KLABU ya soka ya Real Madrid imedaiwa kushindwa kumsajili mshambuliaji wa timu ya Barcelona, Lionel Messi, baada ya kujaribu kwa miaka mitatu mfululizo ndani ya miaka mitano iliyopita.
Kwa mujibu wa kituo cha redio cha mjini Madrid, Partido de las Doce, kilichokuwa kwenye programu ya Cadena COPE, kilielezea ripoti ya  klabu hiyo juu ya kujaribu kumsajili mchezaji huyo mwaka 2011, 2013 pamoja na 2015, lakini alikataa.
Messi mwezi huu alifanikiwa kushinda tuzo ya tano ya Ballon d’Or na kutajwa kwamba ni mchezaji mwenye mafanikio makubwa katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, Primera Division pamoja na Copa del Rey.
Ripoti hiyo ilidai kwamba mbinu ya kwanza iliyofanyika mwaka 2011 ilikuja wakati mwafaka kwa Cristiano Ronaldo, akihusishwa na kuhamia Manchester City.
Juni mwaka 2013 iliripotiwa kwamba Mtendaji Mkuu wa Real Madrid, kupitia kwa rais wa klabu hiyo, Florentino Perez, alishindwa harakati za kumsajili Neymar Jr.
Jaribio la mwisho lilifanywa mwaka jana kwa mujibu wa ripoti hiyo, baada ya Barcelona kuwa kinara mbele ya Real barani Ulaya na Ligi ya nyumbani, lakini mbinu yao iligonga mwamba.
Hata hivyo, hatua hiyo kati ya mahasimu hao wa jadi ilionekana kuwa nadra kutokea, hasa kwa klabu hiyo inayoongozwa na kocha Luis Enrique, ambaye akiwa mchezaji alijiunga na klabu hiyo mwaka 1996, akitokea Rea Madrid, ambapo miaka minne baadaye Perez aliweza kumsajili Luiz Figo akitokea Barcelona.
Kuondoka kwa Figo kulisababisha ghasia Catalonia na kumzonga kwa kila aina ya hila pamoja na kutupiwa kichwa cha nguruwe aliporudi Camp Nou akiwa mchezaji wa Real Novemba 2002.
Mmoja kati ya nguli wa timu ya Real, Alfred Di Stefano, awali alitaka kusaini timu ya Barcelona mwaka 1953, lakini ilikuwa vigumu kufanya hivyo baada ya kutokea mzozo juu ya uwepo wake Real, ambapo Shirikisho la Soka Hispania liliingilia kati na kuamua mchezaji huyo kujigawa katika kila msimu ili kuzichezea klabu hizo.
Barcelona ilijiondoka katika makubaliano hayo na Di Stefano alikuwa huru kusaini kuichezea Real ambapo baadaye iligundulika kuwa ilikuwa njama ya Serikali iliyokuwa chini ya Franco ili mchezaji huyo kubaki katika timu hiyo.