mjadala huo ambao pamoja na mambo mengine ungejadili maslahi mapana yanayohusu uchumi, chama hicho kimepiga marufuku wanachama wake hao kujihusisha katika midahalo yoyote ile.
Kabla ya kupigwa marufuku, matangazo yaliyokuwa yakitolewa na matajiri hao yalitoa taswira ya wao kutaka kutafuta nafasi ili waweze kufanya uamuzi wao katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Akizungumzia hilo jana mjini Dodoma, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, Idara ya Oganaizesheni, Dk. Mohammed Seif Khatib, alisema hakuna mgombea wa CCM anayeruhusiwa kushiriki katika midahalo hiyo hadi hapo chama kitakapompata mgombea mmoja wa nafasi hiyo ya urais.
“Tumesikia huko nje watu wanaanzisha meza duara au midahalo kwa wagombea wa urais, kwa wagombea wetu sisi bado hawaruhusiwi kushiriki midahalo hiyo kwa kuwa bado hatujampata mgombea.
“Tukiruhusu washiriki midahalo hii, baadhi wataanza kupakana matope, hata hivyo muda hautoshi, wanatakiwa waende kutafuta wadhamini na Mkutano Mkuu upo karibu unafanyika Julai 12, mwaka huu,” alisema.
Awali kabla ya kupigwa marufuku, mwelekeo wa matajiri hao kuwaita wagombea urais waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi, ilikuwa ni kuona yule ambaye anaweza kubeba maslahi mapana kuhusu masuala yanayohusu uchumi.
Mdahalo huo ulikuwa uanze keshokutwa katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro, ambapo wagombea urais wangeeleza sera na vipaumbele vyao, pia pamoja na mambo mengine, vingegusa kipengele cha uchumi.
Awali akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Umoja huo, Ali Mfuruki, alisema miaka yote wagombea urais wamekuwa wakishirikishwa katika midahalo inayojadili masuala ya kisiasa na kuacha suala kubwa la uchumi wa nchi.
“Miaka mingi tunaona wagombea urais wanaalikwa katika midahalo lakini mjadala unakuwa unalenga masuala ya kisiasa, mtu, rangi, lakini uchumi unaachwa pembeni.
Alisema katika mdahalo huo wagombea wangepata nafasi ya kueleza mikakati yao katika mambo muhimu. “Ni fursa ya mgombea kueleza mikakati yake ya kuifikisha nchi katika uchumi wa muda mrefu na siyo wa mwaka mmoja au miwili,” alisema na kuongeza kuwa mdahalo huo usingeangalia rangi ya mgombea au umaarufu wake.
Dhana hii ya matajiri kutaka kuona suala la uchumi linapata nafasi kwenye uchaguzi wa mwaka huu, inapewa nguvu na mfumo wa uchumi ambao nchi inaufuata kwa sasa.
Licha ya kwamba kikatiba Tanzania inafuata mfumo wa ujamaa, lakini kiuhalisia inafuata ubepari ambapo kwa sasa uchumi kwa kiasi kikubwa unaendeshwa na sekta binafsi, huku Serikali ikitegemea kodi huko.
Baadhi ya wachambuzi wanasema nchi nyingi duniani hivi sasa zina mfumo wa uchumi ambao ni mchanganyiko (mixed economy) ambapo hakuna upebari ulioiva wala usoshalisti ulioiva.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles