Na MWANDISHI WETU – Dar es Salaam
UAMUZI wa Idara ya Uhamiaji kuhoji uraia wa baadhi ya watu maarufu baada ya kutoa kauli, tafiti au kuonyesha mwenendo ambao baadhi wanaona una taswira kinzani na upande wa Serikali, umezua mjadala huku wasomi na wafuatiliaji wa mambo wakiuponda.
Tukio lililoamsha mjadala huo ambao huibuka na kupotea mara kwa mara, ni uamuzi mpya wa idara hiyo kuhoji uraia wa Mkurugenzi wa Taasisi inayojishughulisha na tafiti ya Twaweza, Aidan Eyakuze.
Kabla ya Eyakuze, hivi karibuni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo, alihojiwa na Uhamiaji kuhusu uraia wake, ikiwa ni siku chache baada ya kushtakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa kwa kuwapo taarifa za kudai ametekwa.
Ikumbukwe kuwa Nondo alipata umaarufu wakati wa kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline, alipoibuka na kauli za kukemea mauaji na hata kutaka Waziri wa Mambo ya Ndani ajiuzulu.
Mbali na tukio hilo, inadaiwa Nondo alianza kupokea vitisho na kisha inaelezwa aliwahi kukamatwa na polisi eneo la Milimani City, Dar es Salaam, akituhumiwa kufanya uchochezi kwa baadhi ya wanafunzi waliokosa mikopo ya elimu ya juu.
Ukiachilia mbali tukio la Nondo, pia Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Katoliki la Rulenge, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Severine Niwemugizi, aliwahi kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji  kuhusu uraia wake.
Askofu huyo alihojiwa siku chache baada ya kukaririwa akisema yupo tayari kuitwa mchochezi kutokana na msimamo wake wa kutaka Katiba Mpya.
Watu wengine ambao walihojiwa kuhusu uraia wao ni mwanahabari mkongwe, Jenerali Ulimwengu ambaye inadaiwa alikumbana na mapito hayo magumu baada ya kuandika habari katika moja ya magazeti ya kiingereza hapa nchini iliyokuwa imeanika ukweli juu ya taarifa ya mke wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Dk. Hassy Kitine, aliyekuwa amepelekwa nje ya nchi kutibiwa.
Mwingine ni Mkurugenzi wa Kituo cha Utetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olegurumwa ambaye kuchunguzwa kwa uraia wake kulihusishwa na majukumu ya taasisi anayoiongoza ambako amesikika mara kwa mara akitoa matamko mazito ya kutetea haki za watu.
Pia Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) Zacharia Kakobe, aliwahi kukumbwa na dhahama hiyo ikiwa ni siku chache baada ya kusema ana pesa kuliko Serikali.
Mbali na Askofu Kakobe, pia Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda, naye inadaiwa alichunguzwa uraia wake siku za nyuma wakati akiongoza vuguvugu la kudai mali za Waislamu.
Mwingine ni aliyekuwa Mwandishi wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), Kabendera Shinani, ambaye kutokana na majukumu yake ya habari, alipata misukosuko ya kuchunguzwa uraia wake na aliamua kujitosa ndani ya Ziwa Victoria na ukawa mwisho wa maisha yake.
WASOMI WANENA
Kwa msingi huo, baadhi ya wasomi na wafuatiliaji wa mambo wamekosoa mwenendo wa Idara ya Uhamiaji kuchunguza baadhi ya watu muda mfupi baada ya kuwa wametoa kauli zinazoonekana kukinzana na matakwa ya upande wa Serikali, wakisema ni aina mojawapo ya ukandamizaji wa haki za watu.
Kwa habari zaidi jipatie nakala yako ya gazeti la MTANZANIA.