29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

UHURU KENYATTA AANDIKA HISTORIA

Nairobi-Kenya


RAIS Uhuru Kenyatta amesema kuanzia sasa wananchi wote kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wataingia Kenya kwa kutumia vitambulisho vyao, kumiliki ardhi, kuoa, kuishi, kufanya kazi au biashara  sawa na Mkenya yeyote.

Alisema wakazi wa mataifa mengine ya Afrika watakuwa wakipokea viza za kusafiria mpakani au viwanja vya ndege nchini humo.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuapishwa kwa muhula wa pili na wa mwisho wa miaka mitano mbele ya umati wa watu wapatao 100, 000 kwenye Uwanja wa Michezo Kasarani mjini Nairobi jana,  Kenyatta alisema uamuzi huo unatokana na dhamira ya Kenya kuimarisha ushirikiano wa kanda.

“Kwa kaka na dada zangu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ninyi ni marafiki zetu wa karibu; hatima yetu na yenu imeunganishwa pamoja, matatizo na mafanikio yetu ni yenu na yenu ni yetu. “Nitafanya kazi nanyi, kaka zangu, viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuleta ari mpya na matumaini kwa taifa letu. Kwa pamoja tunaweza kuleta amani na ustawi kwa raia wetu,” alisema huku akishangiliwa na kuongeza:

“Kama ishara ya kuendelea kwa dhamira yetu kwenu, kaka na dada zetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; kuanzia sasa mtatendewa kama Wakenya. Kama kaka na dada zenu Wakenya, kitahitajika tu kitambulisho chako.

“Unaweza kufanya kazi, kufanya biashara; kumiliki mali, shamba na ukitaka kutafuta mbia, unaweza kuoa na kuishi Kenya,” alisema.

“Na dhamira hii tunaifanya bila masharti yoyote ya kubadilishana, bali imechochewa na tamaa yetu ya dhati ya ushirikiano wa  kanda. Wakati nikiwakaribisha mfahamu kuwa mtafuata  sheria na kanuni zile zile kama kaka na dada zako Wakenya,” alisema.

Kuhusu mataifa mengine ya Afrika, Kenyatta alisema raia wa bara hilo watapata visa wakati wakiingia Kenya katika vituo vya mpakani, bandarini au viwanja vya ndege  ili kuendana na msingi wa jamii katika Afrika  wa   mwingiliano huru wa watu kutoka taifa moja hadi jingine kwa kuzingatia undugu, urafiki na mshikamano wa bara hili.

“(Kuanzia leo (jana) naagiza mwafrika yeyote anayependa kutembelea Kenya atatakiwa kupata viza anapoingia Kenya. Ili kwenda sambamba na  dhamira ya Kenya, hili haitakuwa na sharti lolote la kubadilishana na taifa husika.

“Kwa kadiri tunavyotembea kwa uhuru na kuishi miongoni mwetu, ndivyo mtangamano na mtambuka wetu wa jamii utakavyofikiwa. Kugawanyika katika siasa ambako kunahatarisha usalama wetu wa pamoja, siasa chafu za utaifa vitapungua wakati undugu wetu ukiimarika kwa kukumbatia zaidi Uafrika,” alisema Rais Kenyatta

Aliahidi kuendelea kushirikiana na mataifa mengine nje ya bara hili katika maeneo mbalimbali ikiwamo kupambana na ugaidi wa kimataifa, kushirikiana katika biashara na kujenga ujirani mwema.

NASA WAONJA MKONO WA CHUMA

Sherehe hiyo ilifanyika huku usalama ukiwa umeimarishwa katika sehemu kadhaa za mji huo kutokana na  wito wa mungano wa wapinzani wa NASA  kuandaa mkutano mbadala kuomboleza wafuasi wao waliouawa wakati wa maandamano ya kupinga ushindi wa Kenyatta.

Polisi pia  walifyatua mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa Kenyatta waliotaka kuingia katika uwanja wa Kasarani baada ya uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000, kujaa kupita kiasi.

Watu wengi   waliofika uwanjani hapo walisafirishwa kwa mabasi kutoka maeneo  ambayo ni ngome ya Rais Kenyatta.

Vilevile  polisi walilinda  doria na kuuzingira Uwanja wa Jacaranda ambao   NASA walipania kuutumia kuandaa mkutano wao wa maombolezi.

Polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya baadhi ya wafuasi wa upinzani waliojaribu kukusanyika kwenye uwanja huo.

Rais Kenyatta alikula kiapo saa 6.30 mchana baada ya kuwasili na  kukagua gwaride la heshima lililoandaliwa na kikosi cha wanajeshi wa Kenya (KDF).

Jaji Mkuu, David Maraga ndiye aliyemuapisha Rais   na Naibu wake, William Ruto, shughuli ambayo ilishuhudiwa na Msajili wa Mahakama, Anne Amadi.

Awali   Amadi alisema Rais na Naibu wake wanapaswa kuapishwa kabla ya saa 8.00 mchana ili kuepusha mtafaruku wa Katiba.

“Rais na Naibu wake wanapaswa kuapishwa kati ya saa 4.00 asubuhi na saa 8.00 mchana, kwa hiyo bado tuko ndani  ya wakati huo,” alisema Amadi   dakika chache kabla ya Jaji Mkuu kuwataja kwa majina Rais   Kenyatta na Naibu wake  Ruto kuwa walichaguliwa katika uchaguzi halali.

“Nimemtangaza  rasmi Rais Uhuru Muigai Kenyatta kama Rais wa Jamhuri ya Kenya, ninamuomba Msajili Mkuu wa Mahakama  Anne Amadi amlishe kiapo,” alisema Maraga.

Ruto pia alipitia utaratibu huo huo wa kula kiapo cha kuliongoza taifa katika wadhifa   wa Naibu Rais.

ATUMIA BIBLIA YA BABA YAKE

Rais Kenyatta aliapa kwa kutumia Biblia aliyotumia baba yake, mwasisi wa Kenya,  Mzee Jomo Kenyatta, mwaka 1964 wakati nchi ilipopata  uhuru.

Naye Ruto alitumia Biblia aliyotumia Mzee Kenyatta kuapa kuwa Waziri Mkuu wakati wa serikali ya mkoloni mwaka 1963.

Vilevile meza iliyotumiwa kutia saini wawili hao   ni aliyotumia  Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki wakati akiidhinisha Katiba Mpya mwaka 2010.

VIONGOZI MASHUHURI

Zaidi ya marais 10 kutoka nchi mbalimbali Afrika walishuhudia kuapishwa kwao wakiwamo  viongozi mashuhuri kutoka mataifa kadhaa duniani.

Marais hao ni Yoweri Museveni wa Uganda, Ismail Omar wa Djibouti, Ian Khama wa Botswana, Ali Bongo wa Gabon, Paul Kagame wa Rwanda, Mohammed Abdullahi wa Somali, Edward Lungu wa Zambia, Salva Kiir wa Sudan Kusini, Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn Boshe na Rais (Mstaafu) wa Afrika Kusini ,Thabo Mbeki.

Makamu Rais waliohudhuria ni Samia Suluhu wa Tanzania na Yemi Osinbajo wa Nigeria.

Kiongozi wa upinzani nchini kutoka Chadema, Edward Lowassa pia alihudhuria hafla hiyo.

Lowassa ni rafiki wa karibu wa Rais Kenyatta na Naibu wake Ruto na aliwapigia debe kwenye kampeni ya kuchaguliwa kwao.

Licha ya hafla hiyo kuwa na mvuto mkubwa, baadhi ya viongozi wakuu ambao hawakushiriki kama ilivyopangwa na waliokuwa wakisubiriwa kwa hamu ni pamoja na Rais Dk. John Magufuli   na Waziri Mkuu wa Israel,i Benjamin Netanyahu.

Awali, ripoti zilisema Netanyahu angefika kama viongozi wengine ila   kutokana na wingi wa watu,  Netanyahu hakufika Kasarani ingawa alitegemewa kuwapo Ikulu   Nairobi.

KENYATTA: NITAKUWA RAIS WA WOTE

Katika hotuba yake, ambayo ilizungumzia masuala kuanzia ya ndani ya Kenya hadi Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla,  Rais Kenyatta aliwaahidi Wakenya kuwa rais wa wote bila kujali kama walimchagua au la.

Pia aliahidi kuheshimu Katiba kuliongoza taifa hilo mbele, akitilia mkazo umuhimu wa amani na kuleta jamii zote pamoja.

“Tumeapa kuheshimu matabaka yetu, dini, mila na Katiba kwa jumla. Lazima tuishi kwa amani kama tuliyoapa kuhakikisha inadumu nchini,” alisema Kenyatta.

Alimtaka kila Mkenya kuheshimu Katiba na endapo ana malalamiko yoyote atumie mkondo wa sheria kueleza ila si kwa kuvuruga amani ya nchi.

Rais pia aliwashauri watumishi wa umma kufanya kazi kwa mujibu wa katiba.

“Lazima kila mtu afanye kazi yake kulingana na katiba, kwa kufanya hivyo tutaweza kufikia ndoto na sera zetu kwa wananchi,” alisema

Pamoja na hali hiyo alionya kuwa hataruhusu yeyote kuvuruga amani.

“Hakuna atakayeruhusiwa kuharibu taifa hili lenye zaidi ya wananchi milioni 45. Tuishi kama ndugu na dada, jirani yako umheshimu na muishi kwa amani,” alisema akiwalenga wapinzani ambao wameapa kutotambua urais wake.

Rais Kenyatta alisema tayari ameanza kuwanyooshea mkono wa amani viongozi wa upinzani katika juhudi za kuunganisha Wakenya.

“Ninajitolea kuwa mlinzi wa wale walionichagua na wale ambao hawakunichagua. Nitakuwa rais wa Wakenya wote,” alisema Rais Kenyatta.

TOFAUTI ZA SIASA

Aliwaalika viongozi wotekusahau tofauti za siasa na kuungana naye kujenga nchi.

“Nitatumia muda wangu mwingi na nguvu kujenga madaraja ya kuunganisha Wakenya ili wapate ustawi,” alisema Rais Kenyatta.

Akionekana kupuuza wito wa upinzani wa kutotambua serikali yake, Rais Kenyatta alisisitiza kuwa kipindi cha uchaguzi kimekwisha.

“Leo ni siku ya 123 tangu Agosti 8. Hafla hii inadhirisha  mwisho wa kipindi cha uchaguzi na ninasisitiza ni mwisho wa uchaguzi,” alisema Rais Kenyatta.

Kenyatta  alionekana kufunga milango ya mazungumzo yoyote ya kubadilisha Katiba kwa kusema Kenya ina katiba endelevu duniani.

“Kenya ni nchi iliyoungana inayoongozwa na Katiba. Hakuna mianya. Kila mtu afanye kazi yake kulingana na katiba.

“Tumedhihirisha Katiba yetu siyo kipande cha karatasi. Changamoto kuu ni tishio kwa usalama na utawala wa sheria,” alisema.

Alisema yeye mwenyewe aliheshimu mahakama kwa kukubali kuhudhuria vikao aliposhtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC), na Mahakama Kuu ilipobatilisha ushindi wake, na kila mtu anatakiwa  kuheshimu sheria.

Aliahidi kwamba katika kipindi cha miaka mitano ijayo, serikali yake pamoja na mambo mengine, itaimarisha huduma za afya na kubuni nafasi za kazi.

“Kufikia 2022, idadi ya Wakenya watakaofaidika na Bima Taifa ya Afya (NHIF) watakuwa milioni 13.1,” alisema. Kwa wakati huu  ni Wakenya 6.5 wanaonufaika na bima hiyo.

Rais alisema serikali yake itafufua sekta ya viwanda ili Wakenya wengi wapate ajira  na kupunguza gharama ya umeme ili kukuza uchumi.

Aliahidi kwamba serikali yake itahakikisha Wakenya 500,000 wanapata makazi bora kwa kupunguza gharama za ujenzi.

ALIA NA MAHAKAMA

Ingawa alisema Katiba ya Kenya inatambua uhuru wa Mahakama, Rais Kenyatta aliilaumu idara hiyo kwa kuiwekea serikali yake vizingiti katika kutekeleza ajenda yake ya maendeleo.

Alisema mahakama imekuwa ikihujumu utendaji kazi wa serikali.

“Tutashauriana na mahakama kwa sababu imekuwa ikihujumu shughuli za serikali,” alisema Rais Kenyatta. Alionya kuwa maofisa wazembe katika utumishi wa umma   hawatavumiliwa.

Aliagiza Bunge   kuweka sheria zitakazohakikisha serikali za majimbo zinatumia vema fedha za umma.

Rais Kenyatta alisema serikali ya Jubilee haina budi kutimiza ahadi zake kwa Wakenya kwa sababu waliipigia kura kwa wingi.

RAILA NAYE ASUBIRI KUAPISHWA

Kiongozi wa upinzani   Raila Odinga alisema muungano wake wa NASA utatumia kifungu cha Kwanza cha Katiba kumuapisha ili aingie Ikulu.

Akiwahutubia wafuasi wake katika barabara ya Manyanja muda mfupi baada ya kuapishwa kwa Rais Kenyatta, Odinga alidai alishinda uchaguzi wa Agosti 8 hivyo ataapa kwa kutumia nguvu ya raia kuingia Ikulu.

“Tulisema wakiapisha, nasi tunaapisha. Katika uchaguzi wa Agosti 8 nilipata kura milioni 8.5 naye Uhuru akapata kura milioni 7.1 . Sisi hatutambui ushindi wake katika kura ya marudio iliyofanyika Oktoba 26,”alisema.

Odinga alisema upinzani utafuata utaratibu unaofaa katika kuapishwa kwake kabla ya kuingia Ikulu.

“Nitaapishwa kama (Emmerson) Mnangagwa huko Zimbabwe…tutatumia kipengele cha kwanza cha katiba kinachowapa raia mamlaka ya juu.

“Mimi si mwoga, sitaapishwa kienyeji kama Besigye wa Uganda,”alisema Odinga kabla ya polisi kutibua mkutano wake kwa kutumia mabomu ya machozi na virungu.

Viongozi wa NASA walilazimika kukatiza mkutano huo baada ya kuvamiwa na polisi muda mfupi baada ya Odinga kumpa Kiongozi  mwenza wa NASA, Musalia Mudavadi nafasi ya kuhutubia wafuasi hao.

Mapema jana akihojiwa na kipindi cha Newsday cha   Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Odinga alisema kamwe muungano wake hautamtambua Uhuru Kenyatta kama rais halali wa Kenya kwa kuwa alichaguliwa na asilimia ndogo ya Wakenya.

Kwa mujibu wa Raila, hafla ya kumuapisha   Kenyatta iliyofanyika jana katika uwanja wa Kasarani ilikuwa sherehe ya kumpamba ambayo ni kinyume cha sheria.

“Kenyatta ni rais bandia kwa kuwa aliwatishia majaji wa Mahakama Kuu  kwa manufaa yake binafsi. Hivyo uamuzi wa mahakama hiyo ulikiuka haki,” alisema kiongozi huyo wa Chama cha ODM.

Hata hivyo Odinga alikaririwa akisema  yuko tayari kuzungumza na Rais Kenyatta wakati wowote iwapo nafasi hiyo itatokea ili kuleta mageuzi ya uchaguzi wa haki na kumaliza mgogoro wa siasa baina ya wawili hao lakini si kujiunga na Serikali ya Kenyatta.

“Mimi nimekuwa tayari kusuluhisha jambo hili lakini Kenyatta amekuwa akijishughulisha na hafla ya kupambwa na kusema mazungumzo atafanya baada ya kuapishwa,” alisema.

POLISI WAPIGA WAFUASI WA NASA

Watu kadhaa walijeruhiwa vibaya katika makabiliano hayo kati ya polisi na wafuasi wa upinzani.

Awali mkutano wa maombi ambao ulitarajiwa kuhutubiwa na viongozi wakuu wa NASA katika uwanja wa Jacaranda, Nairobi kabla ya kutibuliwa na polisi kwa mabomu ya machozi na risasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles