33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mawaziri watatu kitanzini

LUKUVIsamuel sittaNa Waandishi Wetu, Dar es Salaam
BAADA ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, baadhi ya wananchi wamekuwa wakijiuliza ni nini ambacho mawaziri wapya wataweza kufanya kwa muda wa miezi tisa iliyobaki.
Pamoja na kuwa na muda mfupi, bado kuna mambo kadhaa ambayo huenda ikawa ni ‘kitanzi’ kwa mawaziri hao kabla ya nchi kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu.
Changamoto kubwa ni fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hasa baada ya nchi wahisani kugoma kutoa fedha kwa Serikali kutokana na kashfa ya uchotwaji wa fedha zaidi ya Sh bilioni 300 katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mawaziri wanaokabiliwa na changamoto kubwa ni pamoja na Samuel Sitta aliyeteuliwa kushika Wizara ya Uchukuzi, William Lukuvi (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) na George Simbachawene (Nishati na Madini).

SITTA
Sitta ambaye ana historia nzuri kwenye Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tangu miaka ya 1980, anakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ndani ya miezi tisa atakayoiongoza wizara hiyo, ni mtihani wake kwa wananchi kumpima.
Bandari
Moja ya mitihani ambayo Sitta atakabiliana nayo ni ujenzi wa gati za kisasa namba 12 na 13 kama ilivyoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete, ambao umefanya baadhi ya maofisa wa Mamlaka ya Bandari (TPA) kupanda kizimbani.
Baada ya ujenzi huo kusuasua kwa miaka mitatu, hivi sasa inaelezwa kuwa tayari zabuni ya mradi huo imeshatangazwa na wakati wowote mkandarasi atatangazwa, hivyo ni wazi kuwa utekelezaji wake utaanza chini ya uongozi wa Sitta.
Hotuba ya bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2014/15, imeeleza kuwa TPA imekamilisha majadiliano na Benki ya Dunia wakishirikiana na TradeMark East Africa (TMEA) na Idara ya Serikali ya Uingereza ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID) ili kupata fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa mradi wa kupanua na kuchimba lango la kuingilia na kutokea meli katika bandari ya Dar es Salaam.
Mradi huu utatekelezwa sambamba na uboreshaji wa gati namba 1-7. Kazi ya ujenzi inatarajiwa kuanza Desemba, 2014 na kukamilika Agosti, 2016.
Aidha kazi ya uchimbaji na upanuzi wa lango la bandari ya Dar es Salaam inatarajiwa kuanza Agosti, 2015 na kukamilika Agosti, 2016.
Katika bandari pia, kuna tatizo la uongozi ambapo hadi sasa chombo hicho hakina mkurugenzi mkuu na aliyepo anakaimu kwa takribani miaka minne sasa.

Upanuzi Uwanja Ndege wa Dar
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ni kati ya viwanja ambavyo havina sifa nzuri duniani, kuanzia ubora wake hadi mwonekano.
Mradi wa upanuzi wa uwanja huo kwa kujenga geti namba III, utakaoweza kubadili taswira yake, ni changamoto nyingine kwa waziri huyo.
Katika hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2013/2014, taarifa ya kuanza ujenzi wa jengo la tatu la abiria (Terminal III) katika uwanja huo ilitolewa.
Taarifa ya bajeti hiyo, ilisema awamu ya kwanza ya ujenzi huo ilianza Januari, 2014 na itahusisha ujenzi wa jengo lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 3.5 kwa mwaka na utaghimu Sh bilioni 293. Awamu hii inatarajiwa kukamilika Oktoba, 2015.
Reli
Sekta ya reli ambayo pia inamgusa Sitta moja kwa moja kutokana na Jimbo lake la Urambo Mashariki kupitiwa na reli ya kati, ni changamoto nyingine inayomkabili kutokana na usafiri huo kusuasua kwa miaka kadhaa sasa.
Kwa sasa watu wanaotumia reli ya kati hawana uhakika na safari za treni.
Mbali na reli hiyo, Tazara ni mzigo mwingine atakaoubeba Waziri Sitta kutokana na shirika hilo kukumbwa na migogoro na migomo kila uchwao.

Treni ya Mwakyembe
Pia treni ya Dar es Salaam, maarufu kama Treni ya Mwakyembe, ni changamoto kubwa inayomkabili kiongozi huyo.
Baadhi ya taarifa zimekuwa zikisema kila siku uendeshaji wa treni hiyo husababisha hasara ya Sh milioni 2.3, huku aliyekuwa akiongoza wizara hiyo, Dk. Harison Mwakyembe, akisema treni hiyo inaokoa takribani Sh bilioni 3 kila mwezi kutokana na kupunguza foleni na kuwaisha watu kazini.
Katika hotuba yake ya bajeti iliyopita, Dk. Mwakyembe akiwa Waziri wa Uchukuzi, alisema huduma za usafiri wa reli katika Jiji la Dar es Salaam ilisafirisha abiria 1,343,763 katika mwaka 2013 ikilinganishwa na 230,009 waliosafirishwa katika mwaka 2012.
Aidha kwa upande wa Tazara, abiria 1,460,506 walisafirishwa katika mwaka 2013 ikilinganishwa na 148,524 waliosafirishwa katika mwaka 2012.

Madeni ya ATC
Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), ni changamoto nyingine inayomkabili Sitta kwani licha ya madeni makubwa ya shirika hilo, hali yake ni dhohofu kabisa.
Serikali imesema hadi sasa inakabiliwa na deni la Sh bilioni140 lililosababishwa na uzembe pamoja na ubadhirifu katika shirika hilo.
Wakati wa uongozi wake, Dk. Mwakyembe, alisema Serikali inakusudia kulipa deni hilo ili kutoa nafasi ya kuimarisha upya sekta ya usafiri wa anga nchini, jambo ambalo halikutekelezeka.
Alisema imefikia wakati sasa Tanzania inapaswa kuwa na shirika imara la ndege ili kuepuka kurudia uzembe na ubadhirifu uliojitokeza miaka ya nyuma ATC.
Kuanguka kwa mabehewa
Julai 24, mwaka jana Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) iliagiza mabehewa 25 aina ya Ballist Hopper Bogie (BHB) kwa Sh bilioni 4 ambapo 20 kati yake yalibainika kuwa ni mabovu na baadhi ya watendaji kuyatengeneza kwa kificho.
Mkataba wa kununua mabehewa hayo ulisainiwa Machi 21, 2013 kati ya TRL na Kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries ya India.
Kwa kuwa bado utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa (BRN) sasa unaendelea, Sitta ataendelea kupambana na changamoto nyingi kama hizi za wafanyakazi wasiyo waaminifu.

Mikakati lukuki
Akizungumza wakati wa ziara yake kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana, Sitta aliwashangaa waliobeza uteuzi wake akisema wasubiri mafanikio ya kasi na viwango.
Alisema walioponda utendaji wake hawajui historia yake kwani yeye ndiye aliyetafuta fedha za ujenzi wa uwanja huo wa ndege, ujenzi wa daraja la Salender Dar es Salaam, na kwamba yeye ndiye aliyeleta ndege ya kwanza ya ATC kutoka Canada.
Sitta alisema hadi utakapomalizia uongozi wa Rais Kikwete, reli ya kutoka Dar es Salaam kwenda, Kigoma, Tabora, Uvinza, Msongati, Kaliua, Mpanda Kamero, itakuwa imejengwa.
Kuhusu mabehwea mabovu, alisema watu hao watashughulikiwa na hawezi kuona watu wezi wadogo wakishughulikiwa huku wale wakubwa wakiachwa.
“Hiawezekani watu wachache watuhujumu tuwaache,” alisema Sitta.
Alisema pia atahakikisha ujenzi wa reli kutoka Dar es Salaam kwenda Burundi na Tanga hadi Musoma inasimamiwa na kukamilika.
Kuhusu Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kuwa kichochoro cha kupitisha sawa za kulevya, alisema atahakikisha suala hilo linakoma.

LUKUVI
Kwa upande wake, Waziri Lukuvi, aliingia ofisini juzi na kuanza kuzungumzia changamoto za migogoro ya ardhi na watumishi wasio waminifu kuwa ni mambo yanayomkabili.
“Natambua kabisa wengi wenu hapa ni miongoni mwa wanaokwamisha utendaji kazi, siwatishi, lakini nataka mtambue sijaja hapa sijui kitu kabisa. Kinachoendelea hapa nakijua na ninaahidi kuyashughulikia hayo,” alisema Lukuvi alipokuwa akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Migogoro ya ardhi
Lukuvi aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), sasa anakabiliwa na changamoto zilizoachwa na mtangulizi wake, Profesa Anna Tibaijuka, ikiwa pamoja na kukithiri kwa migogoro ya wakulima na wafugaji katika wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro na mgogoro wa ardhi wa Kiteto.
Mwaka jana mgogoro wa Kiteto ulisababisha mauji ya wakulima na wafugaji kutokana na kile kilichoelezwa kuvamia kwa makundi ya wakulima katika Hifadhi ya Embroi Murtangosi.
Mgogoro huo ulisababisha mauaji ya watu 15, huku wengine 14 wakijeruhiwa.

Makazi holela
Changamoto nyingine inayomsubiri Lukuvi ni makazi holela mijini, hasa Dar es Salaam. Asilimia 70 ya wakazi wa jiji hilo huishi kwenye makazi holela, huku baadhi ya matajiri wakijenga nyumba karibu na fukwe za bahari na wengine wakiziba mito inayotiririka kuelekea baharini, kinyume na sheria.

Mji mpya wa Kigamboni
Changamoto nyingine ni ujenzi wa mji wa Kigamboni uliotarajiwa kugharimu kiasi Sh trilioni 19.
Akitoa tathmini ya wizara hiyo, Mkuruenzi wa Taasisi ya Haki Ardhi, Yefred Myenzi, aligusia mambo matatu muhimu yaliyomo kwenye wizara hiyo.
“Kwanza asilimia zaidi ya 90 ya ardhi ya Tanzania haijapimwa, jambo linalochochea migogoro ya ardhi kila uchao huku kukiwa na msongamano wa watu, makazi na magari mijini.
“Dar es Salaam ilipimwa kwa mara ya mwisho mwaka 2003 katika mradi wa viwanja 60. Vilevile kuna upimaji tu kwenye maeneo ya miradi michache, lakini siyo kote. Huko vijijini kwenye asilimia 70 ya ardhi nako kunatakiwa kuwekewa mipango ya matumizi bora ya ardhi,” alisema Myenzi.

Matumizi bora ya ardhi
Alitaja changamoto ya pili kuwa ni kutokuwapo kwa usimamizi mzuri wa sheria katika kugawa na matumizi ya ardhi.
“Sheria na taratibu hazifuatwi na watendaji kwenye halmashauri hadi wizarani. Kwa mfano kuna sheria inayotaka matumizi ya ardhi ysibadilishwe kwa mtu aliyemilikishwa. Lakini kuna mwekezaji kule Mbarali, Mbeya alimilikishwa shamba la mpunga, yeye akalifanya kuwa la mibono,” alisema.

Rushwa
Alitaja changamoto ya tatu kuwa ni kukithiri kwa rushwa katika sekta ya ardhi kunakosababishwa na urasimu mkubwa.
“Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendelo ya Makazi imetajwa mara kadhaa katika ripoti za Transparency International na East African Bribery Index kwa kukithiri kwa rushwa. Hilo ni jambo ambalo Waziri Lukuvi anapaswa kulivalia njuga,” alisema Myenzi.
Kuhusu ujenzi wa Kigamboni, Myenzi alisema kuna miradi mitatu ambayo ni Mji Mpya wa Kigamboni (New Satellite City) unaosimamiwa na Kigamboni Development Authority.
Mwingine ni mji mpya wa Kibada, mradi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wanaotarajia kujenga kituo cha michezo na mradi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
“Mradi wa mji mpya Kigamboni umekiuka sheria za ardhi, ikiwa pamoja na sheria za mipango miji, na wananchi hawakushirikishwa vya kutosha licha ya kukatazwa kuendeleza makazi yao bila hata kufidiwa kwa zaidi ya miaka miwili,” alisema Myenzi.

SIMBACHAWENE
Kwa upande wa Waziri wa Nishati na Madini, Simbachawene, suala la utekelezaji wa mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, na kupunguza bei ya nishati ya umeme na maji, ni changamoto kubwa kwake.

Gesi
Katika sekta ya gesi, kuna kashfa inayoinyemelea wizara hiyo ya ufisadi wa dola milioni 600 za Marekani, sawa na Sh trilioni 1.2, zilizotumika katika mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Inadaiwa baadhi ya viongozi wa Serikali walijiongezea fedha hizo na kusababisha mradi huo sasa kugharimu Sh trilioni 2.40.
Mradi huo mkubwa wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ambao unamilikiwa na Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kwa asilimia 100 unaelekea ukingoni kukamilika.
Taarifa iliyotolewa na TPDC kupitia wataalamu wake wanaosimamia na kuratibu ujenzi wa mradi huo, inabainisha kuwa sehemu kubwa ya shughuli mbalimbali zinazounda mradi huo zimekamilika kwa kiwango kikubwa.
Shughuli ambazo zimekamilika kwa asilimia mia moja hadi Julai, 2014 kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni usafishaji wa njia, yaani Mkuza kwa ajili ya kupitisha bomba la gesi na usimikaji wa mabomba baharini kutoka Mnazi Bay hadi Madimba mkoani Mtwara, urefu wa kilomita 4.748.
Shughuli nyingine ambazo zimekamilika kwa kiwango kikubwa ni pamoja na usafirishaji wa mabomba ya gesi kutoka kwenye ghala hadi maeneo ya ujenzi ambayo tayari yamefikia urefu wa kilomita 501 kati ya 504, uungaanishwaji na uchomeleaji wa mabomba umekamilika kwa urefu wa kilomita 491 kati ya 504, uchimbaji wa mtaro kwa ajili ya kulaza mabomba umekamilika kwa kilomita 430 katika maeneo ya Dar es Salaam, Mkuranga, Lindi na Mtwara.
Vilevile kazi ya kulaza mabomba na nyaya za mawasiliano yaani Fibre Optic Cables kwenye mtaro imekamilika kwa kilomita 338, ufukiaji wa mabomba na nyaya za mawasiliano ambayo yameshawekwa kwenye mtaro umekamilika kwa kilomita 322.

Wawekezaji wa ndani
Kwa upande mwingine, aliyekuwa waziri katika wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo, alijikuta katika mgogoro na sekta binafsi iliyotaka kuhusishwa katika uwekezaji wa gesi.
Profesa Muhongo aliwaambia watu wa sekta binafsi kuwa hawana uwezo wa kuwkeza kwenye sekta ya gesi bali uwezo wao ni kwenye juisi na matunda.
Hali hiyo imeleta mgongano kati ya Serikali na sekta binafsi, jambo linalomsubiri Simbachawene anapoingia katika wizara hiyo.

Madini na usiri wa mikataba
Katika sekta ya madini bado kuna kilio kikubwa cha upotevu wa mapato, huku ikielezwa makampuni makubwa ya kimataifa ndiyo yanayofaidika.
Makampuni hayo ni pamoja na Golden Pride iliyokuwa na mgodi Nzega na sasa imefunga shughuli zake, Geita Gold Mine, Bulyanhulu uliopo Kahama, North Mara uliopo Tarime na Buzwagi uliopo Kahama yote ikimilikiwa na Kampuni ya Accacia Mining.
Mgodi wa Tulawaka uliopo Biharamulo kwa sasa unamilikiwa na Shirika la Taifa la Madini (STAMICO). Mwingine ni mgodi wa Buhemba uliopo Musoma Vijijini.
Hadi sasa migodi hiyo inalipa mrabaha wa asilimia 4 tu, huku kodi inayolipwa kwa wingi ni ile ya makato ya hifadhi za jamii za wafanyakazi. Hivyo Serikali inapoteza mapato mengi.
Changamoto nyingine ni usiri wa mikataba kati ya Serikali na kampuni hizo za madini hali inayoendelea kutia shaka katika upatikanaji wa mapato ya madini kwa manufaa ya taifa.

Umeme vijijini
Kuhusu nishati, japo Serikali imejitahidi kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), bado ni Watanzania wachache tu wanaotumia nishati hiyo, huku wengi wakiishi gizani.
Katika awamu yake ya pili, REA imelenga kuunganisha umeme kutoka vijiji 3,734 kati ya 15,000 sawa na asilimia 26 hadi kufikia vijiji 5,234 sawa na asilimia 34.5 ifikapo Juni.
Hata hivyo, hadi sasa Watanzania wanaotumia umeme ni asilimia 20, huku Serikali ikilenga kufikisha asilimia 30 mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles