NAIROBI, KENYA
KURA mpya ya maoni iliyoendeshwa na taasisi Ipsos imeonesha Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga wakizidi kukabana koo.
Kiwango cha kukubalika cha Kenyatta kimeshuka kwa asilimia moja huku cha Odinga kikipanda kwa asilimia hiyo, matokeo ya kura hiyo yaliyotolewa jana yameonesha.
Kenyatta anaungwa mkono na asilimia 47 ya Wakenya, ikiwa imeshuka kutoka asilimia 48 mwishoni mwa Juni huku Odinga akiungwa mkono kwa asilimia 43 kutoka asilimia 42.
Utafiti umeonesha asilimia tano ya Wakenya hawajaamua wa kumpigia kura huku baadhi wakipanga kutoshiriki kura na wengine wakifikiria kuwapigia kura wagombea wengine wasio maarufu.
Iwapo mchuano huo utahusisha wagombea wawili tu Kenyatta atapata asilimia 52 ya kura huku Odinga asilimia 48 ya kura iwapo uchaguzi ungefanyika sasa.pao .
Kuhusu wagombea wenza, Kalonzo Musyoka ameonekana kuwa silaha muhimu kwa Odinga kwa vile Wakenya wana imani naye kulinganisha na mgombea mwenza wa Kenyatta, William Ruto.
Asilimia 34 ya Wakenya wana imani na Musyoka wakati asilimia 33 wanaamini Ruto naweza kufanya kazi nzuri kama namba mbili wa Kenya.
Utafiti pia unanesha kuwa asilimia 61 ya wakenya wanahisi taifa hili liko katika mwelekeo usio sahihi huku asilimia 27 tu wakiamini liko mwelekeo sahihi.
Mtafiti Mkuu wa wa Ipsos, Tom Wolf ameondoa uwezekano wa uchaguzi wa marudio akisema utakuwa wa raundi moja na kuwa mwitikio mkubwa wa kura ndiyo utakaoamua mshindi baina ya Kenyatta na Odinga.