29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kuwashangilia akina Obama haitusaidii

Na Markus Mpangala

NITANGULIE kuwaomba radhi wasomaji wangu kwa kukosekana wiki iliyopita, kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu. Sote ni binadamu ambao hukutwa na magonjwa, majukumu na mengineyo yanayotufanya tuwe mbali na vile vitu tulivyovizoea. Baada ya kusema hayo, naomba sasa tujadiliane suala ambalo limekuwa likinifikirisha kwa muda mrefu.

Nchi yetu imeingia kwenye mwingiliano mkubwa wa masuala ya kijamii kama ambavyo historia ya watu wa kale walivyoweza kuzaliana kutoka makabila tofauti. kwa sasa tunao watu waliozaliwa kutokana na mchanganyiko wa wazazi.

Kwa mfano tunao wananchi waliozaliwa kutokana na raia wa Tanzania na nchi za nje. Mzungu anaweza kuzaa na mwafrika wa Tanzania au mwafrika wa Tanzania amezaa na mwarabu au mhindi, mchina mwenye asili ya Asia. Tunao wananchi wengi waliozaliwa kutokana na mchanganyiko wa wazazi. Mfano mzuri ni Timu yetu ya taifa ya mchezo wa kuogelea.

Kuna wachezaji wenye asili ya kiasia, kizungu, kichina na kadhalika. Mchanganyiko huo unakuwa na maana moja tu kuwa wao ni watanzania. Wapo wazungu ambao wamechukua uraia wa nchi hii kama akina Richard Mabala na wengineo.

Tunao wazungu walioamua kuishi nchini na kuchukua uraia wa Tanzania. Kwa hiyo hawa watakuwa na watoto wao ambao kwa mujibu wa sheria watatumbulika kama watanzania. Kwa mantiki hiyo utaona kuwa mustakabali wan chi yetu hauwezi kwenda kinyume cha jamii inayoundwa sasa.

Kwamba Tanzania itakuwa moja yenye machotara, wazungu, wahindi, wachina na kadhalika. Sisemi kuwa wahindi hawapo, hapana. Badala yake ninataka kusema nchi hii itakuwa na mchanganyiko wa rangi mbalimbali ambazo zitakuwa ishara ya Tanzania mpya.

Hatutakuwa na Tanzania ya weusi pekee, bali tutakuwa nao akina Salim Ahmed Salim wengi tu, na hakuna kuwabagua. Kwa nini ninasema hayo? Jibu la swali hilo tunaweza kuangalia namna wazungu walivyokubali kuona mtoto mwenye asili ya Kenya, Barrack Obama akiwa raia wa Marekani.

Tunafahamu namna nchi ya Marekani waafrika walivyobaguliwa lakini inabidi wakiri kuwa mustakabali wao hauwezi kutenganishwa kwa rangi. Mwaka 2008 Barrack Obama alipata washabiki wengi barani Afrika. Ukanda wa Afrika mashariki ulisisimkwa mno na kupamba sifa kuwa mtoto wa kiafrika kuongoza Marekani.

Wengi waliisifu Marekani kwakuwa ilikuwa nchi iliyowapa uhakika kuwa kumbe kunawezekana kuwa na mtawala  yeyote bila kujali rangi yake. Wengi wakaamini kuwa hata mtu mweusi anaweza kutawala china au India. Wengi wanaamini kuwa mtu mweusi anaweza kutawala Uingereza.

Wapo watu wengi ndani ya nchi ambazo zinatawaliwa na wazungu ambao ni weusi wenye uwezo mkubwa na wanaweza kuja kuwa watawala wa mataifa hayo wakati wowote. Kwa hiyo wanapopewa mamlaka ya kutawala huko maana yake bado ni raia halali wa mataifa hayo siyo asili zao.

Ukiangalia Obama hadi sasa anavyoelekea kuhitimisha utawala wake inabidi sasa tuanze kurudi na kukumbushana kuwa je sisi  waafrika tutakuwa tayari kutawaliwa na rais mzungu?

Ni kwamba mwaka 2009 akiwa nchini Ghana, Obama alitaka kuwa mipaka ya dunia hii imevunjwa na mahusiano ya binadamu. Nami nakubaliana naye huku nikikumbuka ndoa iliyofungwa hivi karibuni huko mkoani Lindi inayomhusisha mwanamke mmoja wa Uingereza na raia wa Tanzania. Kwahiyo watakapopata mtoto huyo atakuwa raia wa Tanzania na ndiye hasa dhumuni la makala yangu ya leo kwamba kizazi cha aina hiyo hatuwezi kukitenga hata kidogo.

Naishamirisha hoja hiyo ya Obama aliyotoa Julai mwaka huo pale Accra nchini Ghana. Mantiki yake ilikuwa mwingiliano wa kijamii kama zama za kale. Bila Shaka alijitafsiri yeye kama mfano hai, ametokea asilia ya Afrika, anao ndugu Kenya na Marekani pamoja na Indonesia.  Maisha yake ni somo ambalo linatuletea hoja hii; wakati ukifika Tanzania itakuwa tayari kutawaliwa na mzungu, mchina, mwarabu na mhindi? Ni suala la kusubiri na kuona.

Mfano mwingine ni aliyekuwa mgombea uraiwa Gabon kwa kambi ya upinzani Jean Ping. Baba yake ametokea China, anaitwa Cheng Zhiping. Kwa maana hiyo Gabon wanacho kizazi kutoka Wenzhou kule China.

Tofauti ya Hussein Onyango Obama na Cheng Zhiping ni moja; Mzee Zhiping alikuwa raia wa Gabon na alipata kuwa diwani katika mji aliokuwa akiishi, lakini Hussein Onyango Obama alikuwa Mkenya.

Zhiping alioa binti wa Chifu huko Emboue nchini Gabon na kumzaa Jean Ping. Huyo Jean Ping anatambulika pia kama kijana mtiifu wa damu ya watu wa mji wa Wenzhou nchini China alikotokea baba yake.

Kwa maana hiyo China walikuwa na pa kuanzia Gabon baada ya mjukuu wao Jean Ping kuwa waziri wa mambo ya nje. Ndiyo maana dunia ikashuhudia ziara ya Rais wa China, Hu Jintao.

Wakati Hu Jintao akiwa nchini Gabon ndipo alipoutangazia ulimwengu Sera ya “kutokuwa na mpango wa kuingilia siasa za ndani, hapa kazi tu” za nchi washirika wake. Jean Ping amewahi kuwa Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU). Hivyo Jean Ping ingawa mzazi wake mmoja anatoka China, lakini alikuwa raia wa Gabon.

Kwa Afrika kusini watasema wamezoea mchanganyiko wazungu kuwa mawaziri au chotara Danny Jordan alivyoongoza kamati ya maandalizi ya kombe la dunia ya FIFA mwaka 2010.

Kama nilivyosema awali, wakati tunayaona mabadiliko hayo kwa wenzetu, hata hapa kwetu Tanzania wapo wengi tu, na wakati utafika hatuwezi kuwa na mustakabali wa peke yetu bila machotara au bila uchotara lakini raia halali kama akina Richard Mabala.

Yatakapokuja kwetu tusigombe, tukubali kutambua uraia wa wenzetu bila rangi au asili za kizazi chao. Watakuwa watumishi wetu kama Jean Ping na Gabon. Kwahiyo kuwashangilia akina Obama haitusaidii, bali tupate wa kwetu na tuwe tayari kuwachagua kama raia wetu na kuwapigia kura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles