29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

KWA NINI WEMA SEPETU ANATUSUA?

Mama yake mzazi afunguka siri nzito

Na KYALAA SEHEYE

Unakumbuka Top 5 ya Miss Tanzania mwaka 2006? Kama kumbukumbu zimeondoka nitakukumbusha. Walikuwa ni Irene Uwoya, Wema Sepetu, Sarah Kangezi, Jokate Mwegelo na Lisa Jensen.

Miss Tanzania iliyofunika pengine kuliko mwaka wowote tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo.  Wakati walimbwende hao wakipanda jukwaani haikuwa rahisi kumbashiri mshindi.

Wengine walisema Miss Tanzania angekuwa Jokate, wapo waliomtaja Lisa, huku wengine wakidai angeshinda Sara.

Ubishani ulikuwa mkubwa, lakini kwa waliokuwepo enzi zile watakumbuka uzuri wa Irene Iwoya ulivyokuwa tishio kiasi cha kutabiriwa kuwa mshindi, lakini wapo waliosema Wema anastahili.

Yote kwa yote, ukweli ni kwamba Wema hakupewa nafasi kubwa ya kushinda, lakini mwisho wa siku Irene na Sara waliondoka na kubaki Lisa, Jokate na Wema kwenye Top 3 iliyomtangaza Wema kuwa ndiye mshindi.

Baadaye mwaka 2008 Wema aliingia kwenye tasnia ya filamu za Kibongo ambapo kwa mara ya kwanza alishiriki kwenye Filamu ya A Point Of No Return. Hapo Wema aling’ara tena.

Baada ya filamu hiyo aliyocheza na marehemu Steven Kanumba, aliendelea kuonyesha makali yake kwenye sinema nyingine nyingi na hajawahi kushuka kiwango.

Kwenye mambo ya kijamii ndiyo kabisa. Wema anang’ara kwenye siasa, tangu akiwa memba wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mpaka sasa ambapo amehamia Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Hata hivyo kwa sasa staa huyo mwenye umri wa miaka 29, amekuwa kimya na haonekani sana kwenye mitandao ya kijamii wala majarida ya burudani akihusishwa na skendo mbalimbali kama ilivyokuwa huko nyuma.

Nini kipo nyuma ya ukimya huo? Je, nini kinachomfanya Wema ang’are kwenye sanaa na mitindo? Mama yake mzazi, Miriam Sepetu amezungumza na Swaggaz na kufunguka mengi kuhusiana na mwanaye.

 

WEMA YUKO WAPI?

“Wema yupo. Namshukuru Mungu kwa hali iliyopo sasa maana ndiyo aliyopaswa kuwa nayo. Huwezi kumuona tena kwenye mitandao akishindana na watu au kujibizana. Maisha hayo yalishapita.

“Mwanangu Wema wa sasa ndiye yule niliyemuona kabla hajazaliwa. Huyu wa sasa ni Wema halisi na ninamshukuru Mungu kwa hilo,” anasema mama Wema, Miriam.

 

KUMBE ALIMUWEKEA NADHIRI

Anasema yeye na marehemu mumewe, Balozi Abrahamu Sepetu hawakumuita Wema kwa bahati mbaya kwani waliweka nadhiri kwa Mungu juu ya binti yao huyo.

“Mungu amenijalia watoto wa kike watupu. Tulikuwa na hamu ya kupata mtoto wa kiume. Wanne waliotangulia ni wa kike, tuliomba na tuliamini Wema angekuwa wa kiume, tukimtabiria makubwa – awe mtu wa kuitumikia na kuisaidia jamii.

“Lakini tulimwambia Mungu, kama ameamua kutupa mtoto mwingine wa kike, basi tungemuita Wema kwa maana Mungu amenitendea wema kwa kunipa mtoto huyo na atakuwa na baraka nyingi na radhi za Mwenyezi Mungu. Ikawa hivyo, akazaliwa Wema huyu unayemuona,” anasema mama Wema.

 

VIPI SKENDO?

Mama Wema anasema maisha aliyopita mwanaye siyo yale aliyokuwa akiamini mwanaye angeyaishi, lakini anamshukuru Mungu kwa vile kwa sasa ameanza kurudi kwenye mstari aliotaka awe.

“Hata manabii waliandamwa na kashfa kabla ya kueleweka kwa jamii kuwa ni watu wa aina gani. Pengine walipata mateso makubwa kuliko hata tunavyodhania kwa mwanangu.

“Mapito yake yalikuwa ni njia ya mafanikio na sasa yamekaribia bado siku chache Watanzania na dunia kwa ujumla watajua kuwa Wema aliandikiwa kuwa mtu wa aina gani katika hili taifa na aliyoyapitia ilikuwa moja ya njia ya kufikia malengo.

“Hata hivyo kwa sasa Wema amebadilika… na ninaona kabisa muda si mrefu anakuja kuwa kiongozi mwema na atawatumikia wananchi wake. Hayo maisha ya nyuma tuyaache. Kilichokuwa kinamharibu Wema ni kampani, sasa yupo vizuri.

“Nimeamua kumbadilisha mtoto wangu kabla sijafa ili aje kuwa Wema niliyemkusudia atakayesaidia jamii na kuwafanyia matendo yanayoendana na jina lake.

“Kabla hajazaliwa nilikuwa nimeshamuomba Mungu wangu, Wema aje kuwa mtu fulani, sasa sihitaji umaarufu wake alioupata na kuutunza kwa miaka 11 uje kuwa hauna historia.

“Nahitaji Wema aje kuwa mmoja wa wanawake watakaowekwa kwenye historia ya nchi hii. Hata hospitali niliyojifungulia, daktari wa Kizungu alilitabili hilo, ni kama alikuwa ndani ya maono yangu. Nataka hilo litimie siku moja,” anasema.

 

WEMA MPYA ANAKUJA

“Mashabiki na hata maadui zake watarajie makubwa safari hii maana anakuja kivingine – kiutetezi hata wasiompenda wataelewa kwanini alizaliwa na kuitwa Wema. Watamuona Wema mpya yule niliyemuwekea nadhiri.

“Unajua wengi wanashangaa kwanini nampigania Wema ilihali nina watoto wengine, ukweli ni kwamba napigania ahadi niliyoiweka mbele ya Mungu wangu kwa kuwa niliiona inatekelezeka, ila watu waliokuwa wakihitaji umaarufu na pesa kupitia jina la mwanangu walikuwa wakinikwamisha, sasa imefikia mwisho. Wema mpya anakuja kutekeleza maana ya jina lake kwa vitendo.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles