26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Limeni kilimo cha kisasa-Dk.Chaya

Na Ramadhan Hassan, Manyoni

Mbunge wa Manyoni Mashariki, Dk. Pius Chaya (CCM) amewataka Wakulima Wilayani Manyoni kulima kilimo cha kisasa na chenye tija ili kuinua  uchumi wa familia zao, Wilaya na Taifa kwa ujumla.

Dk. Chaya ameyasema  hayo katika Semina iliyoendeshwa na Mfuko wa Taifa wa pembejeo Wilayani Manyoni ambayo ilikuwa na lengo la kuwasaidia wakulima hao kupata mikopo ya pembejeo na kuitumia kwa ufanisi.

“Tunahitaji Wakulima wetu walime kisasa ili kuongeza kipato, na ndiyo maana niliamua kuwafuata watu wa Mfuko wa Taifa wa pembejeo waje Manyoni kutoa semina hii,”amesema

Dk. Chaya amesema  kuwa semina hiyo itasaidia wakulima wengi kupata mikopo na hakutakuwa na urasimu wala ukiritimba ambao umekuwa ukilalamikiwa na baadhi ya wakulima na Nchini.

“Tutasaidia wakulima wengi kupata mikopo kwa kufuata vigezo, ili kusaidia juhudi za Rais Magufuli katika kuwaletea maendeleo Wananchi wa Tanzania kwani Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ni kuboresha maisha ya wakulima hivyo na mimi siwezi kuwasahau,”amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwagisa akizungumza wakati akifungua Seimna hiyo amewataka  Wakulima Wilayani Manyoni iwapo watafanikiwa kupata mikopo hiyo basi walime kwa tija ili waweze kuilipa.

“Ningependa kusisitiza, pamoja na kufanikiwa kupata mikopo lakini mfanye kilimo chenye tija. Hamasa ni kubwa kwani wengine wana ekari 50 mpaka 100 lakini limeni kwa tija. Iwe alizeti au korosho, limeni kwa tija ili kukuza uchumi wetu kwani Serikali na Mbunge tuko bega kwa bega nanyi” amesema Mwagisa.

Naye, Afisa Uendeshaji kutoka Mfuko wa pembejeo wa Taifa, Joshua Kaleb amesema changamoto zinazowakabili wakulima ni pamoja na ukosefu wa  pembejeo, matumizi ya zana hafifu na kulima kwa kutegemea mvua.

Ameongeza  kuwa Mfuko wa pembejeo unajitahidi kutoa elimu ya kilimo cha kisasa na kutoa mikopo ya pembejeo ili kumsaidia mkulima wa Tanzania kuingiza kipato kikubwa na kuachana na kilimo cha mazoea.

Naye, Kaimu Afisa Kilimo Wilaya ya Manyoni Emelita Kyenga akizungumza baada ya semina hiyo aliwahakikishia wakulima kuwa hakuna vikwazo katika kupata mikopo cha msingi ni kufuata vigezo kwa kukamilisha kujaza fomu zote na kwa usahihi vipitishwe na hatimae wapate.

Hata hivyo baadhi ya wakulima wametoa pongezi kwa Mbunge wao Dk. Chaya kwa kuwatafutia semina hiyo kwani wanaamini itakuwa msaada kwao.

“Semina hii ni nzuri, nimepata ufumbuzi wa njia sahihi ya kupata mkopo sasa naweza kulima bila kutumia nguvu kubwa” alisema mmoja wa wakulima.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakulima wa zao la korosho Wilayani Manyoni Issa Madenge amewashauri wakulima wenzake kutekeleza masharti ya mikopo ya pembejeo ili waipate na kuweza kuwasaidia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles