24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

NI OMMY DIMPOZ HUYUHUYU AU KOPI?

Na CHRISTOPHER MSEKENA

UKWELI ni kwamba Bongo Fleva inahitaji wasanii wenye mawazo chanya yanayokinzana lakini yanayolenga kuupeleka mbali muziki huo. Kwa maana hiyo kuna faida kubwa ya kuwepo kwa bifu za faida baina ya msanii na msanii au kundi na kundi.

Bifu za faida ni ule ugomvi wa msanii na msanii au kundi na kundi kutumia nguvu waliyonayo kwenye jamii kufanya biashara ya bidhaa zao za muziki lakini pia kupitia bifu hizo za faida tasnia nzima ya burudani inachangamka.

Mfano wasanii wakubwa duniani wenye mashabiki wengi hutumia bifu zao pale wanapotaka kudondosha albamu au kanda mseto (Mixtape) na hiyo huwasaidia kuwaongezea mauzo maana bifu zao zinafanya wasikauke kwenye vinywa vya watu na mashabiki wanunue kazi kwa kushindana.

Zitazame bifu za mastaa wa dunia kama Drake na Meek Mil au ile ya Remmy Maa na Nick Minaj. Ni bifu ambalo linaundwa kwenye mazingira yoyote lakini dira yao kubwa inakuwa ni kuwasaidia kibiashara na wanapiga pesa kweli kweli.

Hapa Bongo uhasimu ambao utachelewa kuisha ni ule wa wasanii Ali Kiba na Diamond Platnumz, ambao una miaka zaidi ya mitano sasa na kila siku unachukua sura mpya.

Uwezo wa kufanya bifu hilo liwaingizie mkwanja wanao kwa sababu wana nguvu ya ushawishi na wamefanikiwa kugawana mashabiki kiasi kwamba kuna timu kabisa – Team Kiba na Team Mond na aina ya mashabiki wao wamefanya uhasimu huo ufanane na ule wa vilabu vya soko vya Simba na Yanga.

Uhasimu wao ulianza kufifia lakini ghafla mapema wiki hii mkongwe wa muziki wa Hip Hop nchini, Fareed Kubanda ‘Fid Q’ baada ya kuachia toleo mbadala (remix) la ngoma yake ya Fresh ambayo amewashirikisha wasanii Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Rayvanny kutoka WCB, bifu la Chibu na Ali Kiba limefufuka upya na makali yake.

Inafahamika Diamond alianza muziki kwa kuchana vesi kwenye remix hiyo ya Fid Q, alichora mistari kwenzi iliyobeba maneno yaliyohisiwa moja kwa moja kumdisi hasimu wake, Ali Kiba ambaye yupo nchini Marekani kutumbuiza kwenye Tamasha la One Africa Music Festival 2017.

Katika mistari hiyo Diamond alionyesha wazi kutopenda kufananishwa na Ali Kiba aliyepata ustaa kupitia wimbo wake wa Cinderella, sambamba na kumwachia kiti cha ufalme pale Kiba alipokitaka naye akampa na kitanda ili alale kabisa.

Ali Kiba akaona isiwe tabu, akamjibu Diamond kupitia ukurasa wake wa Twitter kwa kusema: “Mfalme atabaki kuwa mfalme, Je umeshakitandika nilale malkia wangu wa nguvu?”

Maneno hayo ya utani yalimkera Diamond na akazama tena studio kurekodi disi nyingine.

Safari hii Diamond aliwachana Ali Kiba na Ommy Dimpoz kwa pamoja ambao wote wawili wamekuwa pamoja nchini Marekani kwa kuwa hivi sasa wapo lebo moja ya Rockstar4000, ambapo safari hii Ali Kiba hakujibu badala yake Ommy Dimpoz alimjibu kwa namna ambayo si sahihi sana.

Ommy Dimpoz aliweka picha kwenye ukurasa wake ndani ya Mtandao wa Kijamii wa Instagram, katika picha hiyo ambayo ameshaifuta, yupo na mama mzazi wa Diamond. Katika picha hiyo, ameandika maneno yanayoonyesha kuwa aliwahi kutoka kimapenzi na bimkubwa huyo jambo ambalo kiukweli linatutoa katika burudani na kutupeleka kwenye fedheha inayofanya tuone tasnia imejaa uhuni.

Ommy Dimpoz aliwahi kusema moja kati ya vitu vinavyomtoa machozi ni mashabiki kumtukania marehemu mama yake, huyohuyo alilia pale Escape One (ukumbini) alipokuwa akitumbuiza wimbo wa Nani Kama Mama na Christian Bella.

Dimpoz amekuwa na mapenzi makubwa na kina mama, iweje leo amdhalilishe mwanamke na mama mwenye haiba ya mama yake mzazi? Hapo ishu siyo kumjibu Diamond ishu bali kumdhalilisha mama ambaye hahusiki kwenye hilo bifu lao la kitoto.

Waungwana wanajiuliza, iweje leo hii Dimpoz ajisahau kiasi hicho? Anawezaje kumhusisha mama mtu mzima kwenye mabishano yao ya kikazi? Ni utoto na kutokuwa na busara.

Hili si jambo la kufumbiwa macho, linapaswa kuangalia kwa mapana na ikiwezekana mamlaka husika zimchukulie hatua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles