23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 11, 2024

Contact us: [email protected]

WATOTO WANNE WATEKWA KIMAFIA

Na JANETH MUSHI – ARUSHA

WATOTO wanne akiwamo mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Lucky Vincent ya jijini Arusha, Maureen David (6), wametekwa na watu wasiojulikana.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Mtaa wa Olkereyani, Kata ya Olasiti, jijini Arusha, Daudi Safari, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mbele ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema).

Katika maelezo yake, Safari alisema watekaji hao wamekuwa wakiwasiliana na wazazi wa watoto hao wakiwataka wawapatie fedha ili wawaachie watoto wao.

Aliwataja watoto wengine waliotekwa na umri wao kwenye mabano kuwa ni Ikram Salim (3), aliyekuwa akiishi na wazazi wake Mtaa wa Burka, Kata ya Olasiti, Ayub Fred (3) na Bakari Selemani (3), ambao wote wazazi wao wanaishi Mtaa wa FFU, Kata ya Muriet jijini hapa.

Kutokana na matukio hayo, alisema idadi kubwa ya wazazi wamejaa hofu na wengine wanalazimika kuwapeleka na kuwafuata watoto wao shuleni.

“Awali tulidhani kuna suala la visasi kwa sababu watekaji hao walikuwa wakiandika ujumbe kwenye karatasi na kuupeleka nyumbani kwa wazazi wa watoto, wakisema kama wazazi hao wakitekeleza masharti yao, watawasamehe makosa yote waliyowahi kuwatendea.

“Lakini tulipowauliza wazazi, walisema hawana kumbukumbu kama wamewahi kumkosea mtu,” alisema.

MWENYEKITI ASIMULIA MATUKIO

Akizimulia matukio hayo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Olkereyani, Safari alisema: “Tukio la kwanza la Maureen lilitokea Agosti 21, mwaka huu na baada ya mtoto huyo kutoonekana nyumbani, wazazi wake walikwenda kutoa taarifa ofisi ya mtaa na kituo cha polisi.

“Baada ya kumteka, hao watekaji walituma watoto wadogo wapeleke ujumbe nyumbani kwao na mtoto huyo na wazazi waliporudi jioni, waliambiwa mtoto wao yuko na watu fulani.

“Katika karatasi ile, kulikuwa na namba yao ya simu na pia walisema wasipigiwe simu na badala yake watumiwe ujumbe wa maneno.

“Tulipoona hivyo, tulikwenda polisi na zile karatasi, tukafungua kesi ya utekaji. Alhamisi ya wiki iliyopita, wazazi walipoamka asubuhi, walikuta mlangoni nguo za mtoto zikiwa na karatasi iliyowataka watume Sh milioni 4.5,” alisema mwenyekiti huyo wa mtaa.

Akizungumzia tukio la pili, alisema lilitokea Agosti 25, mwaka huu, likimhusisha mtoto Ikram aliyetekwa saa 12 jioni na baadaye watekaji hao kuanza kuwasiliana na babu wa mtoto huyo aliyetambuliwa kwa jina la Kassim Hassan.

“Walimteka Jumamosi, tukatoa raarifa kama kawaida. Pia waliacha ujumbe wakisisitiza wako na mtoto wao na kumtaka babu na wazazi wasitoe taarifa polisi wala mahali popote. Pia walitaka mawasiliano yote yafanyike kwa ujumbe mfupi wa maneno,” alisema.

Kwa mujibu wa Safari, watekaji hao walimtaka babu wa mtoto huyo awatumie pia Sh milioni 4.5 ili wamwachie mtoto wao.

“Walipomwambia wanataka kiasi hicho cha fedha, babu alisema hawezi kupata fedha hizo ila anaweza kuwatumia shilingi laki tatu anazoweza kupata.

“Alipowaambia anazo tayari shilingi laki tatu, wakamwambia awatumie hizo kwanza na kama atashindwa kutimiza masharti, watamletea kichwa cha mjukuu wake nyumbani.

“Kwa hiyo, babu aliogopa na wiki iliyopita jioni aliwatumia fedha hizo. Alipowatumia tu, wakamwambia hawawezi kumpa mtoto huyo kwa sababu wanajua anavyoshirikiana na polisi katika suala hilo, wakati walishamzuia asifanye hivyo,” alisema.

Safari aliiomba Serikali iwasaidie kuwakamata watu hao kwa sababu hadi sasa hakuna amani.

Kwa upande wake, Mbunge Lema alilaani matukio hayo na kusema Jeshi la Polisi linapaswa kufuatilia kwa karibu suala hilo ili kukabiliana na mtandao huo wa wahalifu.

WASIMULIA WATOTO WAO WALIVYOTEKWA

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, mzazi wa Maureen aliyejitambulisha kwa jina la David Njau, alisema mtoto wake alitekwa Agosti 21 mwaka huu, alipokuwa akicheza na wenzake.

“Alipokuwa anacheza na wenzake, kwenye saa 12 jioni hivi, inasemekana alikuja kijana akamwita na alipomfuata, aliondoka naye.

“Hata tulipomtafuta, hatukumpata na baadaye tulipokea ujumbe wa simu ukitutaka tutume Sh milioni 4.5 ili tuweze kumpata mtoto wetu.

“Tena waliniambia nikitaka kuwasiliana nao, nitume ujumbe wa maneno badala ya kuwapigia simu na mara ya mwisho kuwasiliana nao ni jana (juzi) ambapo walinitumia ujumbe wa maandishi wakitaka niwatumie shilingi laki tatu.

“Hapa nilipo nimeshachanganyikiwa, naiomba Serikali itumie vyombo vyake kuwaokoa watoto wetu,” alisema Njau.

Mzazi wa Ikram, Salim Kassim, alisema mtoto wake alitekwa akiwa nje ya geti la nyumba yao akicheza mpira na watoto wenzake.

“Mtoto alikuwa anacheza na wenzake, huku mama yake akimenya viazi ndani. Alipomaliza kazi zake, alitoka nje kumtafuta mtoto ndipo alipoambiwa na wenzake kuwa alichukuliwa na baba yake mkubwa aliyekuwa amembeba.

“Baadaye usiku, tulikuta shati na mpira wa mwanangu vikiwa vimechanwa na kuandikwa ujumbe kwenye daftari uliosema kesho yake saa mbili asubuhi, tutume Sh milioni 4.5 vinginevyo watamkatakata mtoto kama walivyokata mpira wake.

“Mzee wangu aliwasiliana nao, akaomba tuwatumie shilingi laki sita ili wamwachie mtoto. Wakati tunawaambia hivyo, hata hiyo laki sita hatukuwa nayo na kuamua kuwatumia shilingi laki tatu.

“Tulipotuma fedha hizo, walitutumia ujumbe, kwamba hawana mtoto bali walikuwa na shida ya fedha. Kisha waliomba namba ya simu yenye whatsapp ambayo baadaye walitutumia picha mbili za Ikram walizompiga,” alisema mzazi huyo.

KAMANDA WA POLISI

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema taarifa za utekaji huo wanazo na kwamba watoto wawili, Bakari na Ayoub wamepatikana jana usiku wakiwa eneo la Kwamorombo.

Pia, alisema mtuhumiwa mmoja anashikiliwa kuhusiana na matukio hayo.

WIZARA HAINA TAARIFA

Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia maendeleo ya jamii, jinsia na watoto, Sihaba Nkinga, alisema wizara yake haijapata taarifa ya kuwapo kwa watoto waliotekwa.

“Hatuna taarifa, lakini ngoja tufuatilie matukio hayo kwa kushirikisha wadau mbalimbali kwa sababu lengo letu ni kuona watoto wanalindwa na wanaishi katika mazingira mazuri,” alisema Nkinga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles