28 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali Zanzibar yahimiza nidhamu ya mikopo

Na Mwandishi Wetu, Unguja

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Abdallah Hussein Kombo, amewataka wananchi kuwa na nidhamu ya hali ya juu katika matumizi ya mikopo ili waendelee kukopesheka.

Kiongozi huyo alisema mikopo ikitumika kwa malengo yaliyowekwa itaweza kurejeshwa vizuri na kuwaongezea imani wakopeshaji ili waendelee kukopesha na kuongeza uwezo wa kutoa mikopo zaidi.

Waziri Kombo aliyasema hayo mwishoni mwa wiki huko Marumbi wilaya ya Kati Unguja wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa vijiji sita baada ya Benki ya NMB kukutana nao kupanga mikakati ya jinsi ya kuwasaidia katika harakati zao za maisha na maendeleo kwa ujumla.

NMB imetoa fursa ya mikopo kwa wavuvi na wakulima wa mwani wa vijiji hivyo ili kuitumia fursa ya uchumi wa buluu na kuweza kujiinua kiuchumi samabamba na kuleta maendeleo ya nchi.

WAZIRI wa Uchumi wa Buluu na Uvivu Zanzibar (Zanzibar Blue Economy and Fisheries Minister) Abdalla Hussein Kombo akizungumza na wakulima wa vijiji sita vya wilaya ya Kati baada ya uongozi wa benki ya NMB kufika kijijini hapo kupanga mikakati ya jinsi ya kuwasaidia kwa kuwapa mikopo  wananchi hao katika kuendeleza harakati zao za maisha.

Dk Kombo aliupongeza uongozi wa benki hiyo kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta mageuzi ya uchumi wa buluu Zanzibar.

“Nawaomba wananchi mthamini juhudi za Benki ya NMB kwa kuhakikisha mnajipanga vyema ili kupokea mikopo hiyo na kuitumia kama ilivyokusudiwa kwani kufanya hivyo kutajenga imani kwa NMB kuzidi kuwasaidia,” Dk. Kombo aliwaasa wananchi hao katika hotuba yake.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuleta mageuzi ya uchumi kwa kuwawezesha wananchi wake hasa wanyonge kuweza kujikimu, hivyo hatua iliyochukuliwa na NMB kwa kiasi kikubwa itasaidia sana kutimiza malengo ya serikali,” aliongeza.

Pia alisema Serikali itaendelea kushirikiana na benki hiyo ili kuona malengo yaliyopangwa yanatimia na kuiomba kufikiria miradi mingine katika kuwasaidia wananchi wa vijijini.

NMB imesema iko tayari kuwakopesha wananchi ili washiriki kikamilifu katika uchumi wa buluu ambao maendeleo yake ni moja ya ajenda kubwa za Serikali ya Dk. Hussein Mwinyi.

Katika mkutano uliofanyika katika Skuli ya Marumbi, Meneja Mwandamizi wa kitengo cha Kilimo Biashara wa NMB, Wogofya Msalamagoha, alisema wataiunga mkono serikali kuhakikisha lengo lake hilo linatimia.

“Katika kuiunga mkono serikali kwenye suala zima la uchumi wa buluu, NMB imeona ni vyema kuwawezesha wakulima wa mwani na wavuvi kwa kuwapatia mkopo ili kujiletea maendelo kupitia fursa hiyo,” alisema Msalamagoha.

NMB itasaidia kutoa mikopo ya fedha pamoja na vifaa na pembejeo mbalimbali zinazohitajika katika kufanikisha suala zima la uvuvi na kilimo cha mwani ambayo itarejeshwa mara baada ya kuvuna na kuuza.

Naye Meneja wa NMB kwa upande wa Zanzibar, Abdallah Duchi, alisema benki hiyo imejipanga vyema kusaidia kutatua changamoto za wavuvi na wakulima wa mwani ili waweze kuchangia kikamilifu maendeleo ya nchi

Akizungumzia fursa hiyo mpya, Mlenge Khatib ambaye ni mvuvi kutoka kijiji cha Chwaka, aliishukuru NMB kwa kuwapa matumaini makubwa ya kujiinua kiuchumi kupitia ukopeshwaji huo utakaoambatana na kutafutiwa masoko ya kuuzia bidhaa zao.

Mlenge alisema changamoto kubwa katika uvuvi wa mwani ni kuwepo kwa uhaba wa masoko jambo ambalo hupelekea bei ya mwani kuwa chini kwa kuridhia kiasi cha mteja anachokitoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles