
Na Asifiwe George, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema watu wanaotumia simu feki wajiandae kwa maumivu kwa vile wataweza kutamba nazo hadi saa 5:59 usiku wa leo.
Itakapotimia saa 6.00 kamili usiku simu hizo ambazo hazina viwango zitafungiwa na kutotumika tena, imesema TCRA.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba, alisema hatua hiyo ya kuzimwa simu feki itarushwa moja kwa moja na vyombo vyote vya habari hasa runinga.
Kilaba alitoa hahadhari kwa k wauzaji wa vifaa vya mawasiliano ya mkononi na mafundi simu kwamba atakayebainika kubadili namba tambulishi za vifaa vya simu adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka 10 au faini ya Sh milioni 30 au vyote kwa pamoja.
Alisema mfumo huo wa elektroniki ulizinduliwa rasmi Desemba mwaka jana na unahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano.
Alisema uchambuzi uliofanywa Juni 14 mwaka huu, unaonyesha mabadiliko chanya ya idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango kupungua kutoka aslimia tatu hadi asilimia 2.96.
“Idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zimekuwa zikipungua kutoka asilimia mbili hadi kufikia asilimia 0.09 hivyo kufanya idadi ya namba tambulishi za simu halisi kuongezeka kutoka asilimia 85 hadi asilimia 96.95.
“Na idadi ya namba tambulishi za simu halisi ( IMEI) zimeongezeka na kufikia asilimia 96.95 kwa mujibu wa uchambuzi iliofanyika Juni 14, mwaka huu.
“…namba tambulishi za vifaa vyote vya mawasiliano vya mkononi ambavyo vimeibiwa, vimeharibika, kupotea au visivyokidhi viwango katika soko la mawasiliano havitaruhusiwa kuunganishwa kwenye mitandao ya watoa huduma kuanzia (kesho)leo,” alisema Kilaba.
Alisema katika kipindi cha kutoa elimu walikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo uaminifu mdogo kwa baadhi ya wauzaji wa simu kwa kutoa punguzo kwa wananchi kuwashawishi kuzinunua simu bandia kwa bei nafuu.
Alieleza changamoto nyingine kuwa ni uelewa mdogo wa wananchi katika kuitikia wito wa kuhakiki simu zao katika kipindi cha mpito.
Kilaba alieleza faida za mfumo rajisi wa namba tambulishi (IMEI) kuwa ni kupunguza wizi kwa njia ya simu, kuhimiza utii wa sheria na kujenga misingi ya matumizi ya simu halisi zisizo bandia.
TCRA imetoa mwito kwa wale wote wanaofanya biashara ya kuingiza simu nchini kuhakikisha simu wanazoleta zinakidhi viwango na zimehakikiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).