Na Oliver Oswald, Dar es salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana lilazimika kutumia nguvu kubwa kupambana na wafusi wa Chama cha Wananchi (CUF), waliokuwa wanaandamana katika kile kilichoelezwa kukumbuka mauaji ya wanachama wake yaliyotokea Januari 26 na 27, mwaka 2001 visiwani Zanzibar.
Katika purukushani hizo, askari walimpiga kwa kutumia kitako cha bunduki na kisha kirungu, mpigapicha wa gazeti la Jambo Leo, Hamisi Mussa, aliyekuwa anatekeleza majukumu yake ya kazi.
Maandamano hayo yaliyoongozwa na Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, yalianzia katika ofisi za chama hicho Wilaya ya Temeke ambapo kabla ya kuanza, aliwaeleza wanachama wake madhumuni ya kumbukumbu hiyo.
Baada ya hotuba ya Profesa Lipumba, wanachama na wafuasi wa chama hicho walianza maandamano hayo saa 7 mchana, ambayo hata hivyo yalikwama hatua chache kwa kudhibitiwa na askari wa Jeshi la Polisi.
Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walilazimika kuwatawanya waandamanaji hao kwa virungu na mabomu ya machozi na kuwakamata baadhi yao pamoja na viongozi wao akiwemo Profesa Lipumba.
Wanachama hao wa CUF wanadaiwa kukaidi amri ya polisi iliyowataka kusitisha maandamano kwa sababu hawakuwa na kibali.
Pamoja na kutolewa tangazo hilo la polisi, waandamanaji hao walipuuza, ndipo baada ya sekunde chache mabomu ya machozi yalianza kufyatuliwa na watu kuanza kukimbia ovyo.
Maandamano hayo yalihusisha wanachama wa chama hicho kutoka maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake, huku wengine wakitumia usafiri wa aina mbalimbali kufika eneo la Mtongani kuungana na wenzao waliokuwa wanatarajia kukusanyika kuelekea Mbagala Zakhem ambako yangehitimishwa kwa kufanyika mkutano wa hadhara ambao ulikuwa unatarajiwa kuhutubia na Profesa Lipumba.
Awali Profesa Lipumba aliwaomba polisi kumruhusu ili akawatangazie wafuasi wake zuio hilo la polisi kama njia ya kuepuka madhara ikiwamo watu kuumia.
Hata hivyo, polisi walikubalina na ombi hilo la Profesa Lipumba.
Licha ya amri hiyo, hakuna mwanachama yeyote aliyetii agizo, hivyo polisi walianza kurusha mabomu ya kutoa machozi kama mvua huku wakitembeza kichapo kikali kama njia ya kudhibiti maandamano hayo yaliyokuwa yamefika eneo la Mtoni Mtongani.
WATOTO 15 WAPOTEA
Katika purukushani hiyo, watoto 15 kati ya 45 wanaosoma katika Shule ya Awali ya Mengo iliyopo Mtoni Mtongani, hawajulikani walipo baada ya bomu kuingia ndani ya darasa walilokuwa wakisoma.
Kutokana na kupigwa kwa bomu hilo, watoto hao walianza kukimbia ovyo, huku wengine wakiishiwa nguvu hali iliyowalazimu walimu woa na wakazi wa eneo hilo kuwapa huduma ya kwanza shuleni hapo.
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu kupotea kwa watoto hao, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Sabastian Zacharia, alisema polisi haina taarifa hizo, huku akiahidi kufuatilia.
WATU 30 WAKAMATWA
Akizungumzia tukio hilo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Saimon Sirro, alisema katika kudhibiti maandamanp hayo wamefanikiwa kuwatia mbaroni wafuasi 30 wa CUF.
Mbali na Profesa Lipumba, viongozi wengine waliokamatwa ni Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho, Shaweji Mketo, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mtambani – Vingunguti, Mohamed Mtutuma.
Kamishna Sirro, alisema wamelazimika kutumia mabomu baada ya viongozi wa CUF kukaidi amri halali ya kuwataka kutofanya maandamano.
LIPUMBA NA TUME HURU
Awali akihutubia wanachama wa CUF kabla ya kukamatwa, Profesa Lipumba alisema bila uchaguzi huru na haki Oktoba, mwaka huu, taifa linaweza kurudia historia ya mauaji yaliyotokea Zanzibar mwaka 2001.
Profesa Lipumba alitumia nafasi hiyo kutaka wanachama wa CUF pamoja na Watanzania kutoshiriki katika upigaji kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa unaotarajiwa kufanyika Aprili 30.