Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
WAKATI Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), akitarajiwa kufanyiwa operesheni ya 15 wiki hii, taarifa mpya ambazo gazeti hili limezipata zinadai kuwa mbunge huyo tayari ameanza mazoezi ya viungo.
Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alikolazwa Lissu kwa zaidi ya siku 40 sasa, vimeliambia MTANZANIA kuwa ndani ya siku nne kuanzia sasa kuna uwezekano mbunge huyo akatoka hospitalini.
Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7 mwaka huu nyumbani kwake mjini Dodoma alikokuwa anahudhuria vikao vya Bunge.
Vyanzo hivyo vya habari vilivyozungumza na gazeti hili jana kwa sharti la kutotajwa majina vilieleza kuwa, awali taarifa za kitabibu zilionyesha kuwa Lissu angetoka hospitalini Oktoba 31 mwaka huu, lakini kutokana na hali yake kuendelea kuimarika anaweza kuruhusiwa kabla ya muda huo.
“Taarifa za kitabibu zilikuwa zinaonyesha kwamba Oktoba 31 mwaka huu, Lissu atoke hospitalini lakini recovering (namna alivyopata nafuu) yake imeonekana haraka.
“Juzi na jana (Jumamosi na Jumapili), Lissu alianza kutolewa nje akiwa kwenye wheel chair akiota jua… hivyo ndani ya siku nne kuanzia sasa atakuwa ametoka,”kilisema chanzo hicho cha habari.
Pamoja na taarifa hizo, haijajulikana endapo mwanasheria huyo mkuu wa Chadema, akitoka hospitalini ataendelea kubaki Kenya au atarudi nyumbani.
Gazeti hili lilipomtafuta Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe simu yake iliita bila kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu.
Ikumbukwe kuwa msemaji wa suala la Lissu tangu kushambuliwa kwake ni Mbowe, hivyo hakuna kiongozi mwingine wa Chadema aliyekuwa tayari kuzungumzia hali yake.
Hata hivyo tangu aliposhambuliwa zaidi ya siku 40 sasa, hakuna mshukiwa yeyote aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani, licha ya Jeshi la Polisi kuahidi mara kwa mara kufanya hivyo.
Mara kadhaa Jeshi la Polisi limekuwa likieleza kuwa linaendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo, lakini familia ya mbunge huyo pamoja na uongozi wa Chadema walieleza bayana kwamba hawana imani na uchunguzi wa vyombo vya ndani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alipata kusema kuwa kuomba uchunguzi kwa watu wa nje litakuwa ni jambo la mwisho, ambapo aliwataka wananchi kuviamini vyombo vya ndani.
Kuhusu upelelezi wa kesi ya Lissu, Mwigulu alisema ikifika muda mwafaka watasema kila kitu ingawa hadi sasa alisema wamekamata zaidi ya magari 10 yanayofanana na lililobeba watu waliomshambulia Lissu.
Tangu kuumizwa kwa Lissu wabunge mbalimbali, baadhi ya viongozi wa dini na watu mbalimbali wamekuwa wakipishana jijini Nairobi kumjulia hali.
Kwa upande wa CCM, Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ndiye pekee aliyekwenda Nairobi kumjulia hali Lissu huku wengine wakimtumia ujumbe wa kumpa pole.
Wakati anaendelea na matibabu, makundi mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania walikuwa wakihimizana kufanya maombi ya kila aina kwa ajili ya Lissu na wengine wakituma nyaraka mbalimbali za kutaka uchunguzi wa haraka kuwabaini waliomfanyia unyama huo.