24.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

‘KUPENDA KUPITA KIASI NI SAWA NA UTEJA’

Na MWANDISHI WETU – dar es salaam

KUPENDA kupita kiasi kumetajwa kuwaathiri watu kama ilivyo kwa watumiaji wa dawa za kulevya.

Akielezea uhusiano uliopo kati ya kupenda na matumizi ya dawa za kulevya, daktari wa magonjwa ya kawaida, Joachim Mabula, alisema kuwa anayependa huathirika kisaikolojia kama wanavyoathirika mateja.

“Kupenda kunaweza kukusababishia furaha, kukukarahisha na wakati mwingine kukufanya uugue. Dawa za kulevya, sigara na bangi navyo pia hufanya hivyo,” alisema.

Dk. Mabula alisema upendo na dawa zenye kuleta uraibu (addiction) hufanana njia zake za utendaji.

Alisema mwanamume anapokaa karibu na mwanamke anayevutia kwa muda wa dakika tano tu peke yao, huongeza viwango vya cortisol – yaani homoni ya mkazo.

“Kuna utafiti ulifanyika katika Chuo Kikuu cha Valencia nchini Hispania ambao ulibaini kuwa madhara huwa makubwa zaidi kwa mwanamume anayedhani mwanamke anayevutia mbele yake si wa hadhi yake,” alisema na kuongeza:

“Watafiti waliwapima wanafunzi wa kiume 84 kwa kila mmoja kukaa katika chumba na kumpa zoezi la kutatua fumbo la Sudoku. Katika kila chumba alichowekwa mwanafunzi kulikuwamo pia wageni wawili, mmoja wa kiume na mwingine wa kike.”

Alisema mgeni wa kike alipoondoka chumbani na kubaki wanaume wawili waliokaa pamoja, viwango vya msongo vya aliyepimwa vilikuwa chini, lakini alipoachwa mwanamume na mwanamke, viwango vyake vya msongo vilikuwa juu zaidi.

Dk. Mabula alisema kuwa utafiti huo ulibaini pia kuwa mwanamume akiwa na mwanamke mwenye kuvutia, anaweza kudhani kwamba kuna fursa ya uchumba/kutongoza.

“Utafiti huo pia umeonesha kuwa baadhi ya wanaume nao huepuka wanawake wenye kuvutia kwa kufikiri kuwa hawana hadhi ya kuwamiliki. Wengi hupatwa na wasiwasi hata bila ya wao kujua,” alisema.

Dk. Mabula alisema kuwa utafiti huo pia ulibaini kuwa viwango vya homoni mkazo kwa mwanamume huongezeka baada ya dakika tano ya kukutana na mwanamke kijana mwenye kuvutia.

Alisema kuwa ongezeko sugu la homoni mkazo pia linaweza kusababisha hali mbaya kiafya kama vile ugonjwa wa moyo, kisukari, shinikizo la damu na ugumba.

“Hivyo basi, upendo umebainika kuwa ni dawa za kulevya na kuvunjika moyo ni njia ya mwili kutoa dawa hiyo mwilini,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles