LIVERPOOL, ENGLAND
MICHUANO ya Ligi Kuu nchini England inatarajia kuendelea wikiendi hii kwenye viwanja mbalimbali huku mchezo ambao unatarajiwa kuteka hisia za watu wengi wa soka ni kati ya Liverpool ambao watakuwa nyumbani na kuwakaribisha Arsenal.
Huu utakuwa mchezo wa tatu kwa kila timu tangu kufunguliwa kwa msimu mpya wa ligi na timu zote zimefanikiwa kushinda michezo yao miwili lakini Liverpool imekuwa vinara kutokana na idadi ya mabao waliyoyafunga, lakini wote wana pointi sita.
Historia inawabeba Liverpool, lakini soka ni mchezo wa makosa chochote kinaweza kutokea na inategemea timu ipi itakuwa bora katika mchezo huo na itaweza kutumia nafasi bila ya kujali kuwa ugenini au nyumbani.
Huu utakuwa mchezo wa 193 kwa timu hizi kukutana katika historia ya soka kwenye michuano mbalimbali, kati ya hizo Liverpool wamekuwa wababe wakishinda jumla mara 71, wakati huo Arsenal ikishinda mara 68 na kutoa sare mata 53.
Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana ilikuwa Desemba mwaka jana ambapo Liverpool ilikuwa kwenye uwanja wa nyumabani na kufanikiwa na kufanikiwa kuipa Arsenal kichapo cha mabao 5-1, leo wataweza kuendeleza na ubabe huo au Arsenal watalipa kisasi? Muda ukifika kila kitu kitajulikana.
Michezo mingine ambayo itapigwa leo ni pamoja na Manchester United ambao watakuwa nyumbani leo kupambana na Crystal Palace. Huu utakuwa mchezo wa kulipiza kisasi hasa kwa Crystal Palace ambao mara ya mwisho timu hizi kukutana ilikuwa Februari mwaka huu huku Crystal Palace wakiwa nyumbani na kukubali kichapo cha mabao 3-1.
Hata hivyo, katika historia timu hizo zimekutana jumla mara 38 kabla ya mchezo wa leo na Manchester United wamefanikiwa kushinda mara 19, wakati huo Crystal Palace wakishinda mara 11 na kutoka sare mara nane.
Michezo mingine ambayo itapigwa leo ni pamoja na Watford ambao watakuwa nyumbani kupambana na West Ham, wakati huo Leicester City wakiwa ugenini kupambana na Sheffield United, Brighton wakicheza dhidi ya Southampton wakati huo Chelsea wakiwa ugenini wakicheza dhidi ya Norwich City.