27.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

WATOTO WA MICHAEL JACKSON WANAVYOMUENZI BABA YAO

Na BADI MCHOMOLO

NI miaka nane sasa tangu aliyekuwa nguli wa muziki wa Pop duniani, Michael Jackson apoteze maisha kwa mshtuko wa moyo.

Lilikuwa pigo kubwa kwa wadau wa muziki duniani na familia huku akiwa ameacha watoto watatu waliotambulika kwa majina Prince, Paris na Blanket.

Wakati anapoteza maisha kijana wake wa kwanza Prince alikuwa na umri wa miaka 12, akiwa ni wa kwanza kuzaliwa, akifuatiwa Paris ambaye aliachwa akiwa na umri wa miaka 11 na Blanket miaka saba.

Prince na Paris walikuwa na uwezo wa kuelewa nini kinaendelea katika maisha yanayowazunguka tofauti na Blanket. Kwa sasa Prince ana umri wa miaka 20, Paris 19 na Blanket ana miaka 15.

Mbali na utajiri walioachiwa na baba yao, lakini wamedai watahakikisha wanapambana ili kuliendeleza jina la Jackson katika maisha yao ya kila siku na baadaye, hawataki jina hilo lipotee ulimwenguni.

Kila mmoja kati ya watoto hao wamekuwa na ahadi za kuhakikisha analitendea haki jina hilo hasa katika mafanikio.

 

PRINCE JACKSON

Hana jina kubwa kwenye mitandao ya kijamii kama ilivyo kwa mdogo wake Paris, lakini ameweka wazi kuwa anataka kuhakikisha jina la baba yake linabaki kwenye ramani ya muziki.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 20, ameamua kwenda shule kwa ajili ya kusomea muziki ili azidi kulitangaza jina la baba yake.

“Wakati nakuwa baba aliwahi kuniuliza kuwa nataka kuja kuwa nani katika maisha yangu, nilimwambia nataka kuwa prodyuza wa video za muziki. Nashukuru tayari nina studio yangu ikijulikana kwa jina la King’s Son.

“Nitahakikisha kila kitu kinakuwa sawa kwa kuwa baba alikuwa anapenda muziki, lazima mmoja wa watoto wake afanye kile alichokuwa anakifanya yeye ikiwa ni sehemu ya kumuenzi.

“Nilikuwa na lengo la kuja kufanya aina ya muziki wake, lakini nimeshindwa, hivyo nimeona bora nipambane na kazi ya kuwa prodyuza na kuongoza video,” alisema Prince.


PARIS JACKSON

Ni mtoto wa kike wa pekee wa Jackson, katika maisha yake alitamani sana kuja kufanya muziki kama ilivyo baba yake na shangazi yake, lakini kila akijaribu alijikuta akishindwa.

Kutokana na hali hiyo aliamua kuingia kwenye mitindo na kufanya filamu, hivyo ameweza kupiga hatua kwa kuwa jina lake limekuwa juu kwenye mitandao ya kijamii kuliko lilivyo la kaka yake.

Anaamini kufanya filamu na mitindo kutalifanya jina la baba yake liendelee kuwepo kwenye midomo ya mashabiki wake, lakini akaona aende mbali zaidi kwa kuamua kuchora tattoo mwilini za picha za baba yake pamoja na baadhi ya ujumbe aliowaachia.

“Kuna watu wanaamini baba yetu alikuwa mfalme wa muziki wa Pop, lakini kwa upande wangu naweza kusema alikuwa ni mfalme wa moyo wangu.

“Nilitamani siku moja nije kufanya muziki kama yeye ili niweze kumuenzi, lakini nimejaribu nimeshindwa, kuna mambo mengi ya kufanya ili kuendelea kuliweka jina la Jackson kwenye midomo ya mashabiki wake.

“Nashukuru watoto wote tunaishi vizuri kutokana na aina ya maisha ambayo baba yetu alituwekea,” alisema Paris.

Mrembo huyo amekuwa akishauriwa mara kwa mara kuacha kuvuta sigara, lakini jambo hilo ameliweka wazi kuwa anashindwa kuacha kutokana kuwa na marafiki wingi wa kiume ambao wanavuta sana sigara.

“Nimekuwa nikijaribu kuacha kuvuta sigara, lakini nimeshindwa, naamini kuna uwezekano mkubwa wa kuja kuniletea matatizo katika maisha yangu ya baadaye,” aliongeza.

BLANKET JACKSON

Ni mtoto wa pili wa kiume, lakini ni wa mwisho kati ya watoto watatu, mtoto huyo hadi sasa hajulikani mama yake kwa kuwa inadaiwa alipatikana kwa kupandikizwa (surrogate).

Kwa mujibu wa familia ya Jackson, mtoto huyo miaka ya hivi karibuni amekuwa akisisitiza kutaka kulitangaza jina la baba yake japokuwa hana uhakika wa kuwa na mashabiki wengi duniani.

“Sikuweza kufurahia maisha vizuri nikiwa na baba yangu, ameniacha nikiwa na miaka saba, lakini najua kama aliweka historia katika muziki wa Pop duniani, lengo langu ni kuhakikisha nalitangaza jina la Jackson kama familia yangu inavyotaka.

“Sikufikiria kufanya muziki kama ilivyo kwa baba, ila kwa upande wangu nimeona bora niangukie kwenye mchezo wa ngumi ‘Martial arts’, ambao  naamini nikifanya vizuri kwenye mchezo huo nitalitangaza jina la baba,” alisema Blanket.

Blanket ni mtoto mwenye tabia za kipekee, anadaiwa kuwa ni mtu wa aibu sana mbele za watu ambao hawajui, anapenda sana michezo, licha ya kuwa kwenye Chuo cha Martial arts, lakini analelewa na bibi na babu ambao ni wazazi wa Jackson.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles