27 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU ATAJA WANASHERIA WALIOPATA MISUKOSUKO KAZINI

Na ESTHER MBUSSI

-DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kimemwandikia barua Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, kumwelezea sababu za mgomo wao na jinsi wanasheria wanavyonyanyaswa na kuuawa.

Mgomo huo wa siku mbili unatokana na shambulio la mabomu katika Ofisi ya Mawakili ya IMMMA.

Barua hiyo ya TLS iliyotiwa saini na Rais Tundu Lissu, imesema mgomo wao wa siku mbili haumaanishi kupingana na Serikali au kuwaadhibu wateja ila kuhamasisha umma kuhusu mazingira ya hatari waliyopo wanasheria nchini.

Lissu alisema tukio hilo halikufanyika kwa bahati mbaya na matukio kama hayo ya kuwasumbua wanasheria wasifanye kazi zao ipasavyo, imekuwa sehemu ya maisha yao.

“Kwa mfano, Aprili 7, mwaka jana ofisi za Mwanasheria Said Omar Shaaban ambaye kwa sasa ni Rais wa Chama Wanasheria wa Zanzibar (ZLS), zilipigwa bomu na kuharibiwa, lakini hadi leo hakuna ripoti ya uchunguzi wa polisi.

“Wanasheria pia wamefungwa  kizuizini na wengine kukamatwa wakiwa mahakamani wakitekeleza majukumu yao ya kitaaluma na wengine wameuawa kikatili.

“Kwa mfano miaka michache iliyopita, wanasheria Profesa Jwani Mwaikusa na Dk. Sengondo Mvungi, waliuawa baada ya kuvamiwa na kupigwa na watu wasiojulikana.

“Machi mwaka juzi Wakili Philbert Gwagilo, alipotea katika mazingira ya kutatanisha na hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusu kupotea kwake,” alisema Lissu katika barua hiyo.

Akizungumzia kuhusu wanasheria ambao hawatagoma, alisema wanaotaka kwenda mahakamani waende kama wanaona wenzao kulipuliwa kwa mabomu ni sawa, ila wakae wakijua hawako salama.

“Tunataka tuhakikishiwe usalama wetu, siku mbili hizi tunataka wananchi nao wapaze sauti kuomba usalama wa wanasheria, au wanataka tufe wangapi ili wajue tunahitaji ulinzi?” alihoji Lissu.

LHRC WALAANI

Wakati huo huo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na TLS, wamelaani kulipuliwa mabomu kwa Ofisi ya Mawakili ya IMMMA kwa mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali wa kisheria.

Wakiwa na mabango nje ya Ofisi ya LHRC, ambako pia katika hali isiyokuwa ya kawaida mkutano na waandishi wa habari ulifanyika nje, wanasheria hao walikuwa wamevalia nguo nyeusi na vitambaa vyeusi usoni kama ishara ya mgomo na kupinga kitendo cha kushambuliwa kwa ofisi za IMMMA.

Baadhi ya mabango yaliandikwa ‘Hakuna aliye juu ya sheria’, ‘Mabomu Tanzania tunaelekea wapi’, ‘Utawala wa sheria bila wanasheria haiwezekani’, ‘Leo kwa Wanasheria kesho???’, ‘Ulinzi na uhai na mali zetu ni jukumu la Serikali’, ‘Tanzania ya amani???’ na mengine mengi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa LHRC, Helen Kijo-Bisimba, alisema kituo hicho kinalaani tukio hilo na kinasikitika tangu kutokea kwa tukio hilo Serikali haijatoa tamko isipokuwa utetezi wa polisi, wakijitetea kuhusu sare walizovaa watu waliovamia na kulipua ofisi hiyo.

“Viongozi wa Serikali na vyombo vyake vyenye dhamana ya kulinda usalama wa watu nchini na haki za binadamu kwa ujumla wawajibike au kuwajibishwa mara moja pale ambapo wameshindwa kusimamia ipasavyo majukumu yao, tunasikitika hadi leo hii hatujasikia kauli ya Serikali kulaani kitendo hiki.

“Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaitaka Serikali kupitia Jeshi la Polisi kuhakikisha wahusika wa shambulio la Ofisi ya IMMMA Advocates wanakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria haraka iwezekanavyo,” alisema Bisimba.

Pamoja na mambo mengine, alisema wanaunga mkono mgomo wa siku mbili wa mawakili, lakini pia ametaka tasnia ya sheria iachwe huru katika kufanya kazi zake na kupatiwa ulinzi kwa mujibu wa sheria na wanasheria waachwe watekeleze majukumu yao bila kuingiliwa au kutishwa.

Alisema wanasheria hawako huru katika kutekeleza majukumu yao na kwamba wakati mwingine hukutana na kauli za vitisho au kukatisha tamaa.

“Julai mwaka jana, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Salum Msangi, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema wanasheria wanaotetea wahalifu wataunganishwa na wahalifu hao katika makosa waliyoyatenda ili wakateteane wenyewe huko ndani watakapokwenda.

“Hata hivyo, kauli ya Rais John Magufuli katika siku ya sheria Februari mwaka huu, pamoja na mambo mengine, alitoa kauli mbaya inayoingilia mhimili wa mahakama na kuagiza watuhumiwa wa ujangili kuchukuliwa hatua punde wanapokamatwa pasipo kujali utaratibu wa mahakama na kuwajumuisha mawakili wote watakaowatetea.

“Sambamba na hilo, Machi mwaka huu aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria alitishia kufuta Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) akisema Serikali haiwezi kuona TLS ikijiingiza katika siasa,” alisema Bisimba.

Kwa upande wake, Rais wa TLS, Lissu alisema mgomo wa siku mbili wa mawakili uko pale pale lakini kwa watakaokaidi chama hakina cha kuwafanya.

 

KAMANDA MAMBOSASA AWANYOSHEA KIDOLE WANASIASA

Wakati hayo yakiendelea Mwandishi Wetu, Patricia Kimelemeta, anaripoti kwamba Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema anashangazwa kuona baadhi ya wanasiasa kuingilia kati suala la uvamizi wa kampuni ya mawakili ya IMMMA wakati Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa mara kwanza tangu alipoteuliwa kuwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam jana, Mambosasa alisema kitendo kilichofanyika katika kampuni hiyo ni cha kitaalamu zaidi na kwamba wanahitajika wataalamu wenyewe kulizungumzia.

“Mwaka 2013, wahalifu walirusha bomu katika Kanisa Katoliki lililopo Olasiti mjini Arusha, watu waliofahamu aina ya bomu na wahusika ni wataalamu wa mabomu kutoka Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi (JWTZ), hivyo basi, masuala kama hayo yanapaswa kuachwa kwa wataalamu wanaohusika ili waweze kutimiza majukumu yao halafu watatupa taarifa,” alisema Mambosasa.

Alisema tukio hilo la ofisi za mawakili wa IMMMA limeingiwa kisiasa zaidi, jambo ambalo linaweza kusababisha kujitokeza kwa migongano.

“Tumeshangazwa na kitendo cha baadhi ya wanasiasa kuingilia kati bomu lililopigwa katika Kampuni ya Mawakili ya IMMMA wakati suala lenyewe liko kitaalamu zaidi na kwamba wanaofahamu ni aina gani ni wataalamu wa mabomu,” alisema Mambosasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles