Na JONAS MUSHI-DAR ES SALAAM
MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amesema katika kipindi hiki cha ukandamizaji wa demokrasia kwa wapinzani wanatakiwa kujifunza namna ya kufanya siasa za chini kwa chini na kupigania haki kwa kadri inavyowezekana.
Aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika semina ya wanafunzi wa siasa kutoka nchi 10 za Afrika ikiwamo Tanzania, ambao wanatoka vyama vya upinzani.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki alieleza namna siasa zilivyobadilika Tanzania.
Kwa tafsiri yake aliita hali hiyo kuwa ‘New Normal Politics’ akisema ni hali ambayo inaminya demokrasia kwa kukataza mikutano ya siasa.
Alisema katika hali hiyo pia wanasiasa wanawekwa ndani na uhuru wa vyombo vya habari unaminywa tofauti na mwaka mmoja uliopita.
Lissu alisema upinzani hauna budi kujifunza namna ya kufanya siasa kwa maumbo mengine tofauti na vyama vyao na kudai haki zao hata kwa kadri inavyowezekana.
“Tukinyimwa kufanya mikutano hatuwezi kurudi nyumbani na kumwomba Mungu wala hatuwezi kuunga mkono chama tawala au kukubali kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja, badala yake lazimatu jifunze kuishi tofauti na maagizo yao,” alisema Lissu.
Alisema kwa sasa chama chake kimeanza mikutano ya ndani nchi nzima kuhakikisha wanachama wanajua kinachoendelea na wanajiandaa vizuri kwa uchaguzi ujao.
Lissu alisema siasa za sasa zinaelekea kuwa kama kipindi cha kabla ya uhuru ambako hata vyombo vya habari vimebanwa kiasi cha kuogopa kuandika vitu vinavyoikosoa serikali.
Alisema badala yake sasa vyombo vya habari vinaandika serikali inavyotaka.