24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

MWIJAGE AWATAKA WATANZANIA KUWA WABUNIFU

Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam


WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji , Charles Mwijage amesema ili kufanikisha mpango wa uchumi wa viwanda katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni vyema Watanzania kuongeza ubunifu na kuutunza.

Mwijage aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, wakati akifungua semina ya siku mbili iliyoandaliwa na Shirika la Kusimamia Mali za Ubunifu la Kanda ya Afrika(ARIPO) na kuwashirikisha wadau mbalimbali kutoka mashirika, vyuo na taasisi za Serikali.

Alisema mkutano huo ni mkubwa kwa Tanzania ikiwa ni wenyeji na kwamba umefanyika wakati mwafaka kwa kuwa nchi ipo kwenye mpango wa miaka mitano kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea ukuaji wa viwanda.

“Ubunifu lazima ulindwe kwani usipolindwa unaweza ukabuni na kutengeneza kitu saa sita mchana wengine wakawa wameshakopi huku wewe ukiwa umetumia muda mwingi na gharama za kubuni bidhaa husika,’’alisema Mwijage.

Alisema ni vyema watanzania kuwa wabunifu na kuutunza ubunifu wao ili kutengeneza ajira nyingi kupitia sekta hiyo na kuzalisha  faida.

Alisema, katika semina hiyo wataalamu watawaelewesha wadau masuala ya ubunifu na jinsi ya kuutunza ubunifu wao ambapo walengwa ni makampuni madogo, wazalishaji wa mbegu na mimea, watu wa utamaduni na watunzi lengo likiwa ni kuwasaidia kufanya uzalishaji wa ubunifu wao kwa tija kwa kuwa na milki.

Hata hivyo aliwataka watendaji wa Chama cha Hakimiliki Tanzania(COSOTA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni(BRELA) pamoja na Ofisi ya Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa aina Mpya za Mbegu za Mimea(PBRO)  kufanya vizuri zaidi ili nchi ipate faida na kutengeneza ajira nyingi kupitia sekta ya ubunifu.

Kwa upande wake Kaimu Msajili wa  Hakimiliki za Wagunduzi wa aina mpya za mbegu za mimea (PBRO) ,kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Joyce Mosile alisema ni vyema wagunduzi wa mbegu kuendelea kugundua mbegu bora ambazo zitaendana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyopo kwa sasa.

Alisema ni vyema kuhakikisha kwanza kunawekwa nguvu milki bunifu hasa kwa wabunifu wa aina mpya za mbegu ili kupata mbegu bora za mimea na kupata chakula ili na kuviwezesha  viwanda kupata malighafi za kutosha.

Alisema tayari kwa sasa wanajumla ya maombi ya mbegu 76 kati ya hizo 73 tayari zilishapatiwa hakimiliki huku akiwataka watafiti na wagunduzi wengine kuendelea kutafiti.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Doreen Sinare alisema  ni vyema wabunifu wote wakaingia katika mpango wa Hakimiliki ili uweze kuwasaidia kazi zao zisiweze kuibiwa na mtu mwingine kwa kuwa teknolojia ya sasa imekuwa zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles