30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU: NILINUSURIKA RISASI YA FUVU LA KICHWA

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, akimjulia hali Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu jana. Kushoto ni mke wa mbunge huyo, Alice Lissu.

MWANDISHI WETU NA MASHIRIKA


KWA mara ya kwanza, Tundu Lissu amezungumzia shambulio la kinyama alilofanyiwa na watu wasiojulikana kwa kueleza kuwa, alinusurika kufumuliwa fuvu la kichwa kwa risasi.

Lissu, Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), aliyasema hayo jana, jijini Nairobi anakotibiwa wakati akihojiwa na Jarida la Financial Times  la Uingereza.

Yakiwa ni mahojiano yake ya kwanza tangu aliposhambuliwa nje ya makazi yake yaliyoko Area D, mjini Dodoma Septemba mwaka huu, Lissu mmoja wa wakosoaji wakubwa wa serikali alisema anaamini alikuwa mlengwa wa jaribio la mauaji.

Akizungumzia shambulio hilo dhidi yake, alisema sekunde chache baada ya watu wawili wenye silaha kushuka katika gari lililokuwa likimfuatilia kwa wiki tatu, derava wake alimsukuma chini ya sakafu ya gari lake wakati wakihangaika kukwepa risasi nyingi zilizoelekezwa kwenye gari lake, nyingi zilimpiga mgongoni na nyingine kwenye bega lakini risasi moja ilikosakosa kufumua fuvu lake la kichwa.

“Hali ikawa mbaya sana kwa sababu sikuweza kuhesabu risasi, naambiwa kwamba risasi 38 zilipiga gari langu na 16 zilinipata na moja iliyokuwa imelengwa kunifumua fuvu la kichwa ilinipiga begeni karibu na shingo,” alikaririwa Lissu.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu wa kambi ya upinzani alikakririwa akieleza zaidi kuwa kilichotokea ni ushahidi wa kile ambacho amekuwa akikizungumzia mara nyingi kuhusu uwepo wa watu waovu wanaotekeleza kampeni ovu ya kuipeleka nchi pabaya.

Wakati Lissu akikutwa na mkasa huo mbaya, historia yake ya kisiasa inaonyesha kuwa amekwishtakiwa mara sita, mwaka huu kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya uchochezi.

Wachambuzi na wafuatiliaji wa mambo wamekuwa wakieleza kuwa shambulio hilo linaweza kuwa moja ya mikakati ya magenge ya wapinzani wa serikali waliobanwa na dola ambao sasa wanajaribu kutumia kila aina ya mbinu kuifarakanisha jamii hususan wanasiasa.

Tayari Jeshi la Polisi limekwishaanzisha uchunguzi wa tukio hilo na Inspekta Jenerali (IGP), Simon Sirro amekwitoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi huo kuzitoa kwa makachero wa polisi.

Sambamba na hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas naye alikutana na waandishi wa habari kuzungumzia tukio hilo ambapo alitoa rai kuwa shambulio hilo lisichukuliwe kisiasa kwa sababu ni uhalifu wenye sura za ile ile ya matukio ya kihalifu ambayo yamekuwa yakitokea nchini.

Katika mkutano wake na wanahabari alioufanya siku chache baada ya Lissu kushambuliwa, Dk. Abbas alionya kuhusu upotoshaji uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watu waliokuwa wakijaribu kuipata matope serikali kwa kuihusisha na shambulio na aliwataka wote wenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi, akiwemo Lissu kutoa ushirikiano kwa polisi.

SAMIA

Wakati huo huo, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan jana alimtembelea na kumjulia hali Lissu katika Hospitali ya Nairobi alikolazwa kwa matibabu.

Msafara wa Makamu wa Rais Samia, ulifika katika Hospitali ya Nairobi majira ya saa 11:43 jioni. Katika msafara huo walikuwemo pia Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. Pindi Chana na maofisa wengine wa ubalozi wa Tanzania nchini humo.

Akiwa hospitalini hapo, Makamu wa Rais  alimuombea Lissu apone haraka na kurejea katika hali yake ya kawaida.

“Get well quickly…recover na salamu zako zitazifikisha,” alisema Makamu wa Rais Suluhu.

Awali kabla Makamu Rais hajamtakia afya njema Lissu, yeye mwenyewe (Lissu) alimpa salamu za Rais Dk. John Magufuli.

“Msalimia Rais (Dk. John Magufuli), mwambie nashukuru. Mungu akubariki na mrudi salama nyumbani,” alisema Lissu katika salamu alizomtumia Rais Dk. Magufuli kupitia kwa Makamu wake, Suluhu.

Lissu amelazwa katika Hospitali ya Nairobi akitibiwa majeraha ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, aliyoyapa Septemba 7, mwaka huu  nje ya nyumba yake iliyoko Area D, mjini Dodoma.

Lissu alishambuliwa alipokuwa akirejea nyumbani baada ya kutoka kuhudhuria kikao cha Bunge na kutibiwa kwanza katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kusafirishwa hadi Nairobi kwa matibabu zaidi.

Makamu wa Rais, Suluhu alifika hospitalini jana kumjulia hali baada ya kuhudhuria  sherehe ya kuapishwa kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyetta.

Makamu wa Rais, Suluhu amekuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya kitaifa kumtembelea Lissu hospitali kwa ajili ya kumjulia hali na kumtakia afya njema tangu alipolazwa usiku wa Septemba 7, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles