JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA
WAKATI inaweza kuonekana kama kitu cha kuogopesha, kwa mtawa huyu wa Shaolin nchini China hakuna kitu kama hicho.
Hapenywi na kitu chochote chenye ncha kali katika mwili wake kutokana na ngozi yake ngumu iliyotokana na mazoezi ya tangu akiwa mdogo.
Anaonesha namna alivyoweza kufanyia mazoezi mwili wake kuhimili vitu vyenye ncha kali.
Katika mfululizo wa maoneshao anayofanya ambayo haishauriwi kwa yeyote kuyajaribu, Zhao Rui huishindilia mashine ya umeme ya kutoboa kwenye kichwa chake bila kupenya kwenye ngozi.
Huweza kukunja nondo kwa kutumia koo, kulalia tumbo kwenye ncha za mikuki na hata kuvunja mawe kwa kutumia kichwa chake.
Kwa mujibu wa mtandao wa People’s Daily, Zhao hushikilia mashine hiyo ya kutobolea vitu yenye nguvu kwa sekunde 10, lakini ikiacha doa dogo jekundu pale ilipogandamizwa.
Onesho hulenga kuonesha namna kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 alivyoweza kuufanyisha mazoezi mwili wake tangu utotoni.
Mazoezi hayo yalihusisha mafunzo ya sanaa ya mapigano ya mikono – na ujuzi wake umemfanya kuwa nyota katika jiji la nyumbani kwake la Mianzhu katika jimbi la kusini magharibi mwa China la Sichuan.
Lakini kijana huyo alikiri kuwa kwa bahati mbaya aliwahi kutoboa shimo katika kichwa chake wakati akifanya onesho, akachana sehemu ya ngozi.
Anasema: “Iliuma sana lakini nilipona na kujifunza namna ya kukabiliana nayo na sasa naweza kufanya kitendo hicho mara kwa mara bila matatizo yoyote.”
Na kuthibitisha hilo kwa mwandishi alishikilia mashine ya umeme ya kutoboa dhidi ya kichwa chake kwa sekunde 10 bila matatizo.
Shuhuda Lian Tang (25) anasema: “Ilishangaza kwa sababu baada ya kuondoa mashine ya kutobolea, hakukuwa na damu bali alama ya wekundu eneo ambalo mashine ya kutobolea iligandamizwa.”
Mtaalamu huyo wa kung’fu alianza kujifunza sanaa za mapigano tangu akiwa mtoto baada ya kuvutiwa nayo na katika umri wa miaka 16 alitoroka nyumbani kwenda kujiunga na Hekalu la Shaolin.
Alitaka kujifunza Sanda (aina ya mchezo wa mateke (kick-boxing) wa Kichina na ‘hard Qigong’, ambayo huvuta nguvu kutoka kani ya nishati kutokea ndani inayoitwa qi.
Alichukua mafunzo hapo kwa miaka miwili kabla ya kuondoka kuendelea na masomo akijifunza kung’fu kutoka kwa wataalamu mbalimbali wa sanaa hiyo ya mapigano na sasa amekuwa mwalimu mtaalamu wa kung’fu.
Matumizi ya mashine hiyo ya kutobolea ni moja ya maonesho na mazingaombwe anayofanya kuonesha utaalamu, ujuzi na umahiri wake.
Aidha, huwezi kukamata msumeno wa umeme unaozunguka kwa mikono mitupu bila kupata madhara yoyote.
Anasema: “Niliamini katika kuufanya mwili wangu uwe mgumu. Amini usiamini nilikuwa na shaka nikiwa mdogo lakini sasa naweza kuvunja mawe kwa kichwa changu, na hili limenipa hali ya kujiamini.”
Pia ana uwezo wa kurusha sindano mithili ya risasi na kuzuia kisu kwa mikono mitupu.
Kufikia mwaka juzi, tayari anashikilia rekodi tatu tofauti za dunia kwa mujibu wa Kitabu cha Guinness World Records.
Zhao Rui si mtu pekee mwenye uwezo huo, huko nyuma mwaka 2010, Hu Qiong, pia mtawa wa Shaolin aliyepewa jina la ‘mwanaume wa chuma’ aliteka vichwa vya habari duniani kwa kuonesha umahiri kama huo.