24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MSHAHARA MPYA Z’BAR VURUGU TUPU

Na BAKARI KIMWANGA-ZANZIBAR

NYONGEZA ya mishahara ya asilimia 104 iliyofanywa na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Maudline Castico, bila kushirikisha wadau imezua kizaazaa huku Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, akitakiwa kuingilia kati.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Unguja, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI), Seif Masoud Miskry, alisema wanashangazwa na hatua ya Waziri Castico kuwatumia maofisa wake kwa kupita kwenye hoteli mbalimbali visiwani hapa hali ya kuwa amewakimbia kwenye vikao vya majadiliano kwa mujibu wa utaratibu.

 

“Jana (juzi) Zati imeshtushwa na tamko la Chama cha Wafanyakazi Zanzibar ambao wanadai kwamba Zati imekuwa ikitoa maelekezo kwa wamiliki wa mahoteli eti wasilipwe kima kipya cha nyongeza ya mshahara kama ilivyotangazwa na Waziri Castico.

 

 

“Madai haya si ya kweli ila sisi tulikutana na Waziri Julai 25 na 26 mwaka huu ambapo pamoja na majadiliano akatuagiza tusilipe kiwango kipya ila tulipe mishahara ile ya zamani kwa sababu bado hatujakubaliana kwa mujibu wa utaratibu.

 

 

 

“Si nia yetu kuona Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla ambao wanafanyakazi kwenye sekta ya hoteli wakipoteza ajira, ila lengo letu ni kuona wengi wakinufaika na kazi yao kwa kuwa na malipo bora ambayo hayawezi kuumiza upande wowote na mbona hakuna majibu ya kikao chetu tulichokutana Juni 6, mwaka huu,” alisema Miskry.

 

Kutokana na hali hiyo, alisema Julai 27, mwaka huu aliandikiwa barua na Katibu wa Waziri yenye kumbukumbu namba WKUWVWW/0019.70.VOL.1/42  ikimwarifu kuahirishwa kwa kikao cha pili kilichotarajiwa kufanyika  ili kujadili hali hiyo.

 

 

 

Alisema katika barua hiyo iliyosainiwa na Ameir A. Ameir, ilieleza kwamba, Waziri Castico amelichukua suala hilo na kwenda kujadiliana na wenzake na baada ya siku moja akasema anakwenda Pemba na Rais jambo ambalo wao bado wanaamini wanaendelea kulipa mishahara ya zamani kwa maelekezo yake ya awali.

“Sijawahi kuona mahali popote duniani na hili si nia yetu sisi Zati kupingana na Serikali, tangazo la new minimum wages linatolewa ndani ya wiki tatu na tunatakiwa kutekeleza? Kwa hili tulipofika leo hii kama mnavyoona wawekezaji wote wa sekta ya hoteli hapa Zanzibar wamepatwa na hataruki na hatujui la kufanya,” alisema.

Alisema Zati imeshtushwa na namna uamuzi wa Serikali kupandisha mishahara huku wakiwa hawajajibiwa barua zao zaidi ya mbili walizoandika kwa Serikali kuhusu hali hiyo.

Alisema hatua hiyo inaweza kuleta athari, lakini akaeleza kuwa si busara kwa wawekezaji hao kuanza kuchukua hatua ya ama kupunguza wafanyakazi au kukata marupurupu wanayowalipa katika utaratibu waliojipangia.

Miskry alisema Zati inaamini kwamba, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni sikivu na haiko tayari kuona sekta ya utalii inatetereka, lakini hata jumuiya hiyo haitaki kuwaumiza wafanyakazi kwa malipo kidogo.

Mwakilishi CCM ajitosa

Kwa upande wake mlezi wa Zati ambaye pia ni Mwakilishi wa Tunguu, Simai Mohammed Said (CCM), alisema anashangazwa na uamuzi wa Waziri Castico kuwakwepa wawekezaji wa hoteli jambo ambalo ni hatari kwa uchumi wa Zanzibar na watu wake.

 

Kutokana na hali hiyo, alisema wageni hao Zanzibar hushindana na nchi kama Thailand, Tunisia, Morocco, Hispania, Visiwa vya Ugiriki kama Crete, Mexico, Cuba, St. Lucia pamoja na visiwa vingine.

Alisema wanaouza nafasi za hoteli kwa Zanzibar kwa nchi za Ulaya tayari wanaanza kuona Zanzibar ni bei ghali hasa ikiwa mishahara itapanda kupindukia na wao itawafanya wapandishe bei, ina maana katika mapumziko ya mwaka 2018 wataiondoa Zanzibar katika mabango ya kuitangaza hasa kwenye mitandao ya kununua likizo hizo.

 

 

 

“Ninamwomba Rais wetu Dk. Ali Mohamed Shein aingilie suala hili maana kauli yake inaweza kunusuru ajira za Wazanzibari pamoja na wawekezaji wa utalii ambao sasa huenda wakakumbwa na mzigo mkubwa wa gharama na nchi yetu ikajikuta ikishuka kwenye utalii,” alisema Simai.

Alisema kama Waziri Castico alikuwa na nia njema kwanini hadi sasa anawaogopa wawekezaji hao wa hoteli kufanya nao kikao cha pamoja.

Mabadiliko hayo yamefanyika chini ya kifungu cha 97 (1) cha sheria ya Ajira nambari 11 ya mwaka 2005 ambapo kima cha chini kwa wafanyakazi  wenye mikataba ya maandishi kwa taasisi ndogo zitakazoainishwa kwenye kanuni kimeongezeka kutoka Sh 145,000 hadi 180,000.

Kwa wafanyakazi wenye mikataba ikiongezwa kutoka kiwango cha sasa cha Sh 145,000 hadi 300,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles