24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

KUTOKA KAGAME, NKAMIA HADI MUSEVENI


NA MARKUS MPANGALA

VUGUVUGU la kuongeza miaka (muhula) ya kubaki madarakani limeshika kasi katika Ukanda wa Afrika Mashariki, unaojumuisha nchi za Uganda, Tanzania, Kenya, Sudan Kusini, Rwanda na Burundi.

Vuguvugu hilo lilianzia kwenye mijadala ya kikatiba ya kuongeza mihula ya kutawala. Rwanda walifanikiwa, Tanzania imeshindikana kwa muda na sasa Uganda Rais wake Yoweri Museveni amesaini muswada wa sheria inayoondoa ukomo wa umri.

Katiba ya Uganda inakataza raia wa nchi hiyo mwenye umri zaidi ya 77 kugombea kiti cha urais. Kulingana na umri wa Yoweri Museveni mwenye miaka 73, tayari hicho kilikuwa kikwazo chake cha kugombea urais katika uchaguzi ujao mwaka 2021. Lakini sasa ameruka kihunzi cha umri na kutaka kugombea tena urais wa Uganda ambao aliupata mara ya kwanza mwaka 1986.

RWANDA NA JUMA NKAMIA

Tukianzia nchini Rwanda, mwaka 2015 wananchi walipiga kura ya maoni kuamua iwapo wanaendelea na ukomo wa mihula miwili madarakani au waongeze. Kura hiyo ya maoni iliitishwa na Serikali ya Rais Paul Kagame, ikiwa ni njia ya kuhalalisha ongezeko la muda wa kukaa madarakani, ambaye aliingia mara ya kwanza mwaka 2000.

Kagame alifika tamati ya utawala wake ambapo alitakiwa kuondoka madarakani, lakini kura ya maoni ilimpa nafasi ya kugombea urais kipindi cha tatu. Katika kipindi cha kura ya maoni, wananchi wa Rwanda walitakiwa kukubali au kukataa kuwa muda wa rais kukaa madarakani upunguzwe kutoka miaka saba hadi mitano. Na kwamba ukomo wa urais nchini Rwanda baada ya uchaguzi mkuu wa 2024, utakuwa ni miaka mitano.

Rwanda walikuwa na sababu za msingi kutokana na historia ya nchi yao, hivyo ikakubaliwa uongozi uwe wa miaka 7.

Wakati Rwanda wakifanya mabadiliko hayo ya kikatiba wakiwa na sababu za kihistoria pamoja na hali ya nchi yao, kwa upande wa Tanzania aliibuka Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia ambaye alijiandaa kupeleka hoja binafsi bungeni ili kufanyika mabadiliko ya kikatiba, ambapo muda wa mbunge ungeongezwa kutoka miaka mitano hadi saba.

Nkamia alileta ajenda mezani kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, ya kuomba kuwasilisha hoja binafsi ya mabadiliko ya kisheria ya ukomo wa nafasi ya ubunge kutoka miaka mitano kwenda miaka saba.

Kwa mtazamo wa Nkamia, aliona muda wa ubunge wa miaka mitano hautoshi, kwa hiyo ingefaa kufanyiwa mabadiliko ya kisheria na Bunge litamke kuwa muda wa ubunge utakuwa miaka saba.

Jambo hilo lilikuwa likidodoswa mara kadhaa tangu miaka ya nyuma, lakini kitu kimoja kilichokwamisha ni kutoyumba kwa misingi ya nchi juu ya ukomo wa nafasi ya urais au ubunge.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuonya juu ya hatua za aina hiyo hata kama tunajaribu kujidanganya mara kwa mara kwamba yeye si msahafu.

Kupitia kitabu chake cha ‘Uongozi Wetu na Hatima ya Nchi yetu’, anaandika: “Rais alieleza kuwa walikuwa wamekubaliana kwamba vipindi vya kuwa rais ni lazima vitamkwe, lakini walikuwa hawajaafikiana uamuzi viwe vipindi vingapi. Awali baadhi ya viongozi wa chama walikuwa wameanza kampeni za kutaka Rais Mwinyi aongezewe vipindi vya muda wa kuwa rais.

“Nilipotambua hivyo, nilikuwa nimekwenda mara moja kwa rais na kumsihi azizime kampeni hizo na viongozi wahusika nilitafuta nafasi nao, nikawaomba wasilifufue jambo hili. Nikadhani tumeelewana hivyo. Kwa hiyo nilishtuka niliposikia kuwa kumbe suala hilo la vipindi vya urais bado linazungumzwa na ati bado uamuzi wa vipindi vingapi haujafikiwa!” (Uk.9).

Katika ukurasa wa 12 wa kitabu hicho hicho, Mwalimu Nyerere anaeleza: “Suala hili lilikwishakuamuliwa zamani na sasa ni sehemu ya Katiba yetu. Uamuzi huo inafaa uheshimiwe. Rais Mwinyi ndiye rais wa kwanza kuchaguliwa kwa mujibu wa Katiba hiyo. Yeye akisema kuwa vipindi viwili havitoshi na akataka viwe vitatu; rais wa pili atasema vipindi vitatu havitoshi na atataka viwe vinne na kadhalika mpaka tufikie Ngwazi wa Tanzania.”

KESI YA KIKATIBA KUUNGURUMA UGANDA

Kama tulivyoeleza awali kuwa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, anajiandaa kugombea urais katika muhula wa tatu mwaka 2021, akiwa amefanikiwa kuondoa kipengele katika Katiba yao kinachokataza raia yeyote mwenye miaka 77 kugombea urais.

Licha ya kufanikiwa kusaini muswada huo na kuwa sheria, vyama vya upinzani vimeamua kwa kauli moja  kufikisha malalamiko yake mahakamani nchini humo.

Wabunge wa upinzani wanatarajiwa kuwasilisha maombi yao kwenye Mahakama ya Katiba kuiomba kutoidhinisha sheria ambayo Rais Museveni aliidhinisha hivi karibuni.

Mageuzi hayo ya kikatiba yaliondoa kikomo cha umri wa rais, hii inamaanisha kuwa Rais Museveni yupo madarakani tangu mwaka 1986, atawania katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2021. Wakati huo atakuwa ametimiza rasmi umri wa miaka 77. Upinzani haupingi tu matokeo, lakini utaratibu, wabunge waliopigwa au kulipwa, askari waliojihami kwa silaha kuletwa ndani ya jengo la Bunge.

Licha ya hekaheka hizo kutikisa mfumo wa demokrasia nchini humo, Jumuiya ya kimataifa imefumbia macho uvurugaji wa Katiba unaofanyika nchini Uganda. Upinzani nchini Uganda na mashirika ya kiraia yamekosoa mwenendo huo wa jumuiya ya kimataifa.

Hali hii imeendelea kushuhudiwa nchini Uganda kukiwa na kumbukumbu ya mwaka 2005, ambapo Rais Museveni alijaribu kufanya mageuzi ya Katiba bila wasiwasi wowote wala kuchukuliwa vikwazo vyovyote, wakati ambapo angeliweza kuwania kwa muhula wa pili, kulingana na Katiba ya wakati huo. Rais Museveni hajachukuliwa vikwazo ndani na nje ya nchi na hivyo kuvunja sheria, jumuiya ya kimataifa ikishuhudia.

Mwanadiplomasia mmoja aliyezungumza na redio moja ya kimataifa kwa sharti la kutotajwa jina lake, ameonya kwa kusema: “Rais Museveni ni kama Rais wa Rwanda, Paul Kagame, anaua bila wasiwasi, anavunja sheria, anaiba mali za DRC, akiungwa mkono na Marekani, huku nchi kama hizo zikiendelea kupata misaada.”

MUSEVENI KIPENZI CHA MAREKANI

Ingawa wanasiasa wa upinzani nchini Uganda wanailalamikia Jumuiya ya Kimataifa hususani mataifa ya Marekani, Uingereza na Ufaransa, lakini inafahamika kuwa Rais Museveni ni kipenzi cha utawala wa vyama vyote viwili vilivyoongoza nchini Marekani; Democrat na Republican.

Hii ni hoja ambayo Mtafiti na Mwandishi wa Habari, Helen Epstein, ameeleza katika kitabu chake kijulikanacho kama ‘Marekani, Uganda na vita dhidi ya ugaidi’, ambacho kwa kimombo kinaitwa ‘Another Fine Mess: America, Uganda, and the War on Terror.’

Kuanzia miaka ya kwanza, baada ya mapinduzi, Rais Museveni alijiweka karibu na Marekani, mwanafunzi mzuri wa vita dhidi ya ugaidi hata kabla ya tukio baya lililotokea Septemba 11 nchini Marekani. Tangu wakati huo, amepokea jumla ya dola bilioni 20 za misaada ya maendeleo, dola bilioni 4 ya kufuta madeni, msaada wa kijeshi, wa kifedha, vifaa, mafunzo, labda muhimu sana haijulikani kiwango.

Na msaada huo si kutoka tu Marekani, hata Uingereza au Ufaransa, wanaisadia Uganda katika nyanja mbalimbali. Na kutokana na misaada hiyo, Jeshi la Uganda linachukuliwa kwa sasa kama jeshi lenye nguvu zaidi barani Afrika, licha ya vitendo viovu linaloshtumiwa. Jeshi hili pia limefanikiwa kiasi kikubwa kutokana na kutumwa kwake nchini Somalia dhidi ya wapiganaji wa Al Shabab.

“Museveni kama Kagame, ni moja ya nguzo muhimu ya utulivu, hata kama ni maono ya muda mfupi,” chanzo cha kidiplomasia kimepongeza.

Kwa upande wa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani katika Bunge la Uganda, Ibrahim Ssemujju, anasema hali hiyo haishangazi na hatarajii chochote kutoka jumuiya ya kimataifa.

“Wakati Museveni anatuma askari nchini Somalia kupambana katika vita vyao, jumuiya ya kimataifa inafumbia macho kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu au sheria nchini Uganda. Kwa hiyo, hatuwezi kutarajia msaada wowote kutoka kwa nchi hizi, hatuna matumaini yoyote ya msaada kutoka kwao,” anasema.

Wachambuzi wa masuala ya siasa nchini Uganda wanasema huenda hata uamuzi wa Serikali ya Rais Museveni kusaini muswada huo na kuwa sheria hautakuwa na maana yoyote mbele ya jumuiya ya kimataifa, kwani hawataweza kuzungumza chochote kwa kiongozi anayependwa kwa kulinda masilahi yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles