32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

KWANINI UNALAUMIWA WEWE TU?

Na ATHUMANI MOHAMED  

LEO nitaanza mada yangu kwa mfano. Joan (siyo jina halisi) ni msichana msomi, mwenye kujituma na kufanya kazi kwa bidii. Alikuwa akifanya kazi katika kampuni moja jijini Dar es Salaam.

Pamoja na kufanya kwake kazi kwa bidii sana, akijituma na kuwa na ubunifu wa hali ya juu, watu wengi kazini kwake hawakumpenda.

Joan hakupendwa si tu na wafanyakazi wa chini yake, lakini hata mabosi zake. Kwa sababu hiyo alikuwa akigombana na watu kila siku. Leo atagombana na Jamila, kesho Paul.

Sababu hiyo ilimfanya Joan kuchukia na kuamua kuacha kazi katika kampuni hiyo. Baada ya muda akapata kazi katika kampuni nyingine. Alivyoanza kazi kwenye kampuni hiyo mambo yalikuwa mazuri, lakini muda mfupi baadaye hali ikawa ileile.

Uamuzi alioufikia baada ya kuchoshwa na kelele za watu wanaomzunguka ulikuwa ni kuacha kazi. Bahati nzuri kwa Joan ni kwamba kila alipokuwa akiacha kazi, alipata mahali pengine baada ya muda mfupi.

Sababu kubwa ya kupata kazi, pamoja na bahati, alikuwa na CV nzuri, lakini pia rekodi yake ya kuchapa kazi iliridhisha, akiwa msomi mzuri.

Maisha yake kikazi yakaendelea kuwa ya namna hiyo. Kufanya kazi kwa lawama kila mahali. Alichukizwa sana na hali hiyo, lakini ukweli ni kwamba hakujua namna ya kushughulikia tatizo lake.

Kilichosababisha awe mtu wa kugombana na watu kila wakati ilikuwa ni tabia yake ya ujuaji, ujeuri na majibu ya hovyo. Msichana huyo alikuwa mkorofi, msema hovyo na mwenye mdomo!

Kazi yake kubwa ilikuwa kuchukua maneno sehemu moja na kuyapeleka sehemu nyingine.  Leo anagombanisha wale, kesho anatamba kuwa yeye ni mfanyakazi bora zaidi kuliko wengine.

Ni kweli alikuwa akijitahidi kufanya kazi kwa bidii sana, lakini kule kuwasema wenzake kuwa hawawezi, kulimshushia heshima yake. Wengi wakawa wakimchukia.

Alielewana na wachache sana wenye tabia kama zake. Kwa hakika hakuna mtu ambaye angependa kufanya kazi na mtu wa namna yake.

Kitu kimoja tu ambacho alipaswa kufanya ni kubadili tabia yake na siyo kubadili ofisi kila kukicha. Ndugu msomaji wangu wapendwa, bila shaka utakuwa umepata picha halisi ya kile ninachotaka kukizungumzia leo.

Unaweza kulalamika kuwa watu wanaokuzunguka wana matatizo kwa kukulaumu kumbe wewe mwenyewe ndiye mwenye matatizo na unapaswa kubadilika.

 

WEWE UNAISHIJE?

Maisha yako yakoje? Yanafanana na ya Joan? Jenga tabia ya kujipima mwenyewe. Unawafanyia wenzako mema? Inawezekana kila nyumba unayopanga unaona matatizo kwa sababu watu wanakulaumu zaidi, lakini umewahi kujiuliza kuhusu lawama wanazokutupia?

Angalia mtindo wako wa maisha vizuri. Acha kuwalaumu wengine kabla ya kujichunguza. Pengine inawezekana maisha yako ni kikwazo kwa wenzako na laiti kama ungepata muda mfupi tu kutafakari, ungechukua hatua ya kubadilika.

Kama upo kwenye ajira, acha kutegea. Fanya kazi kwa bidii, heshimu sheria za kazi. Wahi kazini na fanya kazi zako kwa weledi.

Wapo wanajiona ni bora zaidi ya wengine; huko ni kujidanganya. Ubora wako haupimi wewe, kiwango chako kitajulikana kutoka kwa watu wanaokuzunguka.

 

JISAHIHISHE

Muungwana huchukua hatua ya kujirekebisha pindi anapoona amekosea. Kuwaudhi wengine ni tatizo kwenye maisha. Unaweza kudhani watu hawajui tabia zako, lakini ukweli ni kwamba sifa mbaya huenea zaidi kuliko nzuri.

Unaweza kuhama nyumba nyingi sawa, unaweza kubadilisha mahali pa kazi utakavyoweza, lakini ipo siku watu watajua tabia zako, wataambiana na utakuwa mwisho wako wa kutokukubalika mahali popote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles