30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu mpya KKKT aonya utumbuaji majipu

IMGS2134Amtahadharisha Rais Magufuli kutumbua majipu kwa haki,busara

Asema Bunge ni nyumba ya demokrasia, haipaswi kulindwa na jeshi

UPENDO MOSHA NA SAFINA SARWATT, MOSHI

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, amemtahadharisha Rais Dk. John Magufuli kuwa kazi ya utumbuaji majipu aliyoanza nayo inapaswa kufanywa kwa kufuata misingi ya haki na busara ili kuepuka watu wasiokuwa waaminifu kutumia mwanya huo kuwaonea wenzao wasiokuwa na hatia.

Akizungumza mbele ya mamia ya waumini wa kanisa hilo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro jana, wakati wa ibada maalumu ya kuingizwa kazini kuwa mkuu wa kanisa hilo, Askofu Shoo alisema kazi ya utumbuaji wa majipu inahitaji hekima na busara ya ki-Mungu na kwamba ifanyike kwa kufuata misingi ya haki pasipo kuwaonea watu wasiokuwa na hatia

“Tuna imani na uongozi wa Serikali ya awamu ya tano na katika kipindi hiki kifupi tumeona juhudi za Serikali katika utumbuaji wa majipu. Utumbuaji huu ufanyike katika misingi ya haki na kwa busara kwani watu wengine wanaweza kutumia mwanya huu kuonea wenzao wasiokuwa na hatia,” alisema.

Mbali na hilo, aliipongeza Serikali ya Dk. Magufuli katika utendaji wake wa kuendelea kuwachukulia hatua watendaji wa Serikali ambao wamekuwa wakijihusisha na ubadhirifu wa mali za umma na ufisadi.

Alisema kwa msingi huo, kanisa hilo bado litaendelea kukemea na kuonya mifumo kandamizi kwa lengo la kujenga maadili mema, upendo, haki na ushirikiano ili kuleta maendeleo ya dhati katika nchi.

Katika hatua nyingine, Askofu Shoo ameonyesha kusikitishwa na vitendo vya ukiukwaji wa maadili na utovu wa nidhamu vinavyofanywa na baadhi ya wabunge katika vikao vinavyoendelea mjini Dodoma.

Kutokana na hali hiyo, Askofu Shoo amewataka wabunge kuendesha vikao vyao kwa kufuata maadili na kuacha mara moja tabia ya utovu wa nidhamu inayojitokeza katika vikao hivyo.

Ibada hiyo ilihudhururiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, dini na Serikali.

Askofu Shoo alisema Bunge ni mhimili ambao haupaswi kuingiliwa na mhimili mwingine, lakini kanisa hilo linasikitishwa na vitendo vya utovu wa nidhamu  vinavyoendelea kufanywa na baadhi ya wabunge.

“Tunahitaji kuona Bunge linajadili vikao vyake kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia. Kanisa linasikitishwa sana na vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyoendelea bungeni, tunapenda kuona hoja zinajadiliwa kwa ustaarabu,” alisema.

Askofu Shoo alisema Watanzania wanatarajia kusikia na kuona hoja zinajadiliwa kwa uwazi, hivyo wabunge wana wajibu wa kulinda heshima zao wanapojadili mambo muhimu ya maendeleo na mustakabali wa nchi.

Alisema Bunge ni nyumba ya demokrasia na kamwe haipaswi kulindwa na jeshi.

Wiki iliyopita vurugu kubwa ziliibuka bungeni, baada ya wabunge wa kambi ya upinzani kutaka kauli ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye kuhusu kutorushwa moja kwa moja kwa matangazo ya Bunge ijadiliwe.

Katika vurugu hizo, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliingia ndani ya ukumbi wa Bunge na kuwalazimisha wabunge wa upinzani kutoka nje.

Baadhi ya wabunge wakiwamo, Susan Kiwanga wa Kilombero na Halima Mdee wa Kawe waliburutwa kwa nguvu na askari hao.

wakati huohuo, Askofu Shoo aliitaka Serikali kuanzisha upya  mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya itakayoheshimu matakwa ya wananchi wote na kuondoa mifumo kandamizi.

Alisema Watanzania wanahitaji Katiba isiyoangalia udini, ukabilia na itikadi za kisasa ambapo kwa namna moja au nyingine, mambo hayo yanaweza  kuligawa taifa na kusababisha uvunjifu mkubwa wa amani.

Kuhusu suala la elimu, Askofu Shoo aliitaka Serikali kutazama upya sera ya elimu bure na kuboresha shule zake.

Alisema iwapo hatua hiyo itafanyika, hakutakuwa na haja ya kupanga ada elekezi katika shule binafsi kwa kuwa shule za umma zitakuwa na mahitaji yote muhimu yatakayomwezesha mwanafunzi kupata elimu bora.

Aliitaka Serikali kufufua viwanda vilivyokufa kwa lengo la kuzalisha bidhaa zinazotakiwa nchini ili kupunguza kasi ya uagizaji wa bidhaa nje ya nchi, kwani asilimia kubwa zimekuwa feki.

“Serikali ijenge viwanda ili tuzalishe biadhaa zetu wenyewe na kupunguza kasi ya uagizwaji wa bidhaa kutoka nje, jambo hili litasaidia kukuza uchumi wetu na wananchi kuondoka katika hali ya umaskini,” alisema

Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema Serikali itaendelea kuheshimu michango mbalimbali inayotolewa na taasisi za dini, ikiwamo katika sekta ya elimu na afya.

Alizitaka taasisi za dini kundelea kushirikiana na Serikali katika kuwekeza katika maeneo muhimu kama afya na elimu ili kuboresha utoaji wa huduma katika jamii.

“Napenda kutumia fursa hii kuyashukuru madhehebu ya dini ambayo yamekuwa msitari wa mbele kuisaidia Serikali katika kufikisha huduma hizi za afya karibu zaidi na wananchi. Wito wangu kwa hili, naombeni mjitahidi kutoa huduma hizi kwa gharama nafuu ili wananchi wengi wapate kuzitumia,” alisema.

Naye Askofu Mkuu mstaafu wa kanisa hilo, Dk. Alex Malasusa, akimuingiza kazini Askofu Shoo, alimtaka kuongoza kanisa hilo kwa uaminifu na uadilifu, ikiwa ni pamoja na kuacha kufumbia macho maovu yanayofanyika katika jamii.

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa Katoliki  Jimbo la Moshi, Mhashamu Isack Amani, aliwataka Watanzania kuwa na moyo wa uzalendo na kuipenda nchi yao, ikiwamo kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles